Mfuko wa maji waeleza matumizi tozo ya Sh50 kwenye mafuta

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) hutumia Sh50 zinazokatwa kwenye kila lita ya mafuta kufadhili na kuendeleza miradi ya maji nchini na kwa mwaka hukusanya takriban Sh170 bilioni.

Pamoja na vyanzo vingine vya upatikanaji wa fedha, makusanyo yake yanatumiwa katika miradi kwa asilimia isiyopungua 88, huku asilimia isiyozidi 10 ikielekezwa katika usimamizi, usanifu, ufuatiliaji na tathmini ya miradi. Gharama za uendeshaji wa mfuko wa maji ni asilimia mbili mpaka sasa.

Hayo yamesemwa jana Alhamisi Agosti 31, 2024 na mtendaji mkuu wa mfuko huo, Haji Nandule alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano ulioratibiwa na ofisi ya Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.

Nandule amesema fedha hizo ni kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

“Mfuko huu pia unahakikisha huduma za maji zinafika katika maeneo yenye uhaba mkubwa, hususani vijijini na maeneo yenye changamoto ya miundombinu. Kupitia michango hii, Mfuko wa Taifa wa Maji unasaidia kupunguza uhaba wa maji,” amesema Nandule.

Amesema mpaka sasa miradi 354 kati ya 998 imekamilika, na mifuko hiyo ni ile iliyokopeshwa fedha na mfuko huo kwa kipindi cha miaka mitatu tangu Julai 2021 hadi Juni 2024 na wananchi takribani milioni 5.3 wamenufaika.

Mkurugenzi huyo mtendaji amesema miradi mingine 104 ya uhifadhi na uendeshaji wa vyanzo vya maji imetekelezwa ikijumuisha uhifadhi wa vyanzo vya maji zaidi ya 92 na wamejenga bwawa moja na kuyakarabati saba, wamechimba visima 50 na kurudisha mito mitano iliyopoteza mikondo yake.

Pia amesema katika kuboresha hali ya upatikanaji wa maji nchini, mfuko ulifungua dirisha la mikopo ambalo lina miezi sita na tayari umetoa mikopo ya Sh5.3 bilioni kwa mamlaka za maji ambazo ni pamoja na Tanga, Dar es Salaam na Bunda zilizopokea jumla ya Sh800 milioni.

“Tunatoa fedha na kufuatilia utekelezaji wake kila baada ya miezi mitatu na kunapotokea changamoto, tunaishauri wizara na katibu mkuu ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Nandule.

Amesema katika kukabiliana na changamoto ya ukusanyaji wa madeni, walishashughulikia changamoto hiyo kwa kukatwa moja kwa moja kwa mamlaka husika kupitia kwenye akaunti zao za benki.

Pia, amesema wanaendelea kupambana kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto ya huduma ya maji wanayatambua na kuyapa kipaumbele katika mwaka wa fedha na hilo ndilo lengo la Serikali la kuanzisha mfuko huo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa bodi wa mfuko huo wa maji, Abdallah Mkufunzi akijibu swali la Said Kubenea kuhusu kukopesha makandarasi na kufanikisha miradi kwa wakati, amesema mfuko kwa sasa unapitia baadhi ya kanuni za mikopo na kuziboresha.

 “Tulikutana na changamoto mbalimbali ambazo ilibidi kubadilisha na kuboresha kanuni tulizokuwa nazo, tutawapatia wataalamu wetu waone kama wanaweza kuliingiza kwenye maboresho na inaweza kuwa ni eneo moja la kutoa mikopo,” amesema Mkufunzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Maji, Prosper Buchafwe amesema Mfuko wa Maji unasimamia miradi, “hii haitoshi, wanahitaji pia kuwa na vyanzo vya upatikanaji wa fedha ili kuipunguzia kazi wizara ibaki na kazi ya kuandaa miongozo kwa kuzielekeza taasisi zao ili zitekeleze.

“Katika utekelezaji, Mfuko wa Maji umetekeleza kwa kusimamia miradi ya maji ya mjini na vijijini na sasa hivi tumeanzisha taasisi ya Ruwasa ambayo inafanya kazi vizuri na imepiga hatua kwenye kutatua changamoto za maji vijijini,” amesema Buchafwe.

Amesema Mfuko wa Maji kwa sasa ni chanzo cha uhakika ambacho mamlaka na mabonde ya maji hukopeshwa fedha za kuendeleza na kuanzisha miradi ya maji na hujipatia fedha zinazotokana na tozo za kila mwezi.

Related Posts