Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala, amedai hayo leo Oktoba 23,2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Maximilian Malewo wa mahakama ya HakimuMkazi Kisutu,wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Mheshimiwa kesi imekuja leo kwa ajili ya kutajwa lakini upelelezi bado haujakamilika, hivyo naomba tarehe nyingine ya kutajwa,” amedai Wakili Winiwa.
Baada ya kudai hayo, Hakimu Malewo, ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23, mwaka huu kwa kutajwa, washitakiwa wamerudishwa mahabusu.
Mbali na Mapande, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa Kanisa hilo, Winnie Owino( 33) na mfanyabiashara Nicolaus Owino(29) ambao walipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Maximilian Malewo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manane ambapo shtaka la kwanza kuongoza genge la uhalifu, la pili wizi na tatu hadi nane ni utakatishaji fedha.
Inadaiwa katika shtaka la kwanza inawakabili washitakiwa wote, ambapo inadaiwa kati ya Mei mwaka 2021 na Januari mwaka 2023, jijini Dar es Salaam waliongoza genge la uhalifu kisha kujipatia sh. milioni 717, 126,245, kutoka akaunti ya benki ya CRDB, mali ya Kanisa hilo.
Shtaka la pili ambalo ni wizi inamkabili mshitakiwa Mapande ambapo inadaiwa kati ya Mei mwaka 2021 na Januari mwaka 2023, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa mtumishi wa Kanisa hilo aliiba sh. milioni 717.1, mali ya Kanisa.
Katika shtaka la tatu ambalo ni utakatishaji fedha, inadaiwa kwa kipindi hicho alifungua akaunti benki ya CRDB lenye jina lake kisha akaingiza sh. milioni 396, 629,029
Shtaka la nne linawakabili Mapande na Winnie, inadaiwa katika kipindi hicho walifungua akaunti benki ya CRDB, yenye jina la Winnie, kisha wakaingiza sh. milioni 208,468, 091.
Pia katika shtaka la tano, linamkabili Mapande na Owino, inadaiwa washitakiwa hao walifungua akaunti benki hiyo na kuingiza sh. 112, 029,123, lenye jina la Owino.
Shtaka la sita hadi nane , linamkabili Mapande na Winnie, inadaiwa katika kipindi hicho walitumia fedha hizo kisha kununua magari mawili aina ya Toyota Harrier, Toyota Crown na walinunua nyumba katika eneo ambalo halijapimwa mtaa wa Mtambani, Mapinga Bagamoyo.