Rostam atoa neno uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taifa Group Ltd, Rostam Aziz amezungumzia umuhimu wa mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na kampuni ya DP World katika kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Rostam akizungumza katika mkutano wa kilele wa Financial Times Africa uliofanyika jijini London, Uingereza hivi karibuni alisisitiza umuhimu wa mkataba huo kwa kuzingatia kuwa Tanzania iko katika eneo muhimu kijiografia, ikiwa imezungukwa na nchi saba zinazoitegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya biashara.

“Uzoefu wetu na uendeshaji wa bandari kabla ya hili umekuwa wa kusikitisha, na ufanisi umekuwa wa kiwango cha chini. Tumekuwa na meli zinazongoja kwa muda mrefu bandarini, jambo ambalo linagharimu watumiaji wa mwisho na uchumi kwa ujumla,” alisema.

Kwa mujibu wa Rostam, DP World ni mshirika anayefaa kwa sababu ya rekodi nzuri na masilahi ya kijiografia yenye kuzingatia mahitaji ya Dar es Salaam.

Alisema uwekezaji huo ni njia ya kuhakikisha ufanisi na kuimarisha uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

“Ikiwa utaenda Dar es Salaam na kutazama baharini, utaona kama vile kuna miti mingi ya Krismasi kutokana na meli nyingi zinazongoja kutia nanga. Hivyo, tulihitaji kutafuta mwendeshaji mwenye uzoefu, rekodi nzuri, na masilahi kijiografia kuhusu Dar es Salaam,” alisema.

Akizungumzia mradi wa gesi asilia (LNG), alisema ulistahili kuanzishwa mwaka 2014, lakini kutokana na changamoto mbalimbali, haukufikia hatua hiyo. Alisema ni matumaini yake kuwa mradi huo utaleta mabadiliko makubwa kwa uchumi wa Tanzania.

Mkutano wa Kilele wa Financial Times Africa ulihudhuriwa na wakuu wa nchi, magavana wa benki kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, mawaziri wa Uingereza, IMF, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa, mabenki, na wadau wengine.

Related Posts