Ndoa mseto ni muunganiko kati ya Wakatoliki na waumini wa madhehebu mengine ya Kikristo kama Walutheri, Waanglikana au makanisa ya Kipentekoste.
Pia, inaweza kuhusisha muumini wa Kanisa Katoliki na Muislamu na baada ya kufunga ndoa, kila mmoja huwa anaendelea kuabudu katika dhehebu lake; Muislamu ataendelea kwenda msikitini na Mkatoliki ataendelea kusali kanisani.
Mwananchi limezungumza na Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini kuhusiana na ndoa za aina hii naye alikiri kuwa Kanisa Katoliki linazifungisha kama kawaida.
Alisema wapo Waislamu wengi tu ambao wamefunga ndoa hizo mseto na Wakatoliki na baada ya ndoa, wanaoamini kwenye ukatoliki huendelea kupokea sakramenti zao kama kawaida.
“Kanisa Katoliki inazitambua na ndiyo maana inazifungisha lakini tunazingatia mambo mengi kabla ya kuzifungisha ndoa hizi mseto,” anasema askofu Kilaini.
Hata hivyo amekiri kwamba ni rahisi zaidi kufunga ndoa mseto kati ya Mkatoliki na Mlutheri au Muanglikana kuliko madhehebu na dini nyingine.
Askofu huyo anaeleza kwamba kwa dini zingine, ikiwemo zile zinazokubali ndoa za wake wengi au talaka, ndoa mseto hazikabiliwi na changamoto kubwa.
Hata hivyo, anasema Kanisa linaangalia mambo kadhaa kabla ya kuidhinisha ndoa ya aina hiyo. “Tunawaeleza kuwa, ikiwa mmoja ataamua kuongeza mke kwa mujibu wa dini yake, sisi kama kanisa hatutavunja ndoa hiyo. Kwa hiyo, kabla ya kufunga ndoa mseto, wenzi wanapaswa kufikia makubaliano kamili. Kuna mifano ya ndoa mseto, kama kati ya Mkatoliki na Muislamu, ambapo Mkatoliki anaendelea kusali kanisani na kupokea sakramenti zake,” alisema Askofu Kilaini .
Hatua za kufuata ukitaka kufunga mseto
Askofu Kilaini anasema ili muumini aweze kufunga ndoa ya mseto hana budi kwanza kabisa kupata kibali kutoka kwa askofu wake.
“Unapokwenda kuomba kuifunga, padri akiona hautatetereka, ndipo naye anaomba ruhusa kwa askofu ambaye akiridhika, inafungwa katika misingi ya kanisa Katoliki ambayo inatambua mke mmoja na hakuna talaka
Anasema wanaangalia pia vitu vingine vingi kutokana na ukweli kwamba kanisa likitoa ruhusa ndoa ikafungwa kisha muumini wa dini nyingine akawa haelewi na wakaachana ni kama wanampa dhuluma yule Mkatoliki.
Ugumu wa ndoa mseto na tamaduni za dini nyingine
Kwa Wakatoliki, Ndoa Takatifu ni Sakramenti ambayo ni alama ya muungano wa daima hadi pale kifo kitakapowatenganisha.
Akizungumzia imani ya Kiislamu, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema huwa hawazitambui ndo mseto.
“Kwa sababu ni kiumbe wa Mungu na imani yake anayo hajaikana, ataedelea kusali kama kawaida, lakini hatumtambui kama aliyeoa,” anasema.
Japo mifano ipo, Sheikh Kitogo anasema katika uislamu hakuna ndoa ya mchanganyiko wa dini tofauti na Muislamu anayefanya hivyo ikitokea wamepata watoto katika sheria ya dini yao, mtoto anayezaliwa na Muislamu, huyo naye ni muislamu.
