Waziri Aweso avalia njuga suala la upatikanaji wa maji Dodoma

Waziri wa Maji *Mh. Jumaa Aweso* jana amefanya ziara katika maeneo ya Miganga-Mkonze na Nkuhungu kuangalia hali ya upatikanaji wa maji Jijini Dodoma na kutoa maelekezo kwa watendaji maji kuimarisha utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji ili zoezi la uchimbaji visima virefu lianze kwa uharaka.

 

“Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan ametupatia vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji,nataka vianze kazi hiyo hapa Jijini Dodoma ili tuendelee na uchimbaji wa visima virefu kutatua adha ya upatikanaji wa maji iliyosababishwa na ongezeko kubwa la watu Jijini Dodoma.

 

Wakati tunasubiri mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria na Mradi wa Bwawa la Farkwa,endeleeni kuchimba visima virefu maeneo tofauti tofauti ya Jiji ili kupunguza adha ya maji hapa Dodoma.

 

Hakikisheni hamuwabambikizii wananchi bili za maji ni marufuku mtumishi wa mamlaka kufanya hivyo,ili kuondokana na changamoto kubwa iliyolalamikiwa ya kubambikiziwa bili ya maji,tunajiandaa kuja na mfumo wa kulipa maji kadri utakavyotumia“ Alisema Mh Aweso

Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini *Mh. Anthony Mavunde* amemshukuru Waziri Aweso

Kwa jitahada kubwa za utatuzi wa kero ya maji Jijini Dodoma na kuomba rasmi utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa maji wa Nzuguni A ambao utasaidia upatikanaji wa maji katika maeneo ya Ihumwa,Nzuguni,Ilazo,Mlimwa C,Kisasa,Mailimbili,Area C,Area D na Chamwino ili sasa maji yaliyokuwa yakielekezwa maeneo hayo yabadilishwe muelekeo kuwahudumia wananchi ambao awali mgawo wao wa maji ulikuwa mkubwa.

 

Akitia taarifa yake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA) *Mhandisi Aron Joseph* amesema mahitaji ya maji Jijini Dodoma kwa siku ni lita Milioni 147 na huku uzalishaji wa maji ni lita Milioni 79 na hivyo kuwa na upungufu wa lita 68m kwa usiku hali inayopelekea mgao mkubwa wa maji.

Related Posts