MABONDIA ZAIDI YA 10 WAPIMA AFYA KUELEKEA HOMA YA SGR

Zaidi ya mabondia 10 wamepima afya kuelekea pambano la ‘Homa Ya SGR’ itakayofanyika Oktoba 25 mwaka huu Mkoani Morogoro.

Mabondia hao ni Paul Kamata, Osama Arabi, Hassan Ndonga, Debora Mwenda, Abuu Lubanja, Adam Peter, Haruna Ndaro, Abdallah Ponda, Hamza Mchanjo, Shazir Hija, Hamadi Furahisha na Ibada Jafari.

Daktari wa Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Khadija Hamisi amesema mabondia hao wamepima magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi.

“Sheria na kanuni za ngumi wiki moja kabla ya kupima pambano mabondia wanapaswa kupima afya zao, hivyo leo (jana) tumefanya zoezi hili.”

Dk. Khadija amefafanua mbali ya Ukimwi mabondia hao wamepima homa ya ini, kisukari, presha, uwingi wa damu na magonjwa ya zinaa.

“Mandaalizi yanaendeleaje vizuri na wiki iliyopita mabondia 16 kutoka Morogoro walipima afya na tumemaliza Dar es Salaam”.

Mratibu wa matukio kutoka Kampuni ya Peak time ambao ndiyo waandaji wa pambano hilo, Bakari Khatibu amesema lengo la kutoa jina la ‘Homa Ya SGR’ ni kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika michezo kutokana na mchango wake anaoufanya.

“Mapambano hili litakuwa na mabondia wazuri ambao wana vipaji na umahili nzuri wakiwa ulingoni miongoni mwao ni Habibi Pengo, Hassan Ndonga, Osama Arabi, Paul Kamata na Juma Misumari.

Khatibu amewaomba wadau na mashabiki wa ngumi kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo kuja kushuhudia burudani.

Naye bondia Hassan Ndonga amesema amejipanga vizuri kuhakikisha anamchakaza vibaya mpinzani wake, Hamza Mchanjo katika pambano hilo.

“Nimejipanga vizuri nashukuru afya yangu ipo vizuri hapa kilichobaki ni siku ya pambano ifike, mpinzani afanye mazoezi tuje kuonyesha kazi”

Kwa upande wake Bondia Debora Mwenda aliwaomba wakazi wa Morogoro wajitokeze kwa wingi katika pambano hilo kuja kushuhudia burudani kutoka kwake.



Related Posts