WAZIRI wa Maendeleleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Pembe Riziki Juma amewahimiza wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza jitihada za kuwaendeleza wanawake na kuimarisha usawa wa kijinsia nchini na Afrika kwa ujumla.
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Kongamano la Uongozi wa Wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania, Finland, Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN).
“Kumwezesha kiongozi mwanamke kunafungua fursa mbalimbali zinazoweza kumsaidia kufanya maamuzi jumuishi na yenye kuliletea Taifa maendeleo pamoja na kuleta mabadiliko katika nyanya mbalimbali.Tukimjenga mwanamke tunampa nafasi nzuri ya kuleta mabadiliko katika nyanya zote za maendeleo.
“Na hasa katika kushughulikia masuala muhimu ya kuondoa umaskini, kuimarisha elimu hasa kukuza ujuzi na vipaji unaohitajika katika soko la sasa na baadae, kuimarisha huduma za afya na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jinsia zote,” amesema Waziri Juma.
Ameongeza Serikali inatambua uzingatiaji wa masuala ya jinsia una mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa na kwa kutambua hilo msisitizo umewekwa katika kukuza usawa wa kijinsia katika kufanya maamuzi katika ngazi zote.
Waziri Juma amesema ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na uongozi ni moja ya vipaumbele vya Serikali katika kuhakikisha usawa kati ya wanaume na wanawake.
Amesema kwamba takwimu zinaonesha wanawake katika nafasi za uongozi wakiwemo mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakurugenzi katika taasisi mbalimbali za umma ni asilimia 28.6 ya viongozi wote.
“Hiki ni kiashiria chanya kuelekea kufikia asilimia 30 ya uwakilishi wa wanawake katika uongozi, ambayo ni hatua muhimu kuelekea kufikia lengo Na. 5 la Usawa wa Kijinsia (SDG 5) kufikia asilimia 50 ifikapo 2030,” alisema Juma
Pamoja na jitihada za Serikali, bado kumekuwa na changamoto za namna ya kutekeleza ujumuishwaji wa jinsia katika usimamizi wa rasilimaliwatu hali inayosababisha kukosekana kwa uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume katika baadhi ya maeneo nchini.
Awali Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema kuwa kongamano hilo ni sehemu ya programu yao ya Uongozi wa Wanawake (WLP) inayolenga kusaidia wanawake kusonga mbele katika majukumu ya uongozi.
“Kupitia kongamano hili limewaleta pamoja viongozi wakuu wa kiafrika na wanaoibukia kutoka Zambia, Ethiopia, Kenga, Uganda, Afrika Kusini, Botswana, Msumbiji na Cameroon ili kubadilishana mawazo na kupeana mbinu bora ili kukuza ushirikishwaji wa wanawake katika majukumu ya uongozi.”
Ameongeza tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Uongozi inaonesha wanawake wapo wengi katika nafasi za chini za utendaji na katika nafasi za juu za maamuzi wanapungua hivyo wameona waongeze jitihada za kuwaweka zaidi katika programu hiyo.