MIKATABA YA UJENZI WA BARABARA ZENYE 168 KM YASAINIWA DAR ES SALAAM

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetia saini mikataba ya awali kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya mradi wa DMDP awamu ya 2.

Mikataba hii inajumuisha ujenzi wa kilomita 168.22, ambapo mikataba 8 yenye thamani ya Shilingi bilioni 190 imesainiwa, ikihusisha kilomita 63.66, na mikataba iliyobaki yenye thamani ya Shilingi bilioni 262,465,285,305.61 itakayojenga kilometa 104.56 itasainiwa ndani ya mwezi Novemba, 2024.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Oktoba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema Miradi hiyo izingatie mahitaji ya wananchi hususani “kama tunajenga soko je ni kweli wananchi wa eneo hilo wanahitaji soko? Kusiwe na miundombinu inayojengwa ambayo badala ya kukamilika haitumiki ni lazima tuzingatie mahitaji”.

Aidha ameziagiza Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam na Halmashauri zote nchini pindi wanapoanzisha miradi hiyo ya ujenzi wa soko, vituo vya mabasi, wawe wanatenga eneo la kuwapeleka wafanyabiashara kwenye eneo la muda kupisha ujenzi badala ya kuwaondoa bila sehemu mbadala hivyo kuchonganisha wananchi na Serikali yao.

“Maeneo haya ya ujenzi wa masoko, vituo vya mabasi n.k. yanapokamilika wafanyabiashara waliokutwa na mradi wawe kipaumbele katika kupatiwa maeneo hayo”. Amesema Waziri Mchengerwa.

Pamoja na hayo amemtaka Katibu Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Mtendaji Mkuu wa TARURA, kuhakikisha utekelezaji wa mikataba hiyo unafanyika kwa ufanisi mkubwa kama ilivyofanyika katika awamu ya kwanza.

Ameziasa timu ya uratibu wa miradi TAMISEMI na timu za utekelezaji wa miradi katika Halmashauri na TARURA kuhakikisha wanatekeleza mikataba hiyo kwa bidii na weledi mkubwa ili mwisho wa siku wananchi wa Dar es Salaam wakanufaike na uwekezaji huo unaofanywa na Serikali.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema mradi huo utajenga na kuboresha kilomita 90 za mifereji mikubwa ya maji ya mvua, vituo tisa vya mabasi, masoko 18 na madampo matatu ya kisasa.

Amesema Jumla ya kata 72 katika halmsahauri zote za Dar es Salaam zitaguswa na mradi, ambapo takribani wananchi milioni 4 watanufaika moja kwa moja na mradi.

Ameeleza kuwa gharama ya mradi ni Dola za Marekani Milioni 438 ambapo Benki ya Dunia itatoa mkopo wa Dola Milioni 385 na Serikali ya Uholanzi itatoa ruzuku ya Dola Milioni 53.

“Katika mgawanyo wa fedha hizo, Dola 295 milioni (sawa na 67%) zimekwenda kwenye miundombinu, Dola 108 milioni (sawa na 25%) zitatumika katika usimamizi wa taka ngumu, Dola 20 milioni (sawa na 5%) zitatumika uimarishaji taasisi na Dola 15 milioni (sawa na 3%) ni kwa ajili ya usimamizi wa miradi”. Ameeleza

Amesema Madaftari ya fidia kwa mali ambazo zinaathirika na ujenzi wa barabara kwa Halmashauri zote tano yameshakamilika na yana jumla ya Shilingi bilioni 7,974,598,879.39 ikiwa ni gharama ya fidia inayotakiwa kulipwa kwa waathirika kabla ujenzi haujaanza.

“Kwa mujibu wa makubaliano ya mkopo kati ya Serikali na Benki ya Dunia, gharama za fidia zitalipwa na Serikali”. Amesema

Amesema Changamoto inayotarajiwa ni fedha za fidia kutopatikana kwa wakati ili wakandarasi waanze ujenzi bila kuchelewa.

“Hali hii inaweza ikapelekea barabara zenye fidia kubwa kuchelewa kujegwa. Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeshawasilisha maombi ya fedha za fidia Wizara ya Fedha kwa hatua zaidi”. Amesema Mhandisi Kanyenye.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya awali ya ujenzi wa zaidi ya kilomita 168 za barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, zitakazojengwa na mradi wa DMDP awamu ya pili. Hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Humphrey Kanyenye  akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya awali ya ujenzi wa zaidi ya kilomita 168 za barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, zitakazojengwa na mradi wa DMDP awamu ya pili. Hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akipiga ngoma mara baada ya kuwasili kwenye hafla ya utiaji saini wa mikataba ya awali ya ujenzi wa zaidi ya kilomita 168 za barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, zitakazojengwa na mradi wa DMDP awamu ya pili. Hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam.



Wadau mbalimbali wakifuatilia hafla ya utiaji saini wa mikataba ya awali ya ujenzi wa zaidi ya kilomita 168 za barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, zitakazojengwa na mradi wa DMDP awamu ya pili. Hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 24, 2024 Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Related Posts