Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa kipaumbele kwenye ujenzi wa miradi ya nishati jadidifu nchini ili kusaidia utunzaji wa mazingira, kuzalisha umeme wa uhakika na kutoa ajira kupitia miradi hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 31, 2024 na Mkurugenzi wa Teknolojia Mbadala na Nishati Jadidifu kutoka REA, Mha. Advera Mwijage alipotembelea mradi wa Mwenga Hydro unaozalisha umeme wa maji wa megawati nne (4) uliopo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Mha. Mwijage amesema kuwa, mradi huo umewezeshwa na Serikali kupitia REA kwa kutoa kiasi cha fedha takribani shilingi bilioni 16.6 ikiwemo shilingi bilioni 10 ya kuwaunganisha wateja na shilingi bilioni 6.6 ya utekelezaji wa mradi huo.
“Sisi kama wakala tunaendelea kufadhili hii miradi kwa kuhamasisha na kuwawezesha wanaojenga miradi ili kuendeleza shughuli za kiuchumi nchini,” amesema Mha. Mwijage
Vile vile, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fursa kwa wabia wa maendeleo ambao wanaisaidia Serikali katika kutekeleza uzalishaji wa umeme kwenye gridi, kusambazia wananchi na kutoa ajira.
Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mwenga Hydro, Deograsias Massawe amesema mradi huo umewezesha wananchi wa vijiji 32 vya Wilaya ya Mufindi kupata umeme wa uhakika hivyo, kuwawezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Ameongeza kuwa, mradi huo umekuwa na faida kwa wajasiriamali kwa kutoa ajira na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ambao umepunguza gharama za uendeshaji shughuli za kiuchumi kutokana na kuachana na matumizi ya mafuta na kuhamia kwenye matumizi ya nishati ya umeme.
Aidha, ameipongeza REA kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 16.6 ambazo zimefanya maunganisho kwa wateja zaidi ya 8000 wa majumbani, hospitalini, mashuleni na kwenye vituo vya afya.
Amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi zikiwemo utoaji wa fedha za kuendesha mradi na Sera wezeshi katika nishati jadidifu.
Mradi umeanza uzalishaji rasmi mwaka 2012 katika Wilaya ya Mufindi na umelenga kuongeza wateja wapatao 2,900 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.