Jafo Aridhishwa Na Kasi Ya Mtambo Mpya Wa ALAF

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Selemani Jafo (kushoto) akizungumza wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha ALAF Limited alipoenda kukagua ujenzi wa mtambo mpya wa rangi wa kiwanda hicho. Kushoto kwa waziri ni Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited Ashish Mistry pamoja na sehemu ya menejimenti ya kampuni hiyo na wageni wengine walioshiriki katika ziara hiyo.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mtambo wa mabati ya rangi unaofanywa na kiwanda cha ALAF Limited ambacho kinaongoza katika uzalishaji wa mabati nchini.

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam alipotembelea kiwanda cha Alaf na kujionea ujenzi huo unaoendelea na unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

“Nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa na kwa kweli uzalishaji huu ukianza, utakuwa wa aina yake na wenye ubora mkubwa sana hapa nchini kwani hatutakuwa na haja ya kuagiza mabati ra rangi kutoka nje kama tunavyofanya sasa,” amesema

Ameongeza kuwa hatua hiyo itaongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa vijana wa kitanzania na kusisitiza kuwa yote haya yamewezekana kufuatia mazingira mazuri yaliyowekwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kukuza viwanda na biashara kwa ujumla.

“Kama serikali tunafikiria kuweka utaratibu wa kuzuia uingizaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini hususani mabati ili kulinda soko la ndani,” amewaambia waandishi wa habari na uongozi wa Alaf mara baada ya ziara hiyo na kuongeza kuwa kwa sasa uzalishaji wa mabati wa ndani unakidhi mahitaji ya ndani kwa hivyo hakuna haja ya kuagiza bidhaa hii kutoka nje.

Waziri huyo pia ameipongeza ALAF kwa kusimamia ubora na kuhakikisha watanzania wanapata thamani ya fedha wanazotoa ili kupata bidhaa bora.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Ashish Mistry amesema mtambo mpya utahakikisha uzalishaji ni wa hali ya juu zaidi na pia utaendeshwa na vijana wa kitanzania.

“Tayari kuna vijana 30 ambao ni wa Kitanzania kabisa na wameshapata mafunzo ya kina kuhusu uendeshaji huu wa mtambo mpya wa rangi kwa hivyo hatuna haja ya kuleta watu kutoka nje,” amefafanua na kuongeza kuwa nia yao ni kuendelea kuwa namba moja kwani ndio kampuni kongwe ya mabati nchini inayoadhimisha miaka 62 mwaka huu tangu kuanzishwa kwake.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa ALAF, Isamba Kasaka amesema wanatarajia kuanza uzalishani mapema mwakani na kutoa wito kwa watanzania waendelee kuwaunga mkono kwa kutumia bidhaa za kampuni hiyo.

“Mabati ya rangi sasa yatapatikana hapa hapa nchini baada ya mtambo wetu kukamilika kwa hivyo watanzania watarajie mambo mazuri mwakani,” alisema huku akimpongeza waziri na serikali kwa ujumla kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayopamoja na mambo mengine yamesaidia ALAF kutimiza malengo yake.

ALAF imeunganisha kikamilifu operesheni, si tu kwa kutengeneza mabati, lakini pia kwa kuzalisha vifaa vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za uezekaji wa nyumba. ALAF Limited hutengeneza vifaa mbalimbali vya metali kwa matumizi mbalimbali ya uezekaji wa nyumba.

Related Posts