Taarifa ya WAFA inasema mashambulizi hayo yametokea katika mji wa Deir Al-Balah, eneo ambalo linafahamika kuwa ni kambi Nuseirat na mji mwingine wa Al-Zawayda. Jeshi la Israel limesema vikosi vyake viliweza kuwabaini na kuwaangamiza wapiganaji kadhaa wenye silaha katikati ya mji wa Gaza katika operesheni mahususi kwa ajili ya eneo la kaskazini la Jabalia.
Maafisa wa afya katika eneo hilo lililozingirwa wanasema takriban Wapalestina 46 wameuawa kwa mashambulizi ya anga ya Israel, ikiwa idadi kubwa upande wa kaskazini ambapo shambulizi liliilenga hospitali, kuharibu vifaa vya hospitali hiyo na kuvuruga taratibu za matibabu.
Jeshi la Israel linasema Hamas inatumia hospitali kijeshi
Jeshi la Israel limeshutumu kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas ya kutumia Hospitali ya Kamal Adwan huko Beit Lahiya kwa malengo ya kijeshi na kusema idadi kadhaa ya wapiganaji hao wamekuwa kujificha huko, ingawa Maafisa wa afya na Hamas wanakanusha madai hayo. Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza imetoa wito mashirika ya kimataifa “kulinda hospitali na wafanyakazi wa sekta ya afya kwa kile walichokiita ukatili wa uvamizi wa Israeli.
Katika uperesheni nyingine huko Lebanon, Jeshi la Israel mapema leo limeripotiwa kufanya mashambulizi ya nguvu ya anga katika maeneo ya vitongoji vya kusini mwa mji wa Beirut, ikiwa ni kipindi kifupi baada ya kuwaarisha wakazi kuondoka katika maeneo hayo, ikiwa ni shambulizi la kwanza la aina hiyo lenye kuyalenga maeneo yenye idadi kubwa ya watu.
Blinken na matumani ya amani ya Lebanon
Jana Alhamis, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema Israel na Lebanon wapo katika uelekeo wa maelewano ya juu ya nini knahitajika kwa ajili ya kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa lililokiukwa kwa muda mrefu hatua ambayo ni msingi wa kumaliza mzozo uliopo. Lakini muda unakwenda kwa kasi katika kufikia makubaliano kabla ya uchaguzi wa Marekani, uliopangwa Novemba 5.
Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon mzozo wa taifa hilo ambao umedumu kwa majuma matano sasa umesababisha vifo takriban 2,800.
Soma zaidi: Matumaini ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah
Vita vya Gaza ambavyo vilianza baada ya wanamgambo wanaoongozwa na Hamas kuishambulia Israel Oktoba 7, 2023, na kuua watu wapatao 1,200 na kuchukua amateka Waisrael 251, mashambulizi ya Israel ya baadae yanakadiriwa kuwaua watu 43,000 na majengo mengi kugeuzwa vifusi.
Vyanzo: RTR