Mali za Urusi zitakazotumiwa katika mpango huo ni zile zilizozuiwa tangu Moscow ilipowekewa vikwazo baada ya kuivamia Kyiv, uamuzi uliofanywa baada ya Umoja wa Ulaya kufanya majadiliano na Marekani.
Nyaraka za kisheria kuhusu maamuzi hayo zinaonesha kuwa, faida kutokana na mali za Urusi zilizozuiwa Umoja wa Ulaya zitapaswa kutumika kwa ajili ya mikopo inayotolewa na kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiviwanda, G7. Awali mwakilishi wa Marekani alisema kundi hilo limekubali kutoa mkopo wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 50 na zitakwenda Ukraine.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya waridhia vikwazo vipya dhidi ya Urusi
Kabla ya uamuzi wa mwisho wa baraza la Umoja wa Ulaya, siku chache zilizopita Bunge la umoja huo lilipiga kura na kupitisha matumizi ya mali za Urusi kwa ajili ya mkopo wa Kyiv.
Katika vikwazo ambavyo Umoja wa Ulaya uliiwekea Urusi, ulizizuia mali zake zenye thamani ya karibu dola za Kimarekani bilioni 226 mali ya benki kuu ya nchi hiyo tangu Februari 2022.
Mapato makubwa yanayopatikana kama riba kutokana na mali hizo yanakadiriwa kuwa karibu dola bilioni 2 hadi tatu kwa mwaka. Mjadala mkali kuhusu mpango wa kuzitumia faedha hizo kama mkopo ulikuwa magumu huku yakihusisha mataifa mengi na haikuwa wazi ni namna gani Marekani ingeshiriki.
Marekani kuchangia dola bilioni 20 katika mkopo wa Ukraine
Muda mfupi kabla ya uamuzi wa Umoja wa Ulaya, Marekani ilitangaza kuwa ingechangia dola bilioni 20 katika mkopo wa dola bilioni 50 unaotolewa na kundi la G7.
Mwanzoni Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa kiwango cha juu ambacho ungechangia kingekuwa dola bilioni 35, ingawa Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner alisema kuwa umoja huo kabla ya hapo ulipanga kuchangia dola bilioni 20 pekee.
Kulingana na kauli za Umoja wa Ulaya zilizotolewa Jumatano jioni, mkopo wake kwa Ukraine utakuwa tayari kabla ya wisho wa mwaka.
Makubaliano hayo yanatokana na mpango ambao mataifa yanayounda kundi la G7 na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana katika mkutano wa mwezi Juni. Hata hivyo bado kulikuwa na changamoto zilizohitaji kutatuliwa katika mazungumzo hayo, hasa kuhusiana na sheria za vikwazo za Umoja wa Ulaya.