Wanafunzi wote Hazina ya Magomeni wafaulu kwa alama A darasa la saba

 

WANAFUNZI wote wa Shule ya Msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam wamefaulu kwa alama A kwenye matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa leo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Matokeo hayo yametangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani NECTA mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo.

Kwenye matokeo hayo, shule ya Hazina imepata wastani wa ufaulu wa alama 287.3 kwa wanafunzi wote 27 kufaulu kwa alama A na hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepata B, C, D wala F kwenye somo lolote.

Omari Juma, ambaye ni Mkuu wa shule hiyo, alisema wameyapokea matokeo hayo kwa furaha kubwa kwani wanafunzi wote wamepata alama A kwa masomo yote.

Aliwapongeza walimu na watumishi wa shule hiyo kwa namna wanavyojitoa kufundisha usiku na mchana hali ambayo imewasababishia matokeo mazuri.

“Tunampongeza pia Mkurugenzi wa shule kwani wamekuwa akitimiza mahitaji ya walimu na shule kwa ujumla amekuwa akituwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi, ukiniuliza siri ya mafanikio haya nitakwambia ni mazingira bora ya ufundishaji,” alisema na kuongeza

“Hapa Hazina walimu wana ari kubwa sana ya kufundisha wanafundisha kwa upendo na wanaipenda kazi yao na ukiangalia hata matokeo ya mwaka jana yalikuwa kama haya haya na darasa la nne nako ukiangalia tumekuwa tukifanya maajabu kama haya haya,” alisema.

“Tunawaahidi wazazi wa wanafunzi kwamba moto huu hautapoa tutaendelea kufanya vizuri mwaka hadi mwaka na ukiangalia matokeo yetu ya nyuma utabaini kuwa sisi tunasonga mbele na huwa hatugeuki nyuma, kwenye mitihani ya majaribio tumekuwa tukiongoza kwenye wilaya ya Kinondoni na hata mkoa tuko vizuri,” alisema

About The Author

Related Posts