Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema uhusiano kati ya nchi yake na Marekani baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani utategemea mtazamo wa nchi hiyo, huku akiyapongeza maoni ya Donald Trump kuhusu nia yake ya kuumaliza mzozo wa Urusi na Ukraine. Putin ameyasema hayo wakati mzozo kati ya nchi yake na Ukraine ukizidi kufukuta.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari rais wa Urusi Vladimir Putin amesema mtazamo na msimamo wa serikali ya Marekani juu ya Urusi baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika mwezi Novemba utaamua hatma ya uhusiano wa nchi hizo mbili.
Soma zaidi. Mali za Urusi zilizozuiwa Ulaya zitatumika kuikopesha Ukraine dola bilioni 50
“Jinsi uhusiano wa Urusi na Marekani utakavyokua baada ya uchaguzi itategemea Marekani yenyewe. wakiwa wawazi, basi na sisi pia tutakuwa wazi. Na ikiwa hawataki, basi sawa. Hili ni juu ya utawala ujao wa nchi hiyo utakavyochagua” amesema Putin.
Rais Putin ameunga mkono maoni yaliyotolewa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye anawania urais wa Marekani katika uchaguzi ujao juu ya nia yake ya kuvimaliza vita lakini ikiwa tu maoni hayo yaliyotolewa na Trump ni ya dhati.
Putin alikuwa akizungumza mwishoni mwa mkutano wa kilele wa BRICS katika mji wa Kazan ambapo amekabiliwa na wito kutoka kwa baadhi ya washirika wake muhimu wakitaka mapigano nchini Ukraine yafikie ukomo.
Urusi yaendeleza mashambulizi Ukraine
Katika hatua nyingine, Maafisa wa mji mkuu wa Ukraine, Kiyv, wamesema mapema leo kuwa Urusi imefanya mashambulizi ya anga usiku kucha. Msimamizi wa jeshi mjini humo Serhiy Popko amesema katika mtandao wa Telegram kuwa droni kadhaa zilidunguliwa katika mashambulizi hayo.
Msimamizi huyo ameongeza kuwa mpaka sasa mamlaka hazijapokea taarifa zozote juu ya uharibifu au majereha yaliyotokana na mashambulizi hayo.
Soma zaidi.Guterres amwambia Putin, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umekiuka sheria za kimataifa
Waandishi wa habari wa Reuters waliripoti kusikia milipuko mingi mapema leo huku jeshi la anga la Ukraine likisema katika taarifa yake kwamba ulinzi wake wa anga uliziharibu droni 36 kati ya 63 zilizorushwa usiku kucha na Urusi katika maeneo mbalimbali ya
Ukraine.
Kwa upande mwingine katika mzozo huo, Waziri wa ulinzi wa Uholanzi Ruben Brekelmans amesema mapema leo kuwa shirika la ujasusi la nchi hiyo limethibitisha kwamba Urusi inapeleka wanajeshi wasiopungua 1,500 wa Korea kaskazini kupigana nchini Ukraine.
Mpaka sasa Urusi haijakanusha madai hayo hatua ambayo mataifa ya magharibi yanaitazama kuwa inazidi kuvichochea vita hivyo.
Vyanzo: AFP na Reuters.