MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, kesho Jumamosi watakuwa mwenyeji wa Azam katika mwendelezo wa ligi hiyo mchezo ukipigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku kila mmoja akitambia ubora wa timu yake.
Katika mchezo huo wa Dar es Salaam Dabi utakaoanza saa 12:00 jioni, Yanga itaingia uwanjani ikiwa ni timu pekee ndani ya ligi hiyo msimu huu ambayo haijapoteza mchezo mpaka sasa huku ikiwa kileleni na pointi zake 24.
Mbali na hilo, Yanga ndiyo timu pekee isiyoruhusu nyavu zake kutikiswa katika ligi hiyo baada ya kushuka dimbani mara nane na kushinda mechi zote ikifunga mabao 13.
Azam iliyopoteza fainali mbili mfululizo mbele ya Yanga ikianzia Kombe la FA Juni 2, mwaka huu kule Zanzibar kisha Ngao ya Jamii Agosti 11, mwaka huu, kesho ina nafasi nyingine ya kujiuliza.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akizungumzia timu yake amesema kikosi chake kipo tayari kukutana na Azam baada ya kurejea kutoka Zanzibar walipoifuata Singida Black Stars na kushinda bao 1-0.
Gamondi amesema wanatarajia mchezo mzuri na mgumu dhidi ya Azam akienda kukutana na timu ambayo inafundishwa na kocha wanayefahamiana vizuri.
“Tumesafiri na kurudi hapa (Dar es Salaam), tumefanya maandalizi ya kurudisha utulivu wa mwili, tupo tayari kucheza mechi nyingine