Ujerumani yataka kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na India – DW – 25.10.2024

Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu Modi, Scholz amesema wanataka kuyasogeza majeshi ya nchi hizo mbili karibu zaidi. Kando ya ushirikiano wa kijeshi Kansela huyo wa Ujerumani ameeleza nia ya Umoja wa Ulaya kukuza uhusiano wa kibiashara na India.

Scholz aliyeambatana na mawaziri wake wengi anafanya ziara hiyo akiwa na matumaini kuwa kupata soko kubwa nchini humo huenda kukapunguza utegemezi wa Ujerumani kwa China.

Katika mazungumzo na Scholz, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametangaza pia kuwa, utawala wa Kansela Scholz umeamua kuongeza viza zinazotolewa kwa mwaka kwa wafanyakazi wenye uzoefu wa India hadi 90,000 kutoka 20,000. Amesema anaamini kuwa hatua hiyo itaongeza nguvu katika ustawi wa Ujerumani.

Ushirikiano wa kibiashara wapewa kipaumbele

Kando ya mazungumzo baina ya viongozi hao wawili, Modi na Scholz wamehudhuria pia mkutano wa wafanyabiashara wa Ujerumani katika mji mkuu wa India. Katika mazungumzo hayo Modi amesema India inataka kufanya mabadiliko ya miundombinu yake na kwamba uwekezaji mkubwa unafanyika. Amebainisha kuwa mabadiliko hayo yanatoa fursa nyingi kati ya makampuni ya Kijerumani na ukanda wa Indopasifiki.

Ujenzi wa reli Maroda, India
India inafanya mageuzi makubwa katika miundombinu yakePicha: Anushree Fadnavis/REUTERS

Soma zaidi: Ujerumani kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na India

Kampuni ya Ujerumani ya Thyssenkrupp ni moja ya wazabuni wakubwa kuwahi kushirikiana na makampuni ya India katika kutengeneza nyambizi sita nchini India zinazokadiriwa kugharibu dola bilioni tano za Kimarekani.

New Delhi na Berlin pia zimesema zinafanya kazi pamoja katika miradi ya nishati jadidifu katika juhudi za kushirikiana katika suala la mabadiliko ya tabia nchi. Mwaka 2022, Ujerumani iliahidi kuipa New Delhi euro bilioni 10 ili itimize malengo yake mazingira.

 

Related Posts