Viongozi wa nchi hizo, pamoja na wa Uingereza waliokutana nchini Samoa, walifanya mazungumzo marefu na ya utata kuhusu vipengele nyeti vinavyohusu historia yao.
Katika taarifa ya pamoja, viongozi wa Jumuiya ya Madola walitilia maanani miito juu ya fidia iliyosababishwa ya watumwa waliopelekwa nje ya nchi zao. Viongozi hao pia wamezungumia juu ya athari za kudumu zilizotokana na wenyeji wa maeneo kadhaa kuporwa umiliki wa raslimali zao na wakoloni.
Soma Pia: Mfalme Charles wa Uingereza azomewa Australia
Katika tamko hilo viongozi wa nchi za jumuiya ya madola wamesema wakati umefika wa kufanya mazungumzo ya dhati kwa lengo la kujenga mustakabali wa pamoja katika msingi wa haki.
Uingereza yatakiwa kulipa fidia
Mataifa ya Kiafrika, Karibean na Pasifiki yanaitaka Uingereza na mataifa mengine yaliyokuwa na makoloni yalipe fidia kwa kuendesha biashara ya utumwa na kwa ukoloni uliyosababisha matatizo mengine. Nchi hizo zinataka mazungumzo yafanyike juu ya fidia.
Nchi nyingi zimeendelea kuwa maskini zaidi kuliko nchi za wakoloni wao na bado zinaendelea kukabiliwa na athari zilizotokana na biashara ya kikatili ya utumwa. Watu kati ya milioni 10 hadi milioni 15 kutoka bara la Afrika walichukuliwa na kugeuzwa watumwa kwa muda wa karne nne.
Soma Pia: Mfalme Charles asema Jumuiya ya Madola inapaswa kutambua historia chungu ya utumwa
Licha ya Uingereza kuonesha majuto juu ya utumwa, mpaka sasa inapinga wazo la kulipa fidia ya fedh zinazoweza kuwa kiasi kikubwa. Wakati wa mkutano huo, Uingereza ilijaribu kuepuka kutoa ahadi za wazi sambamba na kujaribu kuonesha nia ya kuudumisha umoja wa jumuiya ya madola.
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer, ameeleza wazi kwamba mkutano wa nchini Samoa haukuzungumzia juu ya swala la fidia. Amesema msimamo wa nchi yake uko wazi juu ya swala hilo la fidia. Hata hivyo ameeleza kuwa mazungumzo ya nchini Samoa yalikuwa chanya.
Viongozi wa nchi za jumuiya ya madola walichelewa kutoa tamko la pamoja kutokana na majadiliano ya kutafuta mwafaka.
Bahamas yasisitiza mdahalo juu ya udhalimu
Waziri mkuu wa Bahamas Philip Davis; amesema wakati sasa umefika wa mdahalo wa dhati juu ya udhalimu uliofanyika. Amesema unyama wa utumwa umesababisha majeraha makubwa katika jamii za Karibean na kwamba harakati za kupigania haki ndio kwanza zinaanza.
Waziri mkuu wa Uingereza anakabiliwa na shinikizo ndani ya nchi yake na mfalme Charles wa Tatu, anayetoka kwenye familia iliyonufaika na biashara ya utumwa anatakiwa aombe radhi. Mfalme Charles amesema anatambua machungu yanayoendelea kuwasibu watu kutokana na yale waliyotendewa katika karne zilizopita. Hata hivyo ametahadharisha juu ya kutumiwa lugha ya kuwagawanya watu.
Kuhusu swala la ulinzi
Viongozi wa nchi za jumuiya ya madola waliweza kusimama pamoja juu ya swala la ulinzi wa mazingira. Wamekubaliana kulinda takriban asilimia 30 ya bahari na kurejesha takriban asilimia 30 ya mfumo wa ikolojia baharini hadi kufikia mwaka wa 2030.
Viongozi wa nchi za jumuiya ya madola pia walikuabliana juu ya uteuzi wa waziri wa mambo ya nje wa Ghana, Shirley Ayorkor Botchwey, kuwa katibu mkuu mpya wa jumuia ya madola.
Soma Pia: Jumuiya ya Madola yamtangaza Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana kuwa Katibu Mkuu
Botchwey alikuwa mmoja wa wagombea watatu waliowania wadhifa huo. Wagombea wote waliuunga mkono wito kwa mataifa ya Ulaya juu ya kushughulikia ipasavyo historia ya ukoloni na utumwa.
Shirley Botchwey amehudumu kama waziri wa mambo ya nje kwa miaka saba, pia ameiwakilisha nchi yake Ghana kwa muda wa miaka miwili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Chanzo:AFP
Mhariri: Saleh Mwanamilongo