Katika urushaji wa matangazo ya kidigitali, wajasiriamali wa Marekani, Adam Curry na John Dvorak, kuanzia Oktoba 16, 2007, walianzisha programu ya vichekesho vyenye kujadili hali halisi ya kisiasa, inayoitwa No Agenda.
Curry na Dvorak kama lilivyo jina la programu, wao huwa hawana agenda ya kuzungumzia isipokuwa huendesha mijadala kutokana na upepo wa kisiasa unavyokuwa ndani ya wakati husika.
Kwamba Curry na Dvorak wanapotoka kwenye kipindi kimoja, huwa hawajui nini watajadili au mazungumzo gani wataendesha kwa njia ya ucheshi (comedy) katika programu inayofuata. Upepo wa kisiasa kwa namna vyombo vya habari vinavyoripoti, ndivyo huamua nini wakifanye.
Tanzania ya sasa, ipo kama programu ya No Agenda. Kwamba kama nchi hakuna agenda ambazo taifa linazishika na kupanga kufika nazo mwisho. Ni upepo tu, ukivuma kushoto ndiko hukohuko fikra zote zinaelekea. Upepo ukivuma kulia kila mtu anafikiria kulia.
Ukiwa upepo ni wa Kaskazini, mijadala yote ni Kaskazi, wanaopinga Kaskazi na wenye kutetea mchuano unakuwa mkali. Siku upepo ukiwa wa Kusini, habari zinakuwa za Kusi, mijadala ya kutetea au kuushambulia upepo wa Kusi.
Katika hili la nchi kutoishi kwenye agenda yenye kusimamiwa mpaka mwisho kisha matokeo yaonekane, makosa yanaanzishwa na Serikali, vyama vya siasa hasa vya upinzani vinacheza mdundo wa Serikali mwisho kabisa wananchi wanageuka wafuata mkumbo.
Taifa ambalo watu wake wanajadili mambo yake kwa kufuata mkumbo (band wagon), maana yake halina agenda. Na mijadala ya agenda ndiyo hutafsiri ya nchi na wananchi. Kama nchi haina agenda maana yake haieleweki uelekeo wake.
Sasa basi, tatizo la nchi kutokuwa na agenda linaanzia kwenye masuala ya maendeleo mpaka matukio yanayojiri. Vyama vya upinzani vinakosa agenda, vinapumua kwa udhaifu au makosa ya Serikali.
Kwa mwendo huohuo, Serikali nayo inafanya makosa mengi, kwa hiyo vyama vya upinzani vinajikuta vinahamia kosa la pili la Serikali kabla ya lile la kwanza halijapatiwa ufumbuzi. Mwisho kabisa, unaona kwamba hakuna mahali ambapo Serikali ilibanwa sawasawa na wapinzani mpaka mwisho.
Wakati mwingine unaona kabisa kuwa Serikali inawageuza wanasiasa inavyotaka yenyewe, kwa makosa yake au kupatia kwake. Wanasiasa nao wanacheza mdundo huohuo. Wanavurugwa na wanavurugika, matokeo yake Serikali inabaki yenye afya ndani ya vipindi visivyo na matumaini.
Septemba 2024, agenda za nchi, zote, zilimzunguka mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao, na kifo chake cha kuuawa kikatili. Oktoba inakwenda ukingoni, hakuna mjadala tena wa kibao.
Agosti 2024, agenda ilikuwa kutekwa au kunyakuliwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili. Habari ya soka ilifunikwa na Kibao. Sasa, nchi haina presha kuhusu Kibao wala Soka.
Desemba 2016, nchi ilitekwa na kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe. Ben alitoweka katika mazingira yenye kuacha viulizo vingi tangu Novemba, 2016.
Kufikia Januari 2017, habari za Ben zilififia kabisa. Tangu Desemba 2016, tukio la Ben lilihusishwa na vitendo vya utekaji, vyombo vya usalama vilizungumzwa katika nadharia mojawapo ya kupotea kwa Ben.