“Mtume ametufundisha kila mtu anayezaliwa ulimwenguni hapa ni Muislamu, isipokuwa wazazi wake wanamuunganisha mtoto kwenye dini ya Kiyahudi, Kikristo au zinginezo, lakini sisi tuamhesabu ni Muislamu,”.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambaye pia ni Katibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka amekwenda mbali zaidi na kueleza kwenye uislamu ukiachana na ndoa za waumini wa dini hiyo, wanaitambua ndoa ya mwanaume Muislamu na mwanamke mkristo.
“Pia hatuitambui ndoa ya mwanamke muislamu na mwanaume mkristo, ukiniuliza ni kwanini tutambue ya mwanaume musilamu na mwanamke mkristo na hapo hapo tusiitambue ya mwanamke muislamu na mwanaume mkristo, utaratibu huo ni wa dini unahitaji maelezo mengi na ni jambo la kisheria na lina rai nyingi za wanazuoni,” anasema.
Anasema uislamu unaitambua ndoa ya kikristo endapo mke na mume wote ni wa imani hiyo na wakaamua kuingia kwenye uislamu.
“Hawa hawatofungishwa ndoa ya Kiislamu, wataendelea na ndoa yao ile ile ya kikristo na uislamu utaitambua ndoa hiyo,” anasema.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro anasema ili ndoa ifungwe kuna taratibu za awali wanandoa hupaswa kuzifuata ambazo kwanza ni kukutana na mchungaji.
“Hapa ndipo linaweza kuibuka ili la mmoja wao kuwa Mkatoliki na mwingine M-KKKT hapo wataeleza kila mmoja baada ya ndoa ataendelea kuabudu kwenye kanisa lake baada ya kukubaliana.
Anasema kwa mazingira ya sasa, ndoa itafungwa upande wa mwanaume na kanisa litataka barua ya kanisa ambalo mwanamke anasali.
“Lakini kama ikitokea mwanamke ndiye ana nguvu na ndoa inafungwa kanisa lake, basi yule mwanaume atapewa maelekezo ya kwenda kwa Paroko wake ambaye ataandika barua ya kumtambua,” anasema.
Anasema kwa KKKT, ndoa mseto zinafungwa baada ya kuwepo kwa mazungumzo ya kichungaji kati ya kanisa na kanisa.
“Kuna vitu tumekubaliana na ikitokea labda muumini wetu akafunga ndoa na muumini wa dhehebu jingine wakafunga Serikalini. “
Akimshawishi mwenzake kurudi kanisani ikashindikana, yeye akiamua kumrudia Mungu wake kanisa litaangalia na likijiridhisha litampokea, japo huwa hatupendi vitu hivyo vitokee,” anasema
Mchungaji Richard Hananja anasema Mwenyezi Mungu ni wa wote hana dini, kinachotakiwa ni upendo wa wanandoa bila kujali unaabudu dini au dhehebu gani.
“Tatizo huwa linakuja pale mnapoanza kudharauliana, mmoja akiitwa na kiongozi wa dini fulani ona kama sio mtumishi wake, jambo ambalo halifai.
“Wanandoa wanapaswa kutambua ibada inaanzia nyumbani sio makanisani, wote ni watu wa Mungu, hivyo mnapooana kwenye imani tofauti mkubaliane huo ndiyo umoja wa kiroho, mkianza kubaguana hata watoto mtawagawa wasijue waende wapi, tunasahau Mungu hana dini,” anasema.
Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Luguluni, Charles Mjema anasema makanisa ya Kiadventista yanatambua ndoa za aina tatu, ya kimila, ya Kanisa na ya Serikali. “Ndoa ya Kanisa ina mambo matatu, kiapo, cheti na maombi ya Baraka, ambayo ya Serikali ina cheti na kiapo na ya kimila haina vitu vyote hivyo isipokuwa ina mambo yake ya mila.
“Waumini wetu wakifunga Serikalini, kanisa halitawatenga wala kuwahukumu tutaendelea kuwaheshimu kama wanandoa na kuwasaidia lakinivhatufungishi ndoa mseto,” anasema.
