Mpinzani wa Erdogan, Gulen, afariki uhamishoni Marekani – DW – 21.10.2024

“Vyanzo vyetu vya intelijensia vinathibitisha kifo cha kiongozi wa shirika la FETO,” Waziri wa Mambo ya Nje, Hakan Fidan, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari, akitumia neno la Uturuki kumaanisha vuguvugu maarufu la Gulen linalomiliki shule, biashara, na mashirika ya hisani.

Televisheni ya umma ya Uturuki, TRT, ilisema kuwa mhubiri huyo, ambaye ameishi Pennsylvania kwa robo karne na alienyang’anywa uraia wake wa Uturuki mwaka 2017, alifariki hospitalini usiku.

Habari hizo zilichapishwa kwanza kwenye X na Herkul, tovuti ya Gulen ambayo imepigwa marufuku nchini Uturuki, ikisema alifariki “tarehe 20 Oktoba.”

“Mheshimiwa Fethullah Gülen, ambaye alitumia kila dakika ya maisha yake akihudumia dini takatifu ya Uislamu na ubinadamu, amefariki leo,” iliandika, ikiahidi kutoa maelezo ya mazishi yake.

Soma pia: Jaribio la mapinduzi lazimwa Uturuki zaidi ya 250 wauwawa

Gulen alihamia Marekani mwaka 1999, kwa madai ya sababu za kiafya. Kutoka hapo aliongoza shirika la Hizmet, lenye mtandao mpana wa shule za umma katika kila bara.

Uturuki | Rais Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa shwahiba wake Fethullah Gulen kabla ya wawili hao kugeuka maadui wakubwa.Picha: Turkish Presidency/AP/picture alliance

Lakini shirika hilo kwa muda mrefu limewekwa kwenye orodha ya mashirika yaliopigwa marufuku na mamlaka za Uturuki, ambazo zinaiita FETO kuwa shirika la kigaidi la Fethullah (FETO).

“Shirika hili limekuwa tishio ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya taifa letu,” alisema Fidan, akiwashutumu wafuasi wake kwa “kutumika kama silaha dhidi ya nchi yao.”

Na Waziri wa Sheria, Yilmaz Tunc, alisema vita vya Uturuki dhidi ya vuguvugu hilo vitaendelea, licha ya kifo cha Gulen.

“Vita dhidi ya shirika hili, ambalo linafanya kazi kama tatizo la usalama wa taifa kwa nchi yetu… vitaendelea,” aliandika kwenye X.

Swahiba wa Erdogan aliegeuka audi nambari moja

Kwa wakati mmoja Gulen alikuwa mshirika ambaye alimsaidia Erdogan alipokuwa waziri mkuu mapema miaka ya 2000, lakini aligeuka kuwa mtu asiyehitajika baada ya kashfa ya ufisadi ya mwaka 2013 kumhusisha Erdogan na watu wake wa karibu.

Erdogan alimtuhumu Gulen na baadaye kuanza kumshutumu kwa uhusiano wa kigaidi, na kulilaani vuguvugu lake la Hizmet kama “shirika la kigaidi la FETO.”

Soma pia: Kamata kamata ya wanajeshi na majaji yaendelea Uturuki

Gulen mara kwa mara alisisitiza kwamba vuguvugu lake lenye ushawishi lilikuwa tu mtandao wa taasisi za hisani na biashara.

Mambo yalikua mabaya mwaka 2016 wakati Erdogan alipomtuhumu kupanga mapinduzi yaliyoshindikana, na kusababisha kuanzishwa kwa ukandamizaji mkubwa.

Papo kwa Papo 19.07.2016

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Katika safisha safisha hiyo, watu wapatao 700,000 walifunguliwa mashtaka na karibu 3,000 ya wafuasi wa Gulen walihukumiwa maisha kwa kile ambacho mamlaka zilisema ni ushiriki wao katika mapinduzi.

Watu wengine 125,000 walifukuzwa katika taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na askari 24,000 na maelfu ya majaji, huku mamlaka zikifunga shule za kibinafsi, vyombo vya habari na makampuni ya uchapishaji yanayohusishwa na Gulen.

Uturuki bado inaendelea kuwaweka jela wafuasi wa Gulen na inadai kurejeshwa kwao kutoka nchi ambako mtandao wake unafanya kazi.

Vyanzo vya usalama vya Uturuki vilivyonukuliwa na shirika la utangazaji binafsi la NTV, walisema watu wachache sana wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Gulen na kwamba mwili wake huenda ukazikwa nchini Marekani katika eneo ambalo litahifadhiwa kuwa siri.

Related Posts