Mashambulizi ya anga ya Israel kusini mashariki mwa Lebanon dhidi ya nyumba inayokaliwa na waandishi wa habari mapema siku ya Ijumaa (Oktoba 25) yamewauwa waandishi watatu wa habari.
Kituo cha habari cha Lebanon, Al Jadeed, kilichapisha picha za video kutoka kwenye eneo la tukio zikionesha majengo yaliyoporomoshwa na gari zenye maandishi ya PRESS, kwa maana ya chombo cha habari, zikiwa zimefunikwa na vifusi na mavumbi.
Ripoti zilisema jeshi la Israel halikuwa limetowa onyo lolote kabla ya kufanya mashambulizi hayo.
Soma zaidi: Lebanon yasema shambulizi la Israel limewaua waandishi wa habari watatu
Kituo cha televisheni chenye makao yake makuu mjini Beirut, Al-Mayadeen, kilisema wafanyakazi wake wawili – mpigapicha Ghassan Najjar na fundi mitambo Mohammed Rida – ni miongoni mwa waliouawa.
Kituo chengine cha televisheni cha Al-Manar, ambacho kinamilikiwa na kundi la Hizbullah, kimesema mpiga picha wake, Wissam Qassim, naye aliuawa kwenye mashambulizi hayo katika mkoa wa Hasbaya.
Mkurugenzi wa Al-Mayadeen, Ghassan bin Jiddo, alidai kwamba mashambulizi hayo ya Israel yalikuwa ya makusudi na yalilengwa dhidi ya wale wanaofichuwa uovu wa mashambulizi yake ya kijeshi.
Soma zaidi: Israel na Hezbollah zashambuliana kwenye maeneo muhimu
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Waziri wa Habari wa Lebanon, Ziad Makary, aliyesema waandishi hao waliuawa wakati wakitangaza kile alichokiita “uhalifu wa Israel” wakiwa katikati ya kundi kubwa la wanahabari wenzao. Kwa mujibu wa waziri huyo, kwenye eneo hilo kulikuwa na waandishi 18 kutoka vyombo saba vya habari.
Mashambulizi dhidi ya Khan Younis
Jeshi la Israel pia limekishambulia kitongoji cha Khan Younis kwenye Ukanda wa Gaza asubuhi ya leo na kuuwa watu 28, wengi wao wanawake na watoto. Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina, WAFA, watu wengine kadhaa wamejeruhiwa kwenye mashambulizi hayo yaliyoilenga nyumba moja inayokaliwa na raia wa kawaida.
WAFA imeripoti pia kwamba wanajeshi wa Israel waliivamia Hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza, huku wakirusha risasi kwenye jengo hilo na kuvunja viyoo vyake. Wanajeshi hao pia walizuwia kufikishwa kwa vifaa vya matibabu kutokana na kulizingira jengo la hospitali hiyo.
Soma zaidi: Lebanon yahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa kujiimarisha
Jeshi la Israel linadai kuwa bado linaendelea na operesheni yake kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza. Taarifa ya jeshi hilo imedai kuwa limefanikiwa kuwaangamiza wale linalowaita magaidi kadhaa, kuvunja miundombinu ya kigaidi na kukamata silaha za aina mbalimbali kwenye operesheni yake ya jana.
Idara ya Ulinzi wa Raia ya Palestina, ambayo kwa Gaza iko chini ya kundi la Hamas, imeripoti kuwepo kwa maiti na majeruhi kadhaa kwenye eneo hilo hapo jana baada ya jeshi la Isarel kuzishambulia nyumba kadhaa za raia.