Israel yatanua mashambulizi dhidi ya Hezbollah – DW – 21.10.2024

Kusini mwa Lebanon, mashambulizi ya anga ya Israel yaliyalenga matawi taasisi ya Al-Qard Al-Hassan  katika miji ya Nabatiyeh na Tyre. Taarifa iliyotolewa na jeshi la Israel mapema jumatatu imedai kwamba maeneo kadhaa ya taasisi hiyo yakiwemo matawi yake ya benki yalikuwa yakitumiwa na wapiganaji wa Hezbollah.

Mashambulizi hayo yanaashiria kutanuka kwa vita vya Israel dhidi ya Hezbollah katika kupunguza uwezo wa kundi hilo kuendesha operesheni zake.

Taasisi hiyo inafahamika kwa kutoa mikopo nchini Lebanon ambako mifumo ya kawaida ya kibenki ilisambaratika miaka mitano iliyopita kutokana na mgogoro mbaya wa kiuchumi.

Mashambulizi ya Israel yanayoendelea yamesababisha pia kuuwawa kwa wanajeshi watatu wa Lebanon. Israel imeomba radhi kwa mauaji hayo na kusema kuwa haipambani na serikali ya Lebanon bali wapiganaji wa Hezbollah.

Soma zaidi: Hezbollah yavurumisha makombora na kuua askari 4 wa Israel

Wakati mashambulizi hayo yakiripotiwa, mjumbe wa Marekani Amos Hochstein atafanya mazungumzo na maafisa wa Lebanon mjini Beirut kuhusu masharti ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo viwili vilivyoliarifu shirika la habari la Reuters.

Beirut, Lebanon baada ya shambulio la anga la Israel 11.10.2024
Sehemu ya madhara ya mashambulizi ya anga ya Israel mjini BeirutPicha: Louisa Gouliamaki/REUTERS

Licha ya ziara hiyo inayolenga kushinikiza kurejesha utulivu baada ya mwaka mmoja wa mapigano ambapo Israel imewauwa viongozi wa juu wa Hezbollah na Hamas, Marekani imeweka wazi kuwa inaiunga mkono Israel.

Kwingineko katika Ukanda wa Gaza msemaji wa jeshi la Israel  Daniel Hagari alitangaza kuuwawa kwa Kamanda wake  Ehsan Daska aliyekuwa kwenye operesheni ya kijeshi katika eneo la Jabalia.

Daksa, ni mmoja wa makamanda wa ngazi ya juu wa Israel kuuwawa katika vita vya zaidi ya mwaka mmoja vinavyoendelea Gaza. Wakati huohuo jeshi la Israel limesema limeyaruhusu malori 50 ya msaada wa kiutu yanayotoka Jordan kuingia Gaza wakati Israel ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa Marekani kuharakisha uingizwaji wa misaada  Kaskazini mwa Ukanda huo. Wakaazi wa eneo hilo wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiutu kutokana na vita vinavyoendelea.

 

 

Related Posts