KIONGOZI Mkuu wa jamii ya Kimaasai nchini, Laigwanan Issack Ole Kisongo amesema wanaendelea na mazungumzo na Serikali kwa lengo la kuangalia uwezekano wa zoezi la uhamishwaji wa wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro kusitishwa.
Akijibu swali kutoka kwa washiriki wa mdahalo kuhusu nafasi ya Mila katika kutoka Haki ya vijana na wanawake kumiliki Ardhi katika kongamano la nne la Kimataifa linalohusu vijana na utawala wa Ardhi ( CIGOFA4 ), linaloendelea Jijini Arusha, Ole Kisongo amesema changamoto iliyopo nchini ni kwamba aridhi yote iko chini ya Rais hivyo anaweza kuamua matumizi ya ardhi hiyo wakati wowote.
Aidha amesema jamii hiyo imeamua kuwashirikisha Wanawake kwenye umiliki wa ardhi kwa kuwa vijana wengi katika jamii hiyo wamekuwa wakiuza ardhi pindi wanaporithishwa.
Amesema jamii hiyo imepitisha Sheria kuruhusu Wanawake kutambulika kwenye umiliki wa Ardhi jambo ambalo halikuwahi kufanyika hapo awali.
” Siku hizi vijana wetu hawaaminiki, ukimmilikisha ardhi ataiuza na kutelekeza familia, tumepitisha Sheria ili kukomesha tabia hii ili ikitokea Kijana anataka kuuza ardhi lazima Mke wake aridhie kwanza lasivyo hatoweza kuiuza,”amesema.
Amesema kwa mujibu wa Mila za Kimaasai kijana anapoingia jando anakabidhiwa ardhi na Mali zote za familia na Baba katika familia hiyo anakuwa kama mwangalizi pekee.
Aidha amesema migogoro mingi ambayo imekuwa ikitokea katika maeneo ya wafugaji imekuwa ikisababishwa na utetezi wa Ardhi kwaajili ya shughuli za uchumi.
Wakichangia mada katika kongamano hilo, washiriki wamesema kuna umuhimu mkubwa kwa vijana na wanawake kumilikishwa ardhi kwa kuwa wao ndio nguvukazi katika jamii.
Wamesema hata hivyo pamoja na madai ya vijana wengi kukimbilia mijini na kuacha ardhi Vijijini Bado elimu kuhusu rasilimali ardhi inatakiwa kutolewa kwa vijana kabla ya kukabidhiwa.
Mkurugenzi wa shirika la Jumuiko la Maliasili nchini (TNRF), Faustin Zakaria amesema suala la umiliki wa ardhi kwa vijana linatakiwa kuanza katika ngazi ya jamii kwa kutambua umuhimu wa ardhi, utambulisho. na mgawanyo wa rasilimali hiyo na fursa zinazopatikana kwa vijana.
Aidha ametoa wito kwa Serikali kuwashirikisha vijana katika uundaji wa sera itakayokuwa ikitambua umiliki wa ardhi kwa vijana.
Kongamano hilo lililoanza Jana Jijini hapa, linalofanyika pia kwa njia ya mtandao linashirikisha washiriki zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika wengi wao wakiwa ni vijana pamoja na taasisi zinazofanya programu za utetezi wa haki za ardhi.