Kufikia Februari 2017, Taifa likatekwa na habari za biashara ya dawa za kulevya, baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuanzisha mapambano.
Kitendo cha Makonda kuanzisha mapambano ya dawa za kulevya, kilibadili upepo. Habari za Ben zilifukiwa. Akina sisi ambao tuliandika mwendelezo wa makala za kuhoji kuhusu Ben, tulionekana tunatoka nje ya mdundo wa wakati husika ambao ni dawa za kulevya.
Wakati agenda ikiwa ya dawa za kulevya, mara ikaibuka hoja ya kuwa Makonda anatumia vyeti vya kughushi, kwani jina lake halisi ni Daudi Bashite, kwamba alipata daraja sifuri kwenye mtihani wa kidato cha nne kisha akanunua cheti cha mtu anayeitwa Paul Christian Malanja.
Masuala ya dawa za kulevya na Makonda yakaishia hapo. Kipindi cha mchakato wa vita ya dawa za kulevya kama ambavyo Makonda alikuwa akitekeleza, makosa mengi yalikuwa yakifanyika lakini watu walisahau kila kitu, hoja ikawa vyeti.
Mambo yote kuhusu vyeti yanyamazishwa na tukio la Makonda kudaiwa kuvamia kituo cha matangazo cha Clouds TV na kulazimisha kipindi chenye maudhui ya kumshusha hadhi, Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kirushwe hewani.
Gwajima alikuwa mmoja wa watu ambao waliamua kuvalia njuga suala la vyeti vya kugushi ambalo linamwandama Makonda. Hivyo tafsiri ya Makonda kulazimisha kipindi hicho kirushwe na Clouds TV, ni kwamba alilenga kulipa kisasi.
Nchi ikasimama kwa suala la Clouds TV kuvamiwa na Makonda. Agenda zote za zamani zikanyamazishwa na tukio hilo. Agenda ikawa shinikizo kwamba ama Makonda ajiuzulu au Rais John Magufuli amfute kazi kwa makosa aliyofanya.
Kauli ya Rais Magufuli kuwa hapangiwi cha kufanya ambayo aliitoa siku mbili baada ya Makonda kudaiwa kuvamia Clouds TV, ikageuza agenda. Rais Magufuli hapangwi cha kufanya na wakosoaji wa kauli hiyo.
Siku mbili baadaye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alipokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tuhuma hizo za Makonda kuvamia Clouds TV. Ripoti ilisomwa kisha akaahidi kuiwasilisha kwa viongozi wa juu, kwa maana ya Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais.
Rais Magufuli hakungoja hata aipokee ripoti hiyo, kwani alimfuta kazi Nape kisha akamteua Dk Harrison Mwakyembe kushika nafasi yake. Upepo ukahamia kwa uamuzi wa Rais ambao haukudumu.
Tukio la mtu ambaye anadaiwa ni ofisa wa usalama wa taifa kumtolea bastola Nape na kumtishia, alipokuwa anataka kuzungumza na waandishi wa habari, Oysterbay, Dar es Salaam, lilimeza mjadala wa Rais Magufuli na uamuzi wake kumtengua Nape.
Suala la Nape kutenguliwa likafunikwa na tukio la mwanamuziki wa Rap, Emmanuel Elibariki ‘Nay Wamitego’, kukamatwa kwa tuhuma za wimbo wake unaoitwa Wapo kuwa na maudhui mabaya kwa Serikali na viongozi wake.
Likafuata tukio la Rapa mwingine, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ akiwa na wenzake watatu, jumla wanne, kuvamiwa na kupelekwa kusikojulikana. Mambo yote yakaisha, suala la utekaji likapata nguvu.
Mwendo huu hauna afya kwa usalama wa nchi. Tanzania ya sasa inaonekana ni ya “watasema mchana usiku watalala”. Ndiyo Kibao na Soka siyo agenda tena, kama ambavyo Ben na mwandishi Azory Gwanda, wapotea, zikapazwa sauti, kisha ikawa kimya. Ni taifa la No Agenda.