Na Mwandishu wetu,Michuzi Tv
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia. Adolf Mkenda amesifu shughuli zinazofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima ya kusimamia sekta hiyo muhimu kwa Taifa huku akiitaka taasisi hiyo kuendelea kuweka miundombinu itakayovotia wawekezaji wengi zaidi wa sekta ya bima kutoka Tanzania.
Ameyasema hayo mapema leo wakati alipotembelea Banda la TIRA kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo. Waziri Mkenda amesema, sekta ya bima mbali ya kusaidia kukinga majanga mbalimbali yanayotokea lakini pia ni sekta ambayo watanzania wanapaswa kutumia fursa iliyopo ili kuweza kuwekeza kwa kufungua kampuni ili kuweza kujiingizia kipato binafsi na taifa kwa ujumla.
Akijibu swali kuhusu njia zinazofanywa na Mamlaka ili kuvutia uwekezaji kwa wazawa, Mwanasheria Jamal Mwasha ambae ni Msajili wa Migogoro ya Bima katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima amesema Sheria ya Bima sura ya 394 kupitia kifungu cha 16 imeweka sharti kuwa kila kampuni inayoanzishwa nchini, lazima walau theluthi moja imilikiwe na wazawa. Kwahiyo Mamlaka ina hakikisha kifungu hiki kinazingatiwa ipasavyo na sharti hilo linatimizwa, amesema pia Mamlaka inatumia majukwaa mbalimbali inapokutana na wawekezaji na wadau wa sekta nyingine kuwapa elimu juu ya fursa zilizopo na kumekua na mwitikio mzuri.
Mwasha amemalizia kwa kusema kuwa Mamlaka inasaidia uanzishwaji wa Konsotia ya Bima ya Kilimo ambapo ni muunganiko wa kampuni wazawa walioweka mtaji ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wa Skimu ya Taifa ya Bima ya Kilimo na kuongeza uwezo wa kimtaji wa soko la bima nchini kwa ajili ya kukinga majanga kwenye sekta ya kilimo.
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri kwenye Banda la TIRA, Meneja Uhusiano na Mawasiliano Bi. Hadija Maulid ameeleza kuwa TIRA inashiriki kwenye Maonesho ya wiki ya huduma za kifedha pamoja na wadau wa kampuni za bima kwa lengo la kutoa elimu kwa umma wa Tanzania kuhusu umuhimu bima lakini kwa kampuni zinazoshiriki zinatoa huduma za moja kwa wananchi wanaohitaji kukata bima mbalimbali.
Maonesho ya Wiki ya huduma za fedha kitaifa yanayofanyika jijni Mbeya katika viwanja vya Ruanda Nzovwe yameanza rasmi Oktoba 21 na yatahimishwa Octoba 26, 2024