Dar es Salaam. Katika makuzi yake, Jane Elias anasema aliambiwa alianza kutembea akiwa na miezi saba.
Amesema wazazi wake walimweleza kuwa walifurahia, ingawa hivi sasa ni mateso kwake.
“Huwa nikivaa viatu vinapinda na kuisha upande mmoja, mwanzo sikuelewa ni kwa nini lakini nikiwa tayari nimeshajitambua na kuwa na maisha yangu, niliamua kwenda hospitali kujua nina tatizo gani.”
“Daktari aliniambia nina matege, miguu imepinda kwa chini, ninapokuwa natembea nasugua ardhi hivyo kusababisha viatu vyangu kuisha upande mmoja,” amesema.
Amesema ni nadra mtu kugundua kama miguu yake imepinda, hata yeye mwenyewe hakuwa anafahamu hadi alipokwenda hospitali, ndipo ikagundulika hivyo.
Hali hiyo pia anayo Zuberi Makura wa Mbeya anayesema hana matege, lakini ana changamoto ya viatu vyake kuisha upande mmoja.
“Huwa sielewi ni kwa sababu gani, kuna muda nahisi ni maumbile yangu ya miguu tu ndiyo yapo hivyo,” amesema.
James Aloyce wa Mwanza amesema, yeye hata akivaa ndala mpya akitembea kwa dakika kadhaa anapozivua zinakuwa zimebonyea kana kwamba zimevaliwa kwa muda mrefu.
“Nakumbuka nilipokuwa mdogo, nilikuwa nataniwa wanasema miguu yangu haina uvungu, hata ndugu zangu hawakupenda niwe navaa viatu vyao,” amesema Aloyce.
Watoto kutembea mapema husababisha matege
Kwa wazazi, kama ulikuwa unafurahia mwanao kutembea mapema, Dk Charles anasema hiyo si hatua nzuri kwa mtoto ila kuna uwezekano ikamsababishia matege.
Watoto wote wanapozaliwa, vimiguu vyao huwa vimejikunja, baada ya muda ndipo vinakuwa sawa, sasa ikitokea mtoto akawahi kutembea mapema hiyo inaweza kumsababishia kupata matege,” amesema.
Amesema, kuna watu huzaliwa wakiwa na matege na wengine wanayapata baada ya kuzaliwa.
“Wanapoanza kukanyaga kuna wengine hapo ndipo yanatengeza matege, hasa pale mtoto anapowahi kutembea,” amesema.
Amesema kitaalamu, hawapendelei sana mtoto kutembea mapema, mfano kuanzia miezi saba kushuka chini si ukuaji mzuri kwake.
“Tunashauri angalau aanze kutembea akiwa na miezi tisa, lakini chini ya hapo si nzuri kwake kwa kuwa baadaye inaweza kumsababishia kupata aina fulani ya matege.
Hata hivyo, Dk Charles amesema wapo watoto ambao akifika miaka miwili matege yanakuja, kwa kuwa anapotembea anabeba uzito.
“Baadaye huwa yanapotea akifika miaka mitatu, kwa wale ambao hayapotei ndio wanafanyiwa oparesheni.”
Amesema mtoto mwenye matege akitibiwa yanarekebishika kulingana na aina ya matege, japo upasuaji unafanyika mtoto akifika miaka mitatu hadi minne.
“Huwa tunaacha miaka hiyo ili kuruhusu ‘recovery’ yawezekana ikapona yenyewe au ni madini, kama ni madini atapewa vitamini akifika miaka minne kama hajapona ndipo tunafanya oparesheni,” amesema.
Chanzo viatu kuisha upande mmoja
Andrew Charles, ambaye ni Daktari kutoka Hospitali ya CCBRT amesema viatu kuisha upande mmoja inategemea na maumbile ya mtu, mara nyingi hutokea kwa wenye matege.
Matege ni hali ya mifupa kuwa laini na dhaifu, hali hii husababishwa na kuwepo kwa upungufu endelevu wa madini ya vitamini D.
Dk Charles amefafanua kuwa kwa wenye matege, akivaa viatu mara nyingi huisha upande mmoja kwa kuwa kuna upande anakanyaga zaidi kuliko mwingine.
“Wale wenye matege ya nje, kiatu kitaisha zaidi upande wa nje, na kuna wale ambao wana matege huwa tunayaita matege ya kike, hawa ni wale ambao wakitembea magoti yanasuguana.
“Wenye matege ya aina hii, viatu vyao mara nyingi vinaisha kwa ndani,” amesema.
Dk Charles amesema kila mtu kuna upande ambao anaukanyagia, lakini ikitokea una matege kidogo kuna upande lazima utaukanyagia sana na hivyo kusababisha viatu kuisha upande mmoja.
“Ukiona unavaa kiatu halafu kinaisha upande mmoja au kinapinda kuna aina ya ‘vimatege’ unavyo sema kwa haraka haraka huwezi kuviona,”
“Wengi huwa na vitege vidogo ambavyo huwa havina shida, na inapokuwa matege kama matege kabisa hiyo ni ya kitaalamu na huwa yanatofautiana, lazima ujue yamepindia wapi ni mfupa gani umepinda na yamesababishwa na nini?,” amesema.