Wasiwasi umeongezeka kufuatia hatua ya Israel kupitisha sheria ya kutaka kulizuia shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina kufanya shughuli zake Ukanda wa Gaza.
Wasiwasi huo unakuja wakati Wapalestina wanaendelea kufukua vifusi kaskazini mwa Gaza,huku wengine wakiomboleza kupoteza jamaa zao, baada ya jeshi la Israel kushambulia jengo la maakazi ya raia la ghorofa tano katika mji wa Beit Lahiya.
“Watu wanalia kutoka kwenye kifusi cha jengo hili lakini hakuna anayeweza kuwapa kitu chochote.”
Mahmoud Bassal, msemaji wa shirika la kuwatetea raia Ukanda wa Gaza akizungumzia hali ilivyo baada ya shambulio la Israel huku pia akisema mauaji yanaendelea kwenye eneo hilo.
Watu kiasi 93 wameuwawa kwenye shambulio hilo na wengine 17 hawajulikani waliko huku wizara ya afya ya Gaza ikisema waliouwawa miongoni mwao ni wanawake 12 na watoto 20 wakiwemo watoto wachanga.
Jeshi la Israel halijatowa tamko kuhusu shambulio hilo ingawa limekuwa likisema operesheni yake Kaskazini mwa Gaza ya zaidi ya wiki tatu sasa,inalenga kuwasambaratisha wanamgambo wa Hamas, wanaojipanga upya kwenye eneo hilo.
Wakati huohuo mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa,Francesca Albanese amesisitiza hii leo Jumanne, madai kwamba Israel inaendesha kile alichokiita mauaji ya Kimbari katika Ukanda wa Gaza,akiituhumu nchi hiyo kwamba inataka hasa kuwaondowa kabisa Wapalestina kwenye ardhi yao.Soma pia: Misri yapendekeza kusitishwa mapigano kwa siku mbili Gaza
Mjumbe wa UN na tuhuma dhidi ya Israel
Albanese ni mtaalamu huru na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel tangu mwaka 1967 lakini kwa muda mrefu amekuwa akikosolewa vikali, na kukabiliwa na madai ya kutowa kauli za chuki dhidi ya Wayahudi.
Israel na baadhi ya Washirika wake wamekuwa wakishinikiza aondolewe kwenye nafasi yake kutokana na tuhuma anazozitowa dhidi ya Israel kwamba inaendesha mauaji ya Kimbari.
Aliteuliwa na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lakini hazungumzi kwa niaba ya Umoja huo.
Wasiwasi kuhusu kufungwa kwa UNRWA
Wasiwasi pia umeongezeka kuhusiana na uamuzi wa Israel wa kulipiga marufuku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, kwamba huenda hatua hiyo ikasababisha vifo zaidi vya watoto na kuonekana kama ni aina fulani ya kuwaadhibu raia wote wanaoishi Gaza.Soma pia: Vifaru vya Israel vyazidi kusogelea miji miwili ya kaskazini mwa Gaza
Waziri mkuu wa Ireland Simon Harris ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kutathmini upya mahusiano ya kibiashara na Israel kufuatia sheria hiyo aliyoiita ni ya kufedhehesha. Qatar imeilaani hatua hiyo ya Israel.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema ikiwa sheria hiyo iliyopitishwa Jumatatu itatekelezwa itakuwa na athari kubwa kwa raia.
Msemaji wa Shirika la Umoja huo la kuhudumia watoto,UNICEF, James Elder amsema ikiwa UNRWA itazuiwa kuendesha shughuli zake bila shaka mfumo mzima wa shughuli za kibinadamu Gaza utaporomoka.