Waziri chana aelekeza askari uhifadhi kuweka kambi Ikungi kukabiliana na tembo.

Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameelekeza timu ya Askari Uhifadhi 18 kuweka kambi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida kwa lengo la kukabiliana na tembo wanaovambia makazi ya watu.

Hatua hiyo inafuatiwa na tukio la hivi karibuni la tembo kuwepo katika eneo hilo na kusababisha taharuki kwa wananchi.


Akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara leo Oktoba 28,2024 kwenye Kijiji cha Mkiwa Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida Mhe. Chana amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo inapungua au kumalizika kabisa.

“Tunakwenda kuongeza askari watakaotusaidia kuhakikisha tembo wanarudi katika maeneo yao ya hifadhi sambamba na kuongeza mabomu baridi kufukuza tembo” Mhe. Chana amesisitiza.

Aidha, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji,Wilaya na Mkoa itafanya zoezi la kutambua na kuweka alama katika maeneo ya Korido za wanyamapori (shoroba) na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutoweka shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.

“Baada ya kuzitambua shoroba tunataka kuwepo na shughuli za uhifadhi mfano kuanzisha Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) ili kuendeleza uhifadhi” Mhe. Chana amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amesema Serikali inaenda kuweka mpango wa matumizi bora ya Ardhi ili maeneo ya mifugo, makazi na kilimo yajulikane.

Mhe. Chana ametaja mikakati mingine ya kudhibiti tembo kuwa ni kuwafunga kola maalum kujua uelekeo wa kundi la tembo,kutoa elimu kwa Askari wa Vijiji (VGS) na kufanya sensa ya wanyamapori.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amewataka wananchi wa Ikungi kutoa ushirikiano kwa Askari Uhifadhi hao ili kukabiliana na tembo ipasavyo.

“Ninyi tembo mnawajua vizuri na tabia zao hivyo mshirikiane nao na hawa Askari wetu wa Vijiji mliopata elimu mtaungana nao kuhakikisha tatizo la tembo linaisha” Mhe. Dendego alisisitiza.

Mkutano huo umehudhuriwa na wananchi pamoja na Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka Mkoa wa Singida na Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake.

Related Posts