Wanajeshi wa Israel wameshambulia vikali nchini Lebanon na Gaza, wakiendeleza vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah na huko Gaza dhidi ya kundi la Hamas.
Jeshi la Israel limesema limewazuia watu 100 wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Hamas lilipovamia hospitali ya Kamal Adwan katika mji wa Beit Lahya, ulio kaskazini mwa Gaza mwishoni mwa juma.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kati ya watu waliokamatwa na kuwekwa kizuizini ni wafanyakazi 44 wa hospitali hiyo na wote ni wanaume.
Maafisa wa afya wa Palestina wamesema hospitali hiyo, iliyokuwa inawahudumia wagonjwa wapatao 200, iliharibiwa vibaya katika uvamizi huo.
Soma Pia: Wakuu wa CIA na Mossad kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar kuhusu Gaza
Israel imesema Hamas na wapiganaji wengine wanavitumia vituo hivyo vya afya kuendeleza malengo yao ya kijeshi. Maafisa wa afya wa Palestina wamekanusha madai hayo na kulishutumu jeshi la Israel kwa kuhatarisha maisha ya raia bila kujali.
Mkuu wa Sera ya Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, akizungumza kwenye Mkutano wa 9 wa Jukwaa la Kikanda la Mediterania mjini Barcelona amesema, wasiwasi unaopaswa kupewa umuhimu zaidi kwa sasa ni hali mbaya inayowakabili watu kaskazini mwa Gaza.
Borrell amesema mashirika yote ya Umoja wa Mataifa, kuanzia Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu hadi shirika la OCHA ambalo linaratibu Masuala ya Kibinadamu, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, hadi Shirika la Afya Duniani, WHO, yote yanaonya kuhusu hali mbaya katika Ukanda wa Gaza.
Mkuu huyo wa Sera ya Nje wa Umoja wa Ulaya pia ametoa wito mpya wa kusitishwa mara moja kwa mapigano nchini Lebanon na amelaani mashambulizi ya Israel ambayo amesema yasiyokubalika, dhidi ya vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika vita vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah.
Soma Pia: Miito yaendelea kutolewa ili kutoutanua mzozo wa Mashariki ya Kati
Lebanon imesema imewasilisha malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mashambulio ya Israel ya wiki iliyopita yaliyosababisha vifo vya waandishi watatu wa habari katika eneo la kusini mwa nchi hiyo.
Huku mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani, Misri na Qatar yakiwa yameanza tena hapo jana Jumapili baada ya mengine kadhaa kushindwa kufanikiwa, Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi, amependekeza mpango wa kusimamisha mapigano kwa muda mfupi wa siku mbili ambayo yatashuhudia kubadilishana mateka wanne wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas na kwa upande wa Israel kuwaachia baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walio kwenye jela za Israel. Hakuna maoni yoyote mpaka sasa kutoka Israeli au kundi la Hamas.
Vyanzo: AFP/RTRE