Prof. Kitila aeleza mafanikio ya uwekezaji wa DP World na mradi wa SGR

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais -Mipango na Maendeleo, Prof. Kitila Mkumbo, leo tarehe 01 Novemba 2024 amewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26 ambapo ameeleza mafanikio kumi yaliyopatikana kufuatia uamuzi wa serikali wa kuikabidhi Kampuni ya DP World kuendesha sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mafanikio hayo kumi yaliyoelezwa na Prof. Kitila ni:

i) Kampuni ya DPW imeshawekeza TZS 214.425 bilioni (sawa na 31% ya TZS bilioni 675 zinazopaswa kuwekezwa katika kipindi cha miaka mitano) kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa; ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA; na usanifu na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa Bandari;
ii) Kampuni imenunua na kufunga vitendea kazi vya kisasa (SSG na RTG) katika kupakia na kushusha mizigo. Kufuatia hatua hii, muda wa kuhudumia meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba (7) hadi wastani wa siku tatu (3). Hatua hii imewezesha kupunguza idadi ya meli zinazosubiri angani kutoka wastani wa meli 35 mwezi Septemba 2023 hadi wastani wa meli 15 mwezi Septemba 2024.
iii) Kuongezeka kwa shehena zinazohudumiwa kutoka shehena 141,889 mwezi Mei 2024 hadi kufikia shehena 168,336 mwezi Septemba 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.6 katika kipindi cha miezi mitano
iv) Kuongezeka kwa idadi ya makasha yanayohudumiwa (Twenty-Feet Equivalent Units-TEUs) katika Bandari ya Dar es Salaam (Gati 0-7) kutoka wastani wa makasha 12,000 kwa mwezi hadi kufikia makasha 27,000 kwa mwezi Septemba 2024. Idadi hii ya makasha ilikuwa haijawahi kufikiwa katika historia ya Bandari ya Dar es Salaam. Kiwango cha juu kabisa kabla ya hii ilikuwa ni makasha 15,000.
v) Katika kipindi cha miezi mitano gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1 kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa bandari kwa kampuni
vi) Katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam Serikali imeshakusanya jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrahaba (royalty), na Ardhia (warfage)
vii) Kutokana na kuongezeka kwa mapato na kupungua kwa gharama za uendeshaji kufuatia maboresho yaliyofanyika, serikali, kupitia TPA, imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya TZS 1.922 trilioni (USD 686.628 milioni) kwa kutumia makusanyanyo yanayopatikana. Miradi hii ni Ujenzi wa Kituo cha Kupokwa Mafuta (SRT); Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao (Mtwara); na Ujenzi wa Gati za Majahazi (Dhow Wharf) Dar es Salaam.
viii) Kuunganishwa kwa mifumo ya forodha (Tanzania Customs Integrated System – TANCIS) na ile ya bandari (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS). Hii imewezesha kupunguzwa/kuondolewa kwa mifumo iliyokuwa inafanana na hivyo kupunguza muda wa kuondoa mizigo bandarini, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano.
ix) Mapato ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka hadi kufikia TZS Trilioni Moja mwezi Septemba 2024 ukilinganisha na wastani wa TZS 850 bilioni kwa mwezi. Hii imetokana na TRA kuweza kuchakata mizigo mingi zaidi ndani ya muda mfupi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Mipango na Maendeleo, Prof. Kitila Mkumbo

Aidha, Prof. Mkumbo ameeleza mafanikio tisa ya kiuchumi na kijamii yanayotokana na kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Mafanikio haya ni:

i) Hadi sasa mradi umeshazalisha ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,000 zisizo za moja kwa moja. Ajira hizi zimetengeneza pato la TZS bilioni 358.74.
ii) Mradi umetoa fursa kwa viwanda, wazabuni na wakandarasi ambapo hadi sasa jumla ya kampuni 2,460 zinashiriki katika mradi huu na kandarasi zenye thamani ya TZS 3.69 trilioni zimetolewa tangu mradi uanze
iii) Mradi umechochea kuongezeka kwa mahitaji ya saruji, nondo, na vifaa vingine vya ujenzi na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi
iv) Kupungua kwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka wastani wa masaa kumi kwa basi hadi masaa matatu na nusu kwa Treni
v) Kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watu
vi) Kutunza mazingira/kupungua kwa uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kuwa usafiri wa treni unatumia nishati ya umeme na kwa kuwa safari za mabasi zimepungua
vii) Kuzalisha kipato ambapo hadi kufikia Septemba 2024 jumla abiria 645,421 walisafirishwa na kiasi cha TZS 15.695 bilioni kupatikana
viii) Kuchochea shughuli za utalii katika ukanda ambao reli inayopita, hususan Hifadhi ya Mikumi na Hifadhi ya Ruaha (kupitia Stesheni ya Kilosa)
ix) Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuchochea mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kupunguza muda wa safari na gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria na hivyo kuchochea ukuaji wa biashara za ndani na kimataifa. Hadi Septemba 2024 jumla ya miradi 519 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika ushoroba wa reli yenye kuvutia mtaji wa Dola za Marekani 4.59 bilioni na kutarajia kuzalisha ajira 115,566. Miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji huku baadhi yake ikiwa imeshakamilika na kuanza uzalishaji.

About The Author

Related Posts