Kipigo dhidi ya Yanga hakijaikatisha tamaa Singida BS

LICHA ya Singida Black Stars kupoteza mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kwa bao la Pacome Zouzoua, kocha Patrick Aussems pamoja na kipa wa timu hiyo, Metacha Mnata wamesisitiza bado hawajakatishwa tamaa na kiu yao ya kutaka kubeba ubingwa msimu huu kwani bado nafasi ipo kwao.

Kocha Aussems, raia wa Ubelgiji, alipongeza vijana wake kwa kiwango walichoonyesha, akisema, “Nimefurahishwa na jitihada za wachezaji wangu. Ingawa tumepoteza, kuna mambo mazuri tumeyaonyesha ambayo tutajenga kwenye mechi zijazo.”

Kipigo cha bao 1-0 kilichotokea kwenye Uwanja wa New Amaan kilisababisha Singida kushuka kutoka kileleni, ambapo walikuwa wakiongoza kwa mwezi mmoja.

Katika mchezo huo, Yanga walionyesha uwezo mzuri wa kutengeneza nafasi, lakini Aussems aliamini kwamba wachezaji wake walikuwa na nguvu na ari ya kupambana. “Kila mchezaji alijitahidi na kuna mwanga wa matumaini. Sijawahi kuacha matumaini,” aliongeza.

Kwa sasa, ligi hiyo inaongozwa na Yanga ikiwa na pointi 24, huku Singida ikisalia na pointi 22. Kocha Aussems alisisitiza umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa, akasema, “Ni muhimu kuangalia makosa yetu na kuyarekebisha. Tunahitaji kuwa na umoja zaidi kama timu.”

Mechi ijayo kwa Singida Black Stars ni Jumamosi ya Novemba 2 dhidi ya Pamba. Aussems anaamini kwamba ni fursa nzuri ya kurejea kwenye wimbi la ushindi. “Kila mechi ni fursa, na tutaitumia vizuri. Wachezaji wangu wanaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema kocha huyo.

Aussems alikumbuka jinsi timu yake ilivyoweza kukabiliana na changamoto katika mechi zilizopita, akiongeza, “Tumejifunza kutoka kwa mechi zote. Tumejenga msimamo mzuri, na tunapaswa kuendelea kujitahidi.” Alisisitiza kwamba morali ya wachezaji iko juu, na wanajitayarisha kwa ajili ya mechi ijayo.

Kwa upande wa kipa Metacha aliyewahi kuidakia Yanga, alisema wamesahau matokeo ya juzi na sasa wanaendele a kujipanga upya kwa kuboresha dosari zote walizoonyesha mbele ya Yanga.

“Sisi ni familia, na tutashirikiana kushinda.

Metacha aliyesimama langoni alisema kipigo kimewaumiza kwani walipenda kushinda na kuendleeza rekodi ya kutopoteza mechi, lakini soka ndivyo lilivyo.

“Kwa upande wetu tulipambana kwa kadri tulivyoweza, ila soka lina matokeo ya kikatili tukapoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga, hatuna budi kuyasahau matokeo hayo, badala yake tunapaswa kuangalia mbele, kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Metacha na kuongeza;

“Ligi ya msimu huu ngumu, inahitaji kila mchezaji kujitoa kwa kadri anavyoweza kusaidia timu yake, naamini kwa upande wetu kocha atakuwa ameona wapi tutatakiwa kurekebisha, ile mechi zijazo ziwe kuwa bora zaidi.”

Alizungumzia mwanzo wao katika ligi ulivyokuwa mzuri, kwani hawakupoteza mechi, ila kufungwa na Yanga imewashitua na kuona wakaza zaidi buti. 

“Katika mechi saba, tumepoteza mechi moja dhidi ya Yanga, tulishinda tano na sare moja, tutaendelea kupambana na kuongeza umakini zaidi, kufanya vizuri michezo ijayo mbele yetu,” alisema.

Related Posts