Kinana: Katiba mpya, tume huru ya uchaguzi si sababu pekee ya kushinda uchaguzi

Dodoma.  Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema madai ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi siyo kigezo pekee cha kushinda uchaguzi.

Kinana amesema hayo leo Mei 5, 2024 kwenye mkutano na wana-CCM Mkoa wa Dodoma unaofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete.

Amesema hoja za Chadema za kudai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi si kigezo pekee chama cha siasa kushinda uchaguzi, bali kuwe na “sera nzuri, mjipange, mkubalike na mteue watu wanaokubalika,” amesema Kinana.

Akijenga hoja hiyo, Kinana ametoa mfano wa nchi jirani bila kuitaja, kwamba wamepigania Katiba na Tume huru ya uchaguzi kwa muda mrefu na wameipata, lakini kuna watu wamegombea (chini ya katiba mpya) mara sita na hawajashinda uchaguzi.

Amesema CCM haikatai hoja ya Katiba na kwamba suala hilo kwa mujibu wa CCM haliwezi kufanyika sasa.

Kinana amesema pia suala la Tume huru ya uchaguzi, Serikali imefanya marekebisho ya sheria tatu za uchaguzi na zimepitishwa na Bunge na Rais Samia Suluhu Hassan amesaini.

Amesema sheria hizi mpya ni nzuri kuliko zilizopita ambazo kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ziliwapa (upinzani) wabunge 117, wenyeviti wa vitongoji 13,273, mitaa 1,342 na vijiji 2,539.

Pia, amesema suala la Rais kuteua wajumbe wa Tume ya uchaguzi amekubali litafanywa na kamati na uteuzi wa mwenyekiti na makamu Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi majina yatapendekezwa na (Rais) atateua katika majina atakayopelekewa.

Hata hivyo, amesema hakuna Tume ya Uchaguzi duniani ambayo Rais hana mkono wake.

Ametoa mifano kadhaa ikiwamo India kwamba mwenyekiti na makamu wake wanateuliwa na Waziri Mkuu na watu wake, Nigeria Rais ndiye mwenye uwezo wa kuteua mwenyekiti na makamu wake, Afrika Kusini na Ghana marais wana uwezo wa kuwafuta kazi mwenyekiti wa tume na makamu wake.

Kinana ametumia mkutano huo kujibu hoja mbalimbali ambazo zimekuwa zinaibuliwa na Chadema kwenye mikutano na maandamano yake mikoani.

Related Posts