Dar es Salaam. Tanzania ikiwa bado haina sera rasmi ya afya ya akili, wataalamu wa saikolojia tiba wametaja masuala ya kiuchumi na kijamii, kama vyanzo vya kuongezeka kwa watu wenye changamoto ya afya ya akili nchini.
Mpaka sasa Tanzania haina sera inayozungumzia afya ya akili na wadau wanasema Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, haina uwezo wa kushughulikia changamoto za sasa na inahitaji kufanyiwa maboresho ili kuendana na mahitaji.
Daktari bingwa wa magonjwa na afya ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Fridah Mtui akizungumza na Mwananchi ofisini kwake kuhusiana na hilo, alisema changamoto za kiuchumi na kijamii zinaweza kuchochea magonjwa ya akili kwa mtu kwa kiwango kikubwa na kumfanya kushindwa kupata nafuu.
“Katika mazingira ya sasa mtu kupata shughuli itakayomuwezesha kujipatia kipato ni changamoto, mwingine anaweza kuwa amesoma ana elimu, ujuzi fulani lakini nafasi ya kupata ajira kwake ikawa ngumu,’’ alisema.
Dk Mtui alieleza kwamba msongo wa mawazo, hasa unapotokana na kutafuta ajira bila mafanikio, unaweza kumfanya mtu kuwa na hali ya msongo wa kudumu, ambayo husababisha kukosa usingizi mzuri na hatimaye kuathiri afya ya akili.
“Na iwapo mtu hana mfumo wa usaidizi wa kijamii, anaweza kuishia kuwa na dalili za magonjwa ya akili,” alisema.
Kwa upande mwingine, alibainisha kuwa watu wenye uchumi mzuri nao pia huathirika, hasa wanaposhindwa kumudu mazingira ya kazi yenye mahitaji mengi au uhusiano mbaya na wenzao, jambo ambalo huongeza msongo wa mawazo.
Alishauri kuwa watu wajitambue mapema na watafute msaada katika vituo vya afya, huku wakipata usaidizi kutoka kwa wapendwa wao.
Dk Edward Kija, mtaalamu wa magonjwa ya ubongo na mfumo wa fahamu, aliongeza kuwa hali ya kiuchumi pia ni sababu kubwa inayochangia changamoto za afya ya akili.
Alisema mara nyingi vijana wanapata msongo wa mawazo kutokana na matarajio yasiyoendana na kipato chao, kama vile hamu ya kumiliki mali, magari, au kuishi maisha ya hali ya juu, jambo ambalo linaathiri afya ya akili.
Pia alisema changamoto za kijamii kama vile kujiona hastahili au kutokuwa na mwonekano mzuri wa kimwili, zinaweza kumsababishia mtu msongo wa mawazo.
Alisema mara nyingi husababisha hali ya kujihisi kutothaminiwa, ambayo huweza kusababisha matatizo makubwa ya afya ya akili na kuchochea hatari kama vile mauaji au kujitoa uhai.
Aidha, Dk Kija alisema tamaa ya utajiri kwa njia za mkato pia inaweza kusababisha matatizo makubwa.
“Mtu anapofikia hatua ya kutafuta utajiri kupitia ushirikina, anaweza kuanza kufanya matendo mabaya kama kuua, kubaka na wengine hulawiti,” alisema.
Hivyo, alisema afya ya akili ina mawanda mapana na si lazima mtu awe na tabia ya unywaji pombe au mavazi duni ili ionekane ana matatizo ya akili.
“Ofisini, wanaume wengi wanaathirika zaidi kwa kuwa hawasemi matatizo yao tofauti na wanawake ambao mara nyingi huongea na kupata nafuu kupitia mazungumzo,” alisema daktari huyo.
Hatari ya kupata sonona huongezeka kuanzia umri wa miaka 20 hadi 64 na hivyo kusababisha idadi kubwa ya vijana kuingia katika utu uzima wakiwa na changamoto za afya ya akili.
Tafiti mbalimbali katika makundi tofauti zinaonyesha viwango vya sonona hutofautiana kati ya makundi hayo.
Kwa mfano, asilimia 5.8 ya vijana wanaonesha dalili za sonona, ilhali kwa wazee, kiwango hiki huongezeka hadi asilimia 44.4.
Daktari Elizabeth Sanga anabainisha kuwa tafiti chache zilizofanyika Tanzania zinaonesha kuwa watu walio katika hatari zaidi ya kupata sonona, ni wale wanaojihisi kukosa msaada kutoka kwa jamii.
