Kitendawili cha sakata la Gachagua na mrithi wake

Baada ya Baraza la Seneti kumwondoa madarakani Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, Oktoba 17, 2024, swali kubwa linabaki kuwa je, huo ndio mwisho wake? Au ana majaliwa mengine katika safari yake kisiasa?

Tayari Rais Rais William Ruto ameshamteua Waziri wa Mambo ya Ndani, Profesa Kithure Kindiki kuwa naibu wake mpya, siku moja baada ya kuondolewa kwa Gachagua suala ambalo hata hivyo limebaki kitendawili.

Baada ya uteuzi huo kinachosubiriwa ni kuapishwa, lakini tayari upande wa Gachagua umefungua kesi katika kesi ya Mahakama ya Kerugoya ukidai kuwa uteuzi huo haukufuata utaratibu.

Gachagua alikuwa anakabiliwa na mashtaka 11, ikiwa ni pamoja na utovu wa nidhamu, kudhoofisha uhuru wa mahakama, na uvunjaji wa Sheria ya Uadilifu wa Kitaifa. Seneti ilipitisha mashtaka matano kati ya hayo, jambo lililosababisha kung’olewa kwake madarakani.

Hata hivyo, Gachagua, ambaye alikana mashtaka hayo siku moja kabla, hakuweza kuhudhuria kikao cha mwisho cha Seneti kutokana na kulazwa hospitalini, wakili wake akieleza kuwa alikuwa na maumivu makali ya kifua.

Licha ya kutokuwepo kwake, kesi iliendelea na hoja za kuahirisha kikao zilikataliwa na wajumbe wa seneti. Timu yake ya kisheria ilitoka nje kwa kupinga, lakini hatimaye mchakato wa kumwondoa ulihitimishwa kabla ya saa sita usiku.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kenya kwa naibu rais kuondolewa madarakani.

Maseneta walikataa kuahirisha kesi ya kumwondoa Gachagua madarakani, licha ya kuwa kisheria walikuwa na muda hadi Jumamosi, jambo lililoonyesha nia yao thabiti ya kumwengua.

Kuondolewa kwa Gachagua kunaelezwa kuwa kunatokana na kutofautiana na Rais William Ruto kwa takribani mwaka mmoja uliopita, hata hivyo kiongozi huyo wa nchi hajawahi kusema lolote juu ya jambo hilo.

Kabla ya kesi yake kufikishwa kwenye Seneti, wabunge wengi katika Bunge la Kitaifa nao walipiga kura ya kumwondoa.

Gachagua ambaye pamoja na kuwa mwanasiasa ni mfanyabiashara mashuhuri kutoka eneo lenye kura nyingi la Mlima Kenya, anaielezea hatua hiyo kuwa ni ukatili wa Rais Ruto.

Akizungumzia sakata hilo, mwandishi wa runinga ya NTV, Duncan Khaemba anasema huenda huo ndio ukawa mwisho wa Gachagua hata kama atashinda kesi alizofungua mahakamani.

“Ikiwa Mahakama ya Kerugoya itaruhusu Profesa Kindiki aapishwe maana yake ndio hawezi tena kutolewa, hata kama Gachagua atashinda kesi ya kupingwa kuondolewa.

“Ni sawa na mti uliokatwa, unaweza kuurudishia?” anahoji.

Mbaya zaidi, amesema hata kama Gachagua atashinda kesi yake, bado kutakuwa na ugumu wa kufanya kazi na Ruto, kwani kwa sasa hawaelewani tena.

Anasema tangu awali, Mahakama ilisema haitaingilia mchakato wa Bunge la Seneti kumjadili Gachagua.

Khaemba anasema kwa sasa nchi hiyo inapita kipindi kigumu, hivyo Rais Ruto anahitaji kuwa na msaidizi haraka, kwani lolote linaloweza kumtokea ni lazima awepo mtu wa kukaimu nafasi yake.

Anasema kwa sasa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inahitaji kuziba nafasi tatu za makamishina akiwamo aliyekuwa mwenyekiti, Wafula Chebukati, Abdi Guliye na Boya Molu ambao muda wao ulikwisha mwaka 2023.

“Ukosefu wa makamishna kwenye Tume ya Uchaguzi unaiweka nchi katika hali tete na hata sasa kuna chaguzi tatu zimeshindwa kufanyika na kuna majimbo yalitakiwa kugawanywa, yameshindikana.

