Wanachama wa CCM wadaiwa kujiunga na upinzani – DW – 29.10.2024

Chama hicho tawala ambacho mwishoni mwa wiki kilikamilisha hatua yake ya kwanza kuwapata wagombea, kinamulikwa kwa namna kitakavyoweza kuvuka vuguvugu hilo la shutuma kabla ya kuanza  mchaka mchaka wa kampeni kuelekea siku ya upigaji kura Novemba 27.

Kumekuwa na wimbi la baadhi ya wanachama wake wanaoendelea kupiga hodi katika ofisi za chama hicho, wakilalamika kukatwa kwa wagombea wao licha kwamba baadhi waliondoka na ushindi mkubwa katika mchakato wa mchujo wa kura za maoni, kura mbazo ziligubikwa na hali ya sintofahamu katika baadhi ya maeneo.

Mbali ya kutoa shutuma zao,  baadhi wamekuwa wakichukua hatua za ziada za kukipa mkono wa kwa heri na kwenda upinzani.

Wakati hayo yakiendelea ndani ya chama hicho tawala, upande mwingine upinzani mbali ya kuwapokea wanachama wapya vimekuwa vikijitokeza  hadharani kubainisha namna vinavyoukaribia uchaguzi huo.

Upinzani waapa kubinya mianya ya matokeo ya uchaguzi kuchakachuliwa

Tanzania | ACT Wazalendo
Mmoja wa kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo amesema watadhibiti matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019 ambao wapinzani wanadai ulichakachuliwa.Picha: Office of the First Vice President of Zanzibar

Tayari baadhi ya wagombea wake wameanza kuchukua fomu zilizoanza kutolewa tangu Oktoba 26 na kukamilika hapo Novemba Mosi. Mmoja wa kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo amesema safari hii watakuwa macho ili kuyadhibiti yale yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019 ambao wapinzani wanadai ulichakachuliwa.

Katika hatua nyingine, wanaharakati waliokwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo kusimamiwa na wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ,Tamisemi, wanasema wanakwenda katika mahakama ya rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kuu iliyotupilia mbali hoja zao.

Bob Wangwe ambaye ni miongoni mwa waliofungua kesi hiyo anasema uamuzi wa mahakama kuu umewavunja moyo wapigania demokrasia ya kweli. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na serkali zinaonyesha zaidi ya wapigiga kura milioni 31 wamejiandikisha katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mwandishi: George Njogoa- DW Dar es Salaam

Related Posts