Kwenye tamko la pamoja lililotolewa siku ya Jumatano (Oktoba 23), wakuu wa mataifa yanayohudhuria kwenye mkutano huo wa kilele walisema kwamba walikuwa wanatiwa wasiwasi sana na athari mbaya za vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya uchumi wa kilimwengu na wakati huo huo wakisikitishwa na migogoro kwenye eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Wakuu hao pia walisema walikuwa wanazingatia kwamba “kumekuwapo mapendekezo ya mataifa mbalimbali ya kupatanisha kwenye mzozo baina kati ya Urusi na Ukraine”, lakini hawakuitaja nchi ambayo inabeba jukumu hilo.
Hata hivyo, inafahamika kuwa India, ambayo ni mwanachama mwanzilishi wa jumuiya hiyo, na Uturuki, ambayo inahudhuria kwenye mkutano huu kama mgeni mualikwa, zimejitokeza wazi kubeba jukumu la kuziweka kitako Moscow na Kiev kumaliza vita vyao.
Soma zaidi: Katibu Mkuu wa UN yuko Urusi kwa mkutano wa kilele wa BRICS
Umoja wa Ulaya, ambao si mualikwa wala mshiriki wa mkutano huo, ulitowa wito hivi leo kwa viongozi wanaohudhuria kumuambia waziwazi Rais Vladimir Putin kwamba “avikomeshe vita vyake nchini Ukraine haraka iwezekanavyo.”
Msemaji wa Umoja huo, Peter Stano, alisema akiwa kwenye makao makuu mjini Brussels, kwamba Umoja huo unaamini kuwa washiriki wote wa mkutano huo wa Kazan watatumia tukio hilo kumnasihi Putin aachane na vita dhidi ya Ukraine.
Stano pia aliikumbusha Uturuki, ambayo bado inapigania kujiunga na Umoja wa Ulaya kwamba msimamo wa Umoja huo ni kuitenga Urusi kimataifa kadiri inavyowezekana.
Mfumo mbadala wa malipo
Hayo yakijiri, Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil aliwaambia washiriki wa mkutano huo wa BRICS kwa njia ya vidio kwamba muda ulikuwa umewadia wa kubuni mfumo mbadala wa malipo baina yao, akiongeza kuwa Benki ya Maendeleo iliyoanzishwa na jumuiya hiyo ilidhamiriwa kuwa mbadala wa taasisi zilizoshindwa na Bretton Woods.
“Sasa ni muda wa kusonga mbele wa kuunda mfumo mbadala wa malipo baina yetu. Haina maana ya kuondosha sarafu zetu, lakini tunapaswa kuhakikisha kuwa mfumo wa vyanzo vingi vya nguvu unaonekana kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa pia. Mjadala kuhusu hili unahitaji kufanyika kwa makini lakini hauwezi kuahirishwa tena.”
Soma zaidi: Mkutano wa BRICS: Putin akutana na viongozi mbalimbali
Tayari, mwenyeji wa mkutano huo, Urusi, ilishapendekeza uundwaji wa mfumo wa mabadilishano ya bidhaa, kwa kuanzia na nafaka.
“Nchi za BRICSni miongoni mwa wazalishaji wakubwa kabisa wa ngano na mafuta ya nafaka ulimwengu, na kwa hivyo tunapendekeza kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya nafaka baina yetu.” Rais Putin aliwaambia wajumbe wa mkutano huo.
Kwa upande wake, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, alitumia hotuba yake mbele ya mkutano huo wa kilele wa BRICS, kuwataka washiriki kusaidia kwenye kukomesha vita katika Ukanda wa Gaza na pia nchini Lebabon.
Pezeshkian, ambaye nchi yake imejiunga na jumuiya mwaka kuu, alivielezea vita hivyo kuwa ni “vya kikatili na vyenye maumivu makali kabisa” kuwahi kushuhudiwa duniani kwa miongo mingi.