MTIBWA Sugar ni kama yule mnyama anaitwa Ngekewa ambaye porini anapendwa na kundi kubwa la wanyama wenzake.
Hapa kijiweni karibia wote tumekubaliana kuwa tunatamani Wakata Miwa wa Mtibwa Sugar warejee ligi kuu kutoka Ligi ya Championship ambayo wapo hivi sasa.
Kila mmoja ana sababu zake zinazomfanya aombee Mtibwa Sugar ivuke kihunzi kigumu cha ligi ya Championship ili msimu ujao ionekane tena katika Ligi Kuu ambayo timi hiyo ni miongoni mwa klabu zilizowahi kutwaa ubingwa.
Mmoja yeye anaipenda Mtibwa Sugar kwa vile timu hiyo imekuwa daraja la mafanikio kisoka kwa vijana wengi kutokana na fursa ambayo imekuwa ikitoa kwa wachezaji wenye umri mdogo hasa wale wa kituo cha Moro Kids.
Jamaa anatoa mfano wa wachezaji kama Dickson Job, Kibwana Shomary, Shiza Kichuya, Abutwalib Mshery, Ismail Mhesa, George Chota, Nickson Mosha, Omary Marugu na Tepsi Evance ambao Mtibwa iliwapa nafasi wakitokea Moro Kids na wanatamba hapa nchini hivi sasa.
Mwanakijiwe mwingine yeye anatamani Mtibwa Sugar irejee ligi kuu kwa sababu tu ya kulinda historia ambayo imekuwa nayo ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ikiwa inatokea mkoani jambo ambao sio rahisi kwa vile kuna Simba na Yanga ambazo zina nguvu kubwa ya kiuchumi na umati wa mashabiki.
Anaona kuna timu nyingi za mikoani ambazo zimeshindwa kuandika historia hiyo ambayo Mtibwa Sugar iko nayo sasa kucheza Championship hakuendani na heshima ambayo timu hiyo kutoka kule Manungu, Turiani iko nayo.
Lakini mwisho wa siku, ndoto ili zitimie, kunaitajika kuwepo na juhudi za kuhakikisha kile kinacotamaniwa kinafikiwa badala ya kukaa na kutegemea miujiza bila kuvuja jasho.
Tunategemea Mtibwa Sugar itapambana ndani ya uwanja ili iweze kutoa tabasamu kwa wadau kijiweni ambao wengi tunatamani kuona inarudi Ligi Kuu.