Sigara, pombe chanzo magonjwa ya moyo kwa watoto

Wakati takwimu za Wizara ya Afya zikionyesha watoto wawili kati ya 100 wanazaliwa na matatizo ya moyo, wataalamu wameshauri kina mama kuzingatia afya wawapo na ujauzito ili kuepuka kupata watoto wenye maradhi hayo.

Wameshauri kina mama wajawazito kutokunywa pombe, kutovuta sigara (kukaa mbali na moshi wa sigara, tumbaku) huku wakisisitiza ulaji wa vyakula bora ili waweze kujifungua watoto wenye afya.

Kwa mujibu wa chapisho la Taasisi ya Kitaifa ya Afya (NIH) ya Marekani, siku 1,000 za kwanza za maisha ya mtoto, ambazo ni kuanzia mwanzo wa ujauzito hadi anapotimiza umri wa miaka miwili, ni kipindi bora kuweka msingi wa afya nzuri na maendeleo ya mtoto.

Kuna mengi yanayoweza kufanywa kuboresha mtindo wa maisha kabla, wakati na baada ya ujauzito ili kuhakikisha afya bora ya mtoto, ikiwemo kutotumia tumbaku, pombe au dawa za kulevya wakati wa ujauzito.

Kujifungua kabla ya wakati, kutenguka kwa kondo la nyuma na ukosefu wa ukuaji wa ndani ya kizazi (IUGR) vinahusishwa na kuvuta sigara wakati wa ujauzito. Mama kuvuta sigara au moshi wa sigara kutoka kwa mtu mwingine, kunasababisha hatari ya kujifungua mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati.

Tovuti ya afya ya Indirect inasema ikiwa mama ni mjamzito au anapanga, basi njia salama ni kutokunywa pombe kabisa ili kupunguza hatari kwa mtoto, kwani kunywa wakati wa ujauzito kunaweza kusababisha madhara ya muda mrefu kwa mtoto, yaani kadiri anavyokunywa ndivyo hatari inavyoongezeka.

Pia, tovuti hiyo inaeleza kuwa kunywa pombe kupita kiasi, hasa kulewa kunaweza kusababisha kuharibika kwa mimba katika hatua za mwanzo za ujauzito.

“Wakati mwanamke mjamzito anakunywa pombe, hupita kwenye placenta na inaweza kuathiri maendeleo ya mtoto. Hii hutokea wakati wote wa ujauzito, si tu katika wiki chache za kwanza,” inaeleza tovuti hiyo.

Akifafanua kitaalamu, Mkurugenzi wa Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Angela Muhozya anasema sigara ambayo ina ‘carcinogens’ pamoja na pombe zinaathiri hatua za mwanzo wakati mtoto anatengenezwa kwa kuwa mama na mtoto wanachangia mzunguko wa damu. Hivyo, damu ikiwa na sumu inaenda kwa mtoto.

“Kwenye sigara au chochote ambacho mama anavuta kuna sumu zinazokwenda kuathiri afya ya mtoto, matatizo ya moyo aidha matundu au mishipa inakuwa haipo sehemu yake, na hata vinasaba pia,” anasema.

Kwa upande wa pombe, anasema mara nyingi inaathiri utengenezwaji wa mtoto, hasa katika ubongo na mishipa ya fahamu kwa yule mzazi anayekunywa pombe, hususan miezi ya mwanzo.

“Mzazi unakuwa kama anamlewesha mtoto badala ya kumpa virutubisho, kwani pombe ina kiwango cha kilevi (alcohol) tofauti tofauti ambayo inaathiri utengenezaji wa mtoto,” anabainisha Dk Muhozya.

Akitaja sababu nyingine, anasema kuna magonjwa ya kuambukiza kama ya zinaa na virusi ambayo mama akiyapata akiwa mjamzito yanasababisha madhara, ikiwemo katika DNA ya mtoto.

Amesisitiza kuhusu lishe ya mama, akisema inapaswa kuwa bora na kamili, hususan katika kipindi cha uzazi kuanzia miaka 14 na kuendelea, wanapaswa kula chakula bora, kwani ni kipindi cha kuhifadhi virutubisho vinavyosaidia kupata mtoto kamili.

Anasema mama asipopata lishe bora basi apate virutubisho kwa njia ya ‘supplement’, hususan kabla au mwanzoni mwa ujauzito. Pia, ametoa rai kwa kina mama wawe wanakagua afya zao mara kwa mara pamoja na kula vyakula bora vya protini na vitamin.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge anasema wajawazito wanatakiwa kula vyakula bora, huku akisisitiza kuacha uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kipindi cha ujauzito.

Dk Kisenge, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, anasema utumiaji wa vilevi ni moja ya visababishi mtoto kuzaliwa na magonjwa ya moyo.

“Nawasihi wazazi kuleni vyakula bora, ikiwa ni pamoja na mboga za majani na matunda, fanyeni mazoezi ili kupunguza uzito mkubwa unaoweza kusababisha mama kujifungua mtoto mwenye kisukari na ugonjwa huu unaweza kusababisha mtoto kupata magonjwa ya moyo,” anasema Dk Kisenge.

Dk Kisenge anabainisha hayo wakati takwimu kwa ujumla zikionyesha ongezeko la magonjwa ya moyo, zaidi ya watu milioni 20 kwa mwaka duniani kote hupata magonjwa ya moyo, wakati asilimia 80 hupata mshtuko wa ghafla wa moyo.

Katika Siku ya Moyo Duniani, maadhimisho yaliyofanyika Septemba 29, 2024 JKCI, Dk Kisenge anasema mpaka sasa wamezunguka mikoa 16 na wameona wagonjwa 17,000 na kati ya hao, asilimia 25 walikuwa wana matatizo ya moyo, huku asilimia 9 wakiwa hawajui kuhusu afya zao.

“Kwa hapa Tanzania, asilimia 13 wana magonjwa ya moyo, tunapopita wodini asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowaona wengi wanakuwa na magonjwa yasiyoambukiza, kama vile moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu pamoja na kiharusi,” anasema Kisenge.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto JKCI, Sulende Kubhoja anasema kumekuwa na dhana katika jamii kuhusu magonjwa ya moyo ni kwa watu wazima tu lakini siyo kweli, kwani yanawapata hata watoto wadogo.

“Jamii inatakiwa kufahamu kuwa hata watoto wadogo wanaumwa magonjwa ya moyo, lakini kwa upande wao, mara nyingi huwa ni magonjwa ya kuzaliwa nayo, ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake, lakini pia kuna ambao wanayapata ukubwani na huwa ni matatizo ya valvu.

“Mara nyingi watu huwatazama watu wazima na kusahau watoto wadogo, jamii ikumbuke watu wote iwe ni kwa mtoto ambaye hajazaliwa au aliyezaliwa mwenye ugonjwa wa moyo na yule mkubwa wote ni sawa inatupasa kuwakumbuka,” anasema Dk Kubhoja, ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya moyo kwa watoto JKCI.

Mmoja ya wazazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo, Zuhura Mkamba anashukuru kwa faraja ya kuona madaktari na wahudumu wengine wa afya wanajitoa kwa watoto wao.

Related Posts