Aidha, alisema watu wasio na kipato cha uhakika, wawe wanajiajiri au wameajiriwa na wale wasioweza kufanya kazi, wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupata sonona.
Pia, alisema watu wenye magonjwa ya muda mrefu, kama vile maambukizo ya virusi vya ukimwi na magonjwa yasiyoambukiza, wanakabiliwa na hatari ya juu zaidi ya kupata sonona.
Dk Sanga pia alisema sonona inaweza kusababishwa na changamoto za kibaolojia, kisaikolojia na kijamii.
“Sababu za kibaolojia ni pamoja na urithi wa sonona, matumizi ya dawa zinazosababisha sonona, magonjwa yanayochochea sonona, na upungufu wa virutubisho kutokana na lishe duni na tabia bwete,” alisema Dk Sanga.
Dk Sanga ambaye ni Waziri Kivuli wa Afya kutoka Chama cha ACT- Wazalendo, anashauri Serikali iweke mfumo imara wa hifadhi ya jamii, ili kuwapa wananchi kinga dhidi ya kuingia katika umaskini na kuwawezesha kupata huduma za afya kulingana na mahitaji yao, badala ya kuzingatia kipato chao kama ilivyo sasa.
Pia alipendekeza kuondoa mianya ya ubadhirifu wa mali ya umma ili kukuza uchumi, kupunguza ukosefu wa ajira na kuhakikisha ustawi wa jamii kwa kupunguza umaskini, ambao ni chanzo kikubwa cha matatizo ya afya ya akili nchini.
“Serikali iweke sera mahsusi ya afya ya akili ili kuboresha na kutoa huduma bora za afya ya akili, pamoja na kufanya marekebisho ya sheria ya afya ya akili ya mwaka 2008,” alisema Dk Sanga.
Alisisitiza pia kuongeza bajeti kwa ajili ya kufadhili tafiti za magonjwa ya akili ili kuimarisha uelewa na mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande mwingine, Dk Sanga alisema kuna umuhimu wa kuboresha huduma za afya ya msingi kama vile zahanati na vituo vya afya, ikiwa ni pamoja na kuongeza wafanyakazi, wataalamu, vifaa tiba, vitendanishi na dawa ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.
Pia alihimiza kujengea uwezo wataalamu wa afya wa ngazi zote katika utoaji wa huduma za afya ya akili na kuelimisha jamii kuhusu njia za kujikinga na kukabiliana na matatizo ya afya ya akili, ikiwemo ugonjwa wa sonona.
Aidha, alipendekeza elimu ya afya ya akili ijumuishwe kwenye mitalaa ya shule za msingi na sekondari, ili kuwasaidia watoto na vijana kupata ujuzi wa kukabiliana na changamoto za maisha.
“Serikali inapaswa pia kuwezesha upatikanaji wa elimu ya afya ya akili kupitia majukwaa ya kidigitali ili kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema.
Alichosema Mganga Mkuu wa Serikali
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alisema kupitia Sera ya Afya ya mwaka 2007, Serikali inaelekeza kuwepo kwa huduma bora za afya ya akili, zilizotajwa kwenye Mkakati wa 5 wa Sekta ya Afya kama huduma za msingi.
Alisema: “Tanzania pia ni miongoni mwa nchi chache zilizo na Sheria ya Afya ya Akili (Mental Health Act 2008) inayolenga kulinda haki na stahiki za wagonjwa wa akili.”
Siku ya afya ya akili duniani huadhimishwa Oktoba 10 kila mwaka. Siku hii ilianzishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la Afya ya Akili Duniani mnamo 1992.
Lengo ni kuboresha ujuzi, kuongeza ufahamu na kuendesha vitendo vinavyokuza na kulinda afya ya akili ya kila mtu kama haki ya msingi ya binadamu ulimwenguni kote.
Ikumbukwe kwamba, afya ya akili ni haki ya msingi kwa watu wote.
Kila mtu, yeyote yule na popote alipo ana haki ya kufikia kiwango cha juu zaidi cha afya ya akili.
Mwaka huu, kauli mbiu ya siku ya afya ya akili imelenga kutukumbusha umuhimu wa ‘afya ya akili kazini.’ Kwamba mazingira salama, yenye afya ya kufanya kazi yanaweza kufanya kama sababu ya ulinzi kwa afya ya akili.
Hali zisizofaa, ikiwa ni pamoja na unyanyapaa, ubaguzi na kufichuliwa kwa hatari kama vile unyanyasaji zinaweza kuathiri afya ya akili.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.