Dar es Salaam. Mwanazuoni maarufu nchini, Profesa Issa Shivji amessema ili Tanzania ipate viongozi bora wa kizazi kijacho, si lazima kuunda programu maalumu za kuwaandaa bali kuboresha mfumo wa elimu uliopo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Profesa Shivji amesema mfumo wa elimu wa sasa unazalisha wanafunzi wanaokariri badala ya kuwafikirisha, hali inayojitokeza hata kwa viongozi walioelimika.
Akiwa katika majadiliano ya kitabu cha Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake juzi, msomi huyo aliyewahi kuongoza kamati na tume mbalimbali nchini, aliongeza kuwa mabadiliko ya haraka katika elimu ni muhimu, kwani ndiyo mzizi wa tatizo la ukosefu wa viongozi wenye uwezo wa kujenga hoja zenye mantiki na zinazoeleweka.
Profesa Shivji mbobevu katika masuala ya sheria amesema mageuzi hayo ya mfumo wa elimu yanapaswa kuanza sasa na si kusubiri yaende sambamba na hali ya ustawi wa kisiasa.
Ameeleza hayo alipokuwa anajibu maswali katika majadiliano na mapitio ya kitabu hicho, yaliyoratibiwa na Taasisi ya Uongozi na kuongozwa na Bakari Machumu, mkurugenzi na mwanzilishi wa kampuni ya BSM Washauri.
Sokoine aliyekuwa waziri mkuu wa tatu wa Tanzania. alishika wadhifa huo mara mbili, tangu Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na mara ya pili kuanzia Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea mkoani Morogoro.
Akijibu swali wanapatikanaje viongozi kama Sokoine katika kizazi cha sasa, Profesa Shivji alisema mfumo wa elimu uliopo unawafanya watu wakariri badala ya kuwafikirisha na hilo lipo hadi ngazi ya elimu ya juu.
“Unakuta mtu ana shahada mbili lakini anashindwa kujenga hoja kwa sababu hajapitia mfumo wa elimu unaomfikirisha.
“Utaikuta hiyo pia kwa viongozi wetu, nasikiliza hotuba za viongozi wetu, siku hizi sioni mwanzo, sioni mwisho. Huwezi ukajua anachotaka kusema ni nini,” alisema na mzizi wa yote hayo ni mfumo wa elimu.
Sokoine na vita vya uchumi
Akiichambua sura ya 12 ya kitabu hicho inayoeleza vita vya uhujumu uchumi, msomi huyo alisema watu wengi wanafikiria vita hivyo vilikuwa ni kwa sababu ya hali ya uchumi, badala yake vililenga kurudisha mamlaka ya Serikali.
“Kipindi cha mwisho cha Mwalimu kilikuwa kigumu sana kiuchumi, bei zilifumuka, bidhaa hewa na wajanja walikuwa wengi.
“Walanguzi walijitajirisha wakati huo na hali ya uchumi ilikuwa mbaya kiasi kwamba zahama za kiuchumi ziligeuka kuwa za kisiasa na hata umaarufu wa Mwalimu ulianza kushuka,” alisema.
Katika kipindi hicho, alisema kwa mara ya kwanza tangu uhuru wa Tanganyika, jaribio la kuipindua Serikali lilikaribia kufanikiwa kwa sababu ya mazingira.
Alisema katika mazingira hayo, pasi za kusafiria ziliuzwa mtaani kama njugu.
“Shida iliyotokea hakukuwa na mpangilio, maandalizi wala ushirikishwaji wa wananchi, vilitokea ghafla na vyombo vya mabavu hasa polisi vilikuwa na uonevu mkubwa na utesaji wa watu na wengine waliwekwa ndani,” alisema.
Alisema unapokipa madaraka makubwa chombo cha mabavu, tarajia kitayatumia kujitajirisha na kukwapua mali za watu.
“Hili ina funzo kubwa, hata ukiwa na nia nzuri, ukikiuka haki, taratibu na kutumia mabavu, haikufikishi mbali,” alisema.
Akifafanua, alisema matumizi ya mabavu yanaotesha mbegu ya ubepari, badala yake jambo muhimu ni kuheshimu haki na utu wa binadamu, vinginevyo chombo cha mabavu kinaweza kuwa adui wa wananchi.
Alisema kila raia ana utu ndani yake na utu wa tajiri na masikini hautofautiani, hivyo unapaswa uheshimike usidhalilishwe.
“Watu wanakamatwa, kabla ya kuulizwa kwanza wanachapwa na nafikiri hata mahakama zetu zingebadili utaratibu, kwamba mtuhumiwa anayekubali kosa kwa kupigwa sana, isimpokee na kutumia maneno yake kama ushahidi,” alisema.
Profesa huyo alieleza furaha yake katika maisha ya Sokoine pale alipoenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuuliza iwapo mijadala ya wasomi inaendelea.
“Alitwambia vipi mijadala yenu mmepooza siku hizi, hamjadili na hii ilinishawishi sana, kwa sababu ukiacha Mwalimu Nyerere, ilikuwa nadra kwa kiongozi yeyote kuja chuoni kujua kinachoendelea,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Shivji, hotuba za Sokoine zilikuwa na mantiki na ziligusa uhalisia wa maisha ya watu, alizisifu kwa mpangilio wa hoja, hasa ile aliyoitoa katika Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 1982.
Msomi huyo alisema ipo nguvu ya malezi, makuzi na utamaduni ndani ya uongozi bora aliokuwanao Sokoine.
“Labda kutokana na jamii yake inavyopanga maneno yanakuwa na mantiki na hiyo utaikuta kwenye hotuba zake,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu siri ya uimara wake yeye binafsi, licha ya umri mkubwa alionao, Profesa Shivji alijibu ni kusoma vitabu, kufanya mazoezi na kula kwa kiasi.
“Raha ya kusoma kitabu ni kupapasa kurasa hadi kusara na ndilo jambo lililonifunza na naendeleza tabia hiyo pamoja na uwepo wa simu siku hizi,” alisema.
Awali, akifungua majadiliano hayo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Taasisi ya Uongozi, Deogratius Usangira, alisema hayo ni majadiliano ya 16 yenye lengo ni kutimiza majukumu ya taasisi hiyo ya kuongeza uelewa na maarifa kwa viongozi wa sasa na wanaochipukia.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.