Nchi za Afrika ambazo zimepitiwa na bonde la ufa la jotoardhi zimetakiwa kushirikiana kubuni mipango mbalimbali ya utafutaji wa rasilimali ya jotoardhi ili kuharakisha maendeleo yatayotokana na rasilimali hiyo.
Rai hiyo imetolewa leo Oktoba 23, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akifungua Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo – C10) linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21 hadi 27 Oktoba, 2024.
Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa washiriki wa kongamano hilo watumie fursa inayotolewa kwenye kongamano hilo kushirikiana ili kuharakisha maendeleo ya rasilimali za jotoardhi na hivyo kuharakisha mabadiliko ya bara la Afrika kutoka kwenye gharama kubwa ya mafuta.
“Mjitahidi kuwa na ushirikiano katika kuchunguza maeneo ya jotoardhi na kutafuta uwekezaji unaohitajika katika kutumia rasilimali hii muhimu. Ni muhimu kuimarisha ubadilishanaji maarifa, mbinu bora, teknolojia pamoja na kubuni na kutekeleza programu za uchunguzi za kikanda.” Amesema Mhe. Dkt. Mpango.
Pia amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila nchi kuwa na taasisi iliyojitolea kuongoza maendeleo ya jotoardhi pamoja na kuwa na mifumo sahihi ya kisheria na udhibiti ambayo inaweza kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi.
Vile vile amependekeza kwamba nchi za ARGeo zinapaswa kuzingatia kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na Benki za Maendeleo kama vile TADB na Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia hivyo kufanya uwekezaji binafsi katika matumizi ya rasilimali jotoardhi kuvutia zaidi.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum), Mhe. Kapteni George Mkuchika amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikiwa kusambaza umeme kwa zaidi ya asilimia 98 nchi nzima ambapo hadi kufikia Disemba, 2024 vijiji vyote nchini vitakuwa vimefikiwa na nishati ya umeme
“Mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka hivyo, wakati tunapeleka umeme kila kijiji ni lazima tuongeze uzalishaji. Nashukuru kwa miradi ya umeme ikiwemo JNHPP na hii ya uzalishaji kupitia jotoardhi,” amesema Mhe. Mkuchika.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kufikia mwaka wa 2044, nchi inatarajia kuzalisha MW 995 kutoka kwenye vyanzo vya nishati ya jotoardhi ambayo itahesabu takriban 4.93% ya jumla ya uwezo uliowekwa.
“Matokeo ya mkutano huu yatachochea maendeleo ya jotoardhi nchini Tanzania na bara la Afrika kwa kuongeza kujulikana, kukuza ushirikiano na kuimarisha ushirikiano na wadau wa ndani na wa kimataifa.Tunaweza kufungua uwezo wa nishati ya jotoardhi ili kuendesha maendeleo ya kiuchumi na uendelevu wa mazingira.” Amemalizia Mhe. Kapinga.