Wasichana kupata ufadhili wa urubani, uhandisi wa ndege

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi amewataka wasichana kutoka familia zisizo na uwezo kiuchumi kuchangamkia mpango wa kuwasaidia kifedha waweze kufikia ndoto zao za kuwa marubani na wahandisi wa ndege.

Akizungumza jana Oktoba 31, 2024 kwenye kongamano la viongozi wanawake katika usafiri wa anga, lililokuwa na kaulimbiu, ‘Kuwawezesha viongozi wa kike wa kizazi kijacho kuinua usafiri wa anga’ amesema Mfuko wa Mafunzo ya Usafiri wa Anga wa TCAA utalenga kusaidia wasichana wenye uwezo wa kimasomo hasa ya sayansi kutoka familia zenye kipato cha chini.

Amesema hilo linatokana na gharama kubwa za mafunzo ya usafiri wa anga ambazo ni kikwazo kwa vijana wengi wenye vipaji nchini Tanzania.

“Gharama za kuwa rubani mara nyingi huzidi Sh150 milioni, jambo ambalo ni gumu kufikiwa na familia nyingi,” amesema.

Amesema kikwazo hicho cha kifedha kimesababisha fani hiyo kubaki kuwa ya wale wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mkubwa kifedha.

“Tunataka kubadilisha hali hii kwa kutoa msaada kwa wasichana wenye uwezo lakini hawana njia za kifedha kufikia ndoto zao,” amesema.

Amesema TCAA inalenga kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye sekta ya anga kutoka asilimia 34 ya sasa hadi asilimia 50 ndani ya miaka 15 ijayo.

“Hili si suala la kufikia idadi fulani tu, ni kuhusu kuendeleza vipaji na bidii vilivyopo tayari miongoni mwa wanawake vijana wa Kitanzania, hasa wale walioonyesha uwezo mkubwa kwenye masomo ya sayansi. Tunaamini anga inapaswa kufikiwa na kila mtu mwenye shauku na ujuzi, bila kujali hali ya kifedha,” amesema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto wa Zanzibar, Riziki Pembe Juma, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo  amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wasichana hasa wakiwa katika umri mdogo.

“Lazima tuwatie moyo na kuwapa ujasiri mapema iwezekanavyo. Hii inamaanisha kuanzisha dhana na mashindano yanayohusiana na usafiri wa anga katika shule za msingi ili wasichana wadogo waone kwa kuwaonyesha fursa halisi, tunavunja vikwazo kabla hata havijaanza kuundwa,” amesema.

Amesema mitazamo ya kijamii inaathiri matarajio ya wasichana.

“Wasichana wengi hukua wakiamini fani za usafiri wa anga si kwa ajili yao kwa sababu hawaoni wanawake kutoka mazingira kama yao katika nafasi hizo. Tunapowatia moyo mapema na kuwapa mifano halisi, tunawaonyesha inawezekana na wanaweza kufikia ndoto zao,” amesema.

Amepongeza mpango wa TCAA akiuita ‘mpango wa kubadilisha hali’ kwa wanawake vijana nchini Tanzania ambao vinginevyo wangeweza kushindwa kufikia ndoto zao kutokana na vikwazo vya kifedha.

“Tunashuhudia juhudi za mabadiliko zinazolenga moja kwa moja usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake vijana kote nchini,” amesema.

Rubani wa Kitanzania, Neema Swai aliyerusha ndege ya mizigo kutoka Marekani hadi Tanzania hivi karibuni, alizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo wanawake vijana kwenye sekta ya anga.

“Gharama ni kubwa sana kwa familia nyingi, ndiyo maana tunapata rubani wengi wakitoka kwenye familia zenye uwezo mkubwa kifedha,” amesema.

Neema anaona mpango mpya wa TCAA kuwa hatua muhimu katika kuleta fursa halisi kwa wasichana.

“Mfuko wa mafunzo maalumu, hasa kwa wanawake vijana kutoka familia zisizo na uwezo kifedha unaweza kufungua milango ambayo imefungwa kwa muda mrefu. Hii itakuwa na faida kubwa kwa wasichana ambao wana ndoto za kuwa marubani lakini hawawezi kumudu gharama. Inamaanisha wanapata fursa halisi ya kufikia ndoto zao,” amesema.

Amesema mpango huo pia utaleta nguvu kwenye sekta kwa kukuza utofauti na ushirikishwaji.

“Kwa kufungua milango kwa wanawake wengi vijana kutoka mazingira mbalimbali, hatuendelezi tu haki, bali pia tunaboresha sekta kwa mawazo mapya na njia mpya,” amesema.

Related Posts