Anasema kwa imani ya Kiadventista, ili ufungishwe ndoa lazima uwe muumini wa kanisa hilo, uwe hujawahi kuwa na ndoa nyingine na ikifungwa haina kuachana hadi mauti au mmoja alikosa uaminifu na taratibu za kiserikali ziwe zimefuatwa. Kama kanisa hakuna ajenda ya talaka, kanisa halina mamlaka hiyo,” anasema.
Nini hutokea wanandoa wakishindwana
Askofu Kilaini anasema, hadi kufungisha ndoa mseto kuna vitu vingi kama kanisa inavizingatia kwa wale wa madhehebu na dini nyingine.
“Kwa Muislamu anayemuoa Mkatoliki uwezekano upo lakini huwa ni ngumu kutoa ruhusa, tunazingatia vitu vingi hadi kutoa ruhusa ya ndoa hiyo,” anasema Kilaini.
Anasema wapo ambao wameishi pamoja na kuzaa watoto na kuwa waaminifu katika maisha yao hayo, hatari ya kuja kuharibika ni ndogo.
Anasema watu wanaopendana ni ngumu mmoja kumdhalilisha mwingine, kwani wanapofunga ndoa mseto ni ya mke mmoja na hawaachani japo kila mmoja anabaki na dini yake.
“Kwa mfano kama huu, kanisa linajiridhisha wanaokwenda kufunga ndoa hawana shida na tunawambia hata mmojawapo akikengeuka hatutengui, inabidi umvumilie kwani hata Wakatoliki wapo wanaokengeuka.
“Tutatengua hiyo ndoa kama tukibaini alipokuwa anaahidi alikuwa anadanganya,” anasema Askofu Kilaini.
Wasiwasi wa wengi ilikuwa ni watoto watakaozaliwa baada ya ndoa mseto watabatizwa na kulelewa katika imani ya Kanisa gani?.
Jambo ambalo linaweza kuonekana ni jepesi, lakini baadhi ya familia zinasema sivyo rahisi kama inayofikiriwa
Akijitolea mfano, Juma Suleiman anasema na mkewe Janeth yeye anapotoa sala, mkewe naye uomba kimya kimya kwa imani yake.
“Kuna nyakati mimi nawapeleka watoto madrasa na kuna nyakati mama yao nae anakwenda nao kanisani, tumeliacha liwe hivyo na watoto watakapokuwa wakubwa watachagua wao wenyewe ni dini gani wataifuata,” anasema.
Hata hivyo, mwanasaikolojia, Deogratius Sukambi anasema watoto kwenda kwenye dini mbili tofauti hakuna athari kwao.
“Athari itakuja kama kutakuwa na mgogoro wa kiimani wa wazazi wa huyo mtoto, lakini kama wamekubaliana .
“Mtoto kwenda kulia na kushoto sio tatizo kwa muktadha wa saikolojia kama wazazi wake wamekubaliana, athari itakuja pale tu baba anampeleka kushoto kisha mama anampeleka kulia halafu kila mmoja anamuaminisha huyo mtoto upande mwingine ni mbaya, hapo ndipo kutakuwa na tatizo, kinyume na hivyo hakuna athari yoyote kwa mtoto,” anasema mwanasaikolojia huyo na mtaalamu wa malezi na mahusiano wa Taasisi ya Wezesha Jamii Organisation.
Akizungumzia kwa muktadha wa sheria, wakili kiongozi wa Haki Kwanza, Aloyce Komba anasema, watu wanapofunga ndoa iwe kanisani au msikitini, wanapaswa kupewa vyeti vya ndoa vya serikali ambavyo havina dini.
“Hata kwa watoto mtakaowazaa, ni uamuzi wenu waabudu dini gani, hakuna sheria inayotambua dini kwa watoto mtakaowazaa,” anasema.