Dar es Salaam. Sasa ni rasmi kwamba mkataba wa ununuzi wa umeme (PPA) kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Songas umemalizika rasmi jana Oktoba 31, 2024.
Hatua hii inaiweka Songas kwenye njia ya kudai takriban Dola milioni 90 za Marekani (takribani Sh250 bilioni) kutoka Tanesco ambazo ni malimbikizo endapo hakutakuwa na makubaliano ya kuongezwa muda wa PPA.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Felchesmi Mramba wamelithibitishia gazeti la The Citizen kuhusu kumalizika kwa mkataba huo.
“Umeshamalizika. Kwa bahati mbaya niko kwenye mkutano hivi sasa siwezi kueleza zaidi,” amesema Dk Biteko.
Alipoulizwa ni nini kitakachofuata baada ya kumalizika kwa PPA, Mramba amesema, “siwezi kusema chochote kwa sababu mkataba unamalizika leo (Oktoba 31, 2024) kwa hiyo hatujafanya mipango yoyote.”
Hata hivyo, taarifa zimeeleza kumalizika kwa PPA kuna maana kuwa Songas inaweza kuanza mchakato wa kusitisha shughuli zake katika kituo cha umeme cha Ubungo na kugawa hisa zote zilizobaki kwa wanahisa wake.
Kwa sasa, Serikali kupitia Tanesco, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na Kampuni ya Maendeleo ya Fedha Tanzania (TDFL) wanamiliki asilimia 46 ya hisa za Songas. Hisa zilizobaki zinamilikiwa na Globeleq.
Fedha za malimbikizo ambazo Songas inaweza kudai kutoka Tanesco zimeongezeka kutoka kiasi kilichokokotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka jana.
Katika ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2022/23, CAG, Charles Kichere alionya dhidi ya kuchelewesha kusuluhisha migogoro mitatu kati ya Songas na Tanesco, ambayo ilikuwa imetajwa kuwa Sh109.07 bilioni wakati huo. Mapitio ya CAG yalionyesha migogoro inayojirudia ambayo haijasuluhishwa tangu mwaka 2022.
Kichere alisema Tanesco ilipinga malipo yenye thamani ya Sh67.94 bilioni.
Hata hivyo, Songas iliendelea kujumuisha gharama za tozo za ukarabati wa mali (sinking) kwenye ankara za kila mwezi kuanzia Agosti 2022 hadi Juni 2023, zikiwa na thamani ya Sh29.34 bilioni, licha ya taarifa ya mgogoro iliyotolewa na Tanesco Desemba 2022.
“Zaidi ya hayo, ankara ya Januari 4, 2023, yenye thamani ya Sh23.94 bilioni na Dola milioni 4.02 kwa Desemba 2022, ilizua mgogoro kuhusu deni la Sh11.78 bilioni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayodaiwa na TRA kutokana na kukosekana kwa nyaraka za kuunga mkono,” alisema CAG mwaka jana.
Mei, mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alilieleza Bunge kwamba, Tanzania ingezingatia masilahi ya kitaifa kabla ya kutoa ruhusa ya kuongeza mkataba kati ya Tanesco na Songas.
Alisema timu ya majadiliano ya Serikali iliundwa Aprili 2023 na kwamba, majadiliano yalitarajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa mkataba.
Ingawa Serikali imeongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwa megawati 662 kutokana na kuwashwa kwa mitambo mitatu kati ya tisa katika mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), umuhimu wa vyanzo mbadala bado unahitaji kusisitizwa.
Uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia hutoa nguvu muhimu kwenye gridi ya Taifa hasa wakati wa ukame.
Wataalamu wa ndani wanasema kwa senti za Marekani 4.9 kwa kilowati kwa saa (kWh), Songas imekuwa ikiuzia Tanesco umeme kwa viwango vya bei nafuu zaidi.
Katika pendekezo la kuongeza mkataba wa PPA kwa miaka sita, kampuni hiyo ilipunguza bei hadi senti 3.9 za Marekani kwa kWh bila kujumlisha gharama za gesi asilia.
Gharama za gesi zinazotarajiwa kujadiliwa zikijumlishwa bei itakuwa senti 6.82 za Marekani kwa kWh.
Kwa mujibu wa watu walio na ufahamu kuhusu suala hili, bado ni chini ya senti 11 za Marekani kwa kWh ambazo Tanesco inawatoza wateja wake.
Kinyume chake, uchambuzi unaonyesha Tanesco italazimika kulipa takribani senti nane za Marekani kwa kWh iwapo itaagiza umeme unaozalishwa kwa maji kutoka Uganda na Zambia, huku gharama zinazotarajiwa za uagizaji kutoka Ethiopia zikijumuisha gharama za usafirishaji zikiwa na makadirio ya senti 7.78 za Marekani kwa kWh.
Bei ya senti 3.0 kwa kWh kama ilivyopendekezwa na Serikali, kwa mujibu wa wachambuzi wa ndani, haitakuwa kivutio kwa wawekezaji wa kimataifa wa kampuni hiyo ambao hawatakubaliana kuwekeza kwenye PPA iliyoongezwa na kufanyia ukarabati mitambo kama inavyohitajika.
Tangu mwaka 2012, Songas imelipa Sh180 bilioni kwa Serikali.