Rodri ashinda Ballon d’Or – DW – 29.10.2024

Kiungo wa kati wa Manchester City na Uhispania Rodri ameshinda tuzo ya mchezaji bora duniani ya Ballon d’Or. Rodri alishinda taji la Ligi ya Premier ya England na la Euro 2024. Uamuzi wa kumtuza kiungo huyo mkabaji ilijiri kwa mshangao, kwa vile mshindi wa taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya Vinicius Junior wa Real Madrid alionekana kupigiwa upatu na wengi. Saa chache kabla ya hafla hiyo ya jana usiku mjini Paris, klabu hiyo ya Uhispania ilitangaza kuwa ujumbe wake hautahudhuria sherehe hiyo kwa sababu ya kile ilichokichukulia kuwa ni kutotendewa haki Vinicius.

Soma pia: City waandika historia ya mataji manne ya ligi mfululizo

Rodri, 28, alichangia pakubwa wakati City iliizuia Arsenal kushinda Ligi kuu ya England msimu uliopita na alitajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano ya Euro 2024 wakati Uhispania iliibuka mshindi nchini Ujerumani. Rodri alitumia lugha ya kidiplomasia wakati akizungumzia suali la Real kutoonekana kwenye hafla hiyo. “Wana uamuzi wao, hawakutaka kuwa hawa kwa sababu zao,” alisema. “Ninaangazia tu klabu yangu na wachezaji wenzangu.”

Vinicius Jr
Vinicius Jr alisema hakushinda tuzo ya Ballon d’Or kwa sababu ya vita vyake dhidi ya ubaguzi wa rangiPicha: Ruben Albarran/ZUMA/picture alliance

Vini aapa kuendeleza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi

Staa huyo amesema ataendelea kupiga vita ubaguzi wa rangi hata kama harakati zake ndizo zilifanya asishinde Ballon d’Or. Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na mchezaji huyo.

Baada ya kuorodheshwa wa pili katika tuzo hiyo, aliandika kwenye mitandao ya kijamii. “Nitafanya mara kumi zaidi kama lazima nifanye hivyo. Hawako tayari,” aliandika Vinicius, 24,  kwenye X. Usimamizi wake ulieleza kuwa alimaanisha ataendeleza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na anaamini ndicho kilifanya ashinde tuzo hiyo, akisema kuwa “ulimwengu wa kandanda hauko tayari kumkubali mchezaji anayepigana dhidi ya mfumo.” 

Soma pia: Vinícius Junior aishtumu La Liga kwa kutopambana na ubaguzi

Vinicius alifunga magoli 24 na kutoa asisti 11 katika mechi 39 kwenye mashindano yote wakati aliingoza Madrid kubeba mataji matatu msimu uliopita.

“Kama vigezo vya tuzo havimpi ushindi Vinicius, basi vigezo hivyo hivyo vinapaswa kumpa Carvajal ushindi,” Imesema Real Madrid.

“Kwa sababu haijawa hivyo, ni wazi Ballon d’Or-UEFA hawaheshimu Real Madrid. Na Real Madrid haiendi mahali ambako haiheshimiwi.”

Ujumbe wa Madrid waliokuwa kwenye orodha ulijumuisha Kylian Mbappe, Antonio Rudiger, Fede Valverde na Jude Bellingham. Tuzo hizo zinatokana na upigaji kura wa jopo la waandishi wa habari za michezo kutoka nchi 100 za juu katika orodha ya viwango vya FIFA. Real Madrid ilishinda tuzo ya timu bora wakati Carlo Ancelotti akishinda Kocha bora.

Ballon d'Or mjini Paris
Aitana Bonmati (gauni nyeupe) alishinda tuzo yake ya pili mfululizo ya Ballon d’Or ya wanawakePicha: FRANCK FIFE/AFP

Bonmati ashinda kwa mara ya pili mfululizo

Staa wa Barcelona na Uhispania Aitana Bonmati alishinda tuzo yake ya pili mfululizo ya Ballon d’Or ya wanawake. Aliiongoza klabu yake kuweka historia ya kushinda mataji manne katika msimu mmoja na pia taji la Nations League na timu ya taifa.

Bonmati, 26, anaungana na mchezaji mwenzake wa Barcelona Alexia Putellas kuwa wanawake pekee walioshinda Ballon d’Or mara mbili tangu tuzo hiyo ilipoanzishwa mwaka wa 2018.

Soma pia: Lionel Messi aweka rekodi kwa kushinda tuzo ya nane ya Ballon d’Or

“Nisingefanikiwa pekee yangu, nina bahati kuzungukwa na wachezaji wanaonifanya niwe bora kila siku,” alisema Bonmati.

afp, reuters, dpa, ap

Related Posts