“Sasa pamoja na hilo ikitokea nafasi ya Naibu Rais nayo inabaki wazi itakuwa hali mbaya zaidi,” anasema.

Akizungumza kupitia mtandao wa Aljazeera, mchambuzi wa siasa, Herman Manyora amesema muungano wa Kenya Kwanza Alliance, unacheza siasa.

Amefafanua kwamba, hali ilifikia hatua ambapo Rais Ruto ameona hawezi kufanya kazi na naibu wake, hivyo naibu wake lazima aondoke.

“Mtu angeweza kutumaini kwamba rais angemvumilia naibu wake hata kama wanakosea, lakini kasi ambayo wanatumia kumwondoa, dhamira yao ya kumwondoa, na hali ya kisasi inayoonekana inashangaza,” amesema.

“Inakuwaje, baada ya kuahidi kwa maneno wazi kwamba hutamwondoa, sasa unageuka na kufanya hivyo? Lakini hawa ni wanasiasa. Wanasema jambo moja na kufanya jingine.”

Kwa upande mwingine, baadhi ya wafuasi wa Gachagua wa ngome yake ya Mlima Kenya wametoa wito wa kuondolewa pia kwa Rais Ruto

Akizungumza na Aljazeera, Erick Mwaura anayeishi Kilifi, amesema walimpigia kura pamoja na naibu wake, na ikiwa naibu rais ametenda makosa yanayosababisha kuondolewa kwake, basi Rais pia anapaswa kuondolewa kwa makosa hayo hayo.

“Kumwondoa Gachagua ni hatua nzuri lakini je, wanaweza sasa kuendeleza hatua hiyo kwa Rais na maafisa wengine wote waliochaguliwa? Wafanye uchunguzi kuhusu uteuzi mkuu wa rais wa watu kutoka jamii yake pekee, wachunguze uteuzi wa kamati za Hazina za Maendeleo ya Maeneo Bunge (Mfuko wa jimbo) uliofanywa na wabunge. Kinachofaa kwa mmoja kinapaswa kufaa kwa mwingine,” alisema,

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 20, 2024 baada ya kutoka hospitali ya Karen jijini Nairobi, Gachagua ameeleza kutoamini kilichotokea kwa mtu aliyemwamini kama Ruto.

Gachagua alifikishwa hospitalini hapo, Alhamisi Oktoba 16, 2024 baada ya kujisikia maumivu ya kifua.

Wakati akifikishwa hospitalini hapo, mchakato wa kumwondoa ulikuwa ukiendelea kwenye Bunge la Seneti.

“Kwa bahati mbaya, nilipokuwa hapa hospitali, kaka yangu na rafiki yangu Ruto aliagiza kuondolewa kwa ulinzi wangu, nilikuwa hapa bila ofisa yeyote anayeniangalia.

“Aliagiza kuondolewa kwa ulinzi nyumbani kwangu kijijini Nyeri na watu waliokuwa karibu yangu waliondolewa na wakaonywa wasiwe karibu na mimi. Sikuwahi kufikiri kwamba Ruto anaweza kuwa namna hiyo,” anasema Gachagua.

Anaendelea, “Mtu niliyemwamini kama Rais, mtu niliyemwamini kama kiongozi, mtu aliyekuwa ameshitakiwa tukamtetea, anaweza kuwa mkatili kiasi hicho, wakati napigania maisha yangu hospitalini? Ni ukatili gani alionao?”

Kwa mujibu wa Gachagua, yeye bado ni Naibu Rais kwani kuna kesi mbili zilizofunguliwa, ikiwemo ya kupinga kuapishwa kwa Profesa Kindiki kurithi nafasi yake na ile ya kupinga mchakato wa kumwengua.

“Rais kwa kupuuza amri ya mahakama na kwa ukatili, ameondoa ulinzi na kuondoa wafanyakazi ofisini kwangu, ameagiza kupitia Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Kosgei kwamba maofisa wote katika ofisi yangu waende likizo ya lazima.

“Jana usiku, magari yote yaliamriwa kuondoka ofisini kwangu. Nashindwa kuelewa ukatili wote huu kwa mtu aliyekuwa naibu wako na aliyekuwezesha kuwa Rais.

