Shahidi: Dk. Saqware alinitisha kunifukuza kazi nilipomkataa kimapenzi

 

SHAHIDI Leila Ahmed (31) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima(Tira) Dkt. Baghayo Saqware alitishia kumfukuza kazi baada ya kukataa alipomtaka kimapenzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Leila ambaye ni shahidi namba mbili katika kesi ya madai namba 167/2023 iliyofunguliwa na Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dk. Baghayo Saqware dhidi ya Hospitali Salamani iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam na mmilii wa hospitali Dk Abdi Wasarme amedai hayo wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi..

Katika kesi hiyo Dk. Saqware anaiomba mahakama hiyo itoe amri kwa Hospitali ya Salamani pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa hopitali hiyo,Abdi Warsame imlipe mshahara wa miezi 13 kiasi cha Sh. 78 milioni.

Akiongozwa na Wakili Juma Nasoro kutoa ushahidi wake, Leila amedai mwezi Aprili 2020 Mkurugenzi Mkuu alitambulisha Dk. Saqware hospitalini hapo na kama meneja wa hospitali hiyo

Amedai kuwa Hospitalini hapo yeye alikuwa anajifunza kufanya kazi upande wa bima na baadaye alipelekwa kukaa mapokezi.

Ameendelea kudai kuwa aliandika barua kuripoti kwa Dk. Wasarme baada ya tukio hilo na akaamua kuacha kazi na hakurudi tena kufanya kazi katika hospitali hiyo.

Shahidi wa kwanza wa kwa upande wa mdaiwa alikuwa ni mmiliki wa Hospitali ya Salamani Health Centre, Dk. Abdi Wasarme ameiomba mahakama ifute kesi hiyo ya madai dhidi yake na hospitali na mahakama imuamuru Dkt Saqware kumlipa fidia ya gharama za kesi toka ilipoanza hadi itakapokwisha.

Dk. Wasarme amedai hayo wakati akitoa ushahidi wake na kueleza namna alivyokutana na Dkt. Saqware na kumpa kazi na baadae kusitisha mkataba naye.

Amedai kuwa walifahamiana na Baghayo Saqware mwaka 2019 baada ya kuwa na mgogoro wa malipo na Kampuni ya Bima ya afya ya AAR ndipo alitoa taarifa kwenye ofisi za Tira.

Akiongozwa na Wakili Juma Nassoro shahidi huyo amedai baada ya kutoa taarifa Dk. Saqware aliitisha kikao kati ya AAR na hospitali hiyo ambapo aliwasuluhisha na ndipo hospitali ya Salamani ililipwa fedha alizokuwa akiidai kampuni hiyo ya bima.

Amedai kuwa mwaka 2020 Dk. Saqware aliondolewa kwenye nafasi ya kamishna wa Tira ndipo alimfuata Dk. Warsame na kumuomba kazi na wakakubaliana atakuwa Meneja wa hospitali ya Salamani na kumsaidia majukumu yake kuanzia Julai Mosi, 2020

Aprili 11,2020 walisaini mkataba wa makubaliano ya kuanza kazi na akaomba awe anafika ofisini ili kuzoea majukumu na kupata utaalamu zaidi wa mambo ya hospitali hadi siku rasmi ya kuanza kazi itakapofika.

Dk. Wasarme amedai alikubali na kumtambulisha kwa wafanyakazi wengine kuwa atakuwa Meneja na watakuwa wanaripoti kwake badala yake.

Amedai alipoanza kufika ofisini alianza kupata malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wengine juu ya Dk. Saqware kwamba alikuwa akiwanyanyasa wafanyakazi wa kike na kuwatishia kuwa atawafukuza kazi akiwa kama meneja.

Pia amedai alikuwa akichukua fedha za hospitali na kufanya matumizi binafsi bila kurudisha na alikuwa akiongeza gharama za vifaa juu zaidi ya bei zake halisi.

“Baada ya kubaini hayo niliimuita na kumuonya lakini hakuonesha tofauti baada ya kuona hivyo niliamua kusitisha mkataba na Dk. Saqware kwani niliona sitoweza kufanya naye kazi na kumuandikia barua Aprili 30,2020 kwa ajili ya kusitisha mkataba.

Aliendelea kudai baada ya hapo Dk. Saqware alianza kumpa vitisho kuwa atawaambia TAKUKURU waanze kufuatilia hospitali yake na kuwa atafungwa apotelee gerezani.

Shahidi wa tatu,ambaye ni Mtunza Fedha wa hospitali, Afifa Suleiman(59) pia alikiri kumfahamu Dk. Saqware na kuwa alikuwa boss wake na alikuwa akifunga naye hesabu za hospital na fedha zilikuwa zikikaa kwake.

Amedai ulitokea upungufu wa fedha kiasi cha Sh 1,700,000 kwa awsmu ya kwanza na nyingine 1,900,000 kwa mara ya pili na hazikurudishwa na alipogundua alitoa taarifa kwa Dk. Wasarme.

Shahidi wa mwisho alikuwa ni Ofisa Manunuzi wa hospitali hiyo Charles Daktari ambaye pia alikiri kumfahamu Dkt Saqware na amedai alikuwa akiripoti kwake akitaka kufanya manunuzi na alikuwa akimwambia aongeze bei za vitu tofauti na bei yake halisi.

Baada ya mashahidi hao kumaliza Hakimu Mushi ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30, mwaka huu kwa ajili ya uamuzi.

About The Author

Related Posts