“Ni vigumu kuelewa katika hali hii, mtu anapigania uhai wake hospitalini, wewe unamfanyia ukatili. Rais Ruto ninayemwona sio yule niliyemfahamu,” ameeleza Gachagua.

Gachagua amesema usalama wake uko mikononi kwa Ruto aliyemwondolea ulinzi.

“Wakenya wajue kwamba leo narudi nyumbani bila ulinzi wowote na ni vizuri wajue kwamba, chochote kitakachonitokea au familia yangu, Rais Ruto anahusika.”

Akieleza jinsi alivyomwamini Ruto, Gachagua amewataka wanasiasa wa nchi hiyo akiwamo Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Alfred Mutua, akisema walimwekea sharti Rais Ruto la kusaini makubaliano kabla ya kushirikiana katika uchaguzi, isipokuwa yeye tu aliyemwamini bila masharti.

“Ni kwa sababu sisi ni Wakristo tunakwenda kanisani pamoja na kama Mkristo naamini Wakristo wengine hawawezi kunisaliti.

“Mwaka mmoja uliopita ulikuwa mgumu sana, mwaka wa kukimbizana na changamoto. Kilichotokea Alhamisi ni kilele cha mateso ya mwaka huu,” amesema.

Ameyafanisha mateso anayopitia kama yaliyomtokea aliyewahi kuwa Makamu wa Rais, Kenneth Matiba kwa Rais Daniel Arap Moi.

“Rais Ruto anataka kunipeleka kwenye njia ambayo Rais Daniel Arap Moi alimpitisha Kenneth Matiba. Alimsababishia Matiba kupata kiharusi na mwisho akafa.

“Sasa Ruto anataka kunitesa, ananifanya kama mnyama nadhani anataka kunipitisha njia ya Matiba, lakini nashukuru kwa rehema za Mwenyezi Mungu ananilinda. Watu wanapiga simu kuuliza kama ni amekufa au bado iko hai, wengine wanasherehekea.

“Ni jambo la ajabu sana kutokea katika nchi hii, kwamba unaweza kumkatili mtu aliyekuwezesha kuwa rais?”

Akifafanua zaidi, Gachagua anasema kosa lake ni kumwambua ukweli Ruto.

“Kosa la mtu huyo ni kukwambia ni ukweli, kwamba usiwahamishe watu bila utaratibu, usiwapige watu, unawaua na unaua biashara zao. Usilazimishe mpango wa nyumba kwa watu, kama hawataki hizo nyumba usiwalazimishe.”

Amesema sababu pia ni mabadiliko ya Katiba nchi hiyo yaliyomfanya Naibu Rais kuteuliwa na Rais na hivyo kukosa nguvu ya uamuzi.

“Sasa matokeo yake ateuliwe mtu ambaye hawezi kuuliza maswali wala kusema chochote?”

Gachagua anakuwa naibu rais wa kwanza kuondolewa ofisini kwa njia hii tangu hatua ya kumwondoa madarakani ilipoanzishwa kwenye Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.

Kwa mujibu wa katiba hiyo, kuondolewa madarakani ni hatua ya moja kwa moja ikiwa imeidhinishwa na mabaraza yote mawili.

Wajumbe 282 wa Bunge la Kitaifa walipiga kura kwa wingi kuunga mkono hatua ya kumwondoa Gachagua madarakani. Katika Seneti, theluthi mbili ya maseneta 67 pia waliidhinisha hoja ya kumwondoa.

Hata hivyo, Gachagua anaweza kupinga hatua hiyo mahakamani – jambo ambalo ameshalifanya.

Kulingana na sheria za Kenya, rais ana siku 14 kuteua mtu mpya kwa nafasi ya naibu rais, kisha Bunge la Kitaifa litakuwa na siku 60 kujadili kuhusu mteule huyo. Tayari uteuzi umeshafanyika ndani ya siku moja tu.

Mwanasheria Charles Kanjama amesema mchakato huo wa haraka unashawishi kuwa ni “hatua iliyopangwa kimakusudi.”

“Ikifika mwisho wa siku ya Ijumaa, huenda hata Seneti watakuwa wameidhinisha mteule wa rais,” alieleza. “Hii ina maana kuwa mchakato ambao kisheria unapaswa kuchukua siku 74 utachukua saa 24 pekee,” Kanjama ameiambia Aljazeera.

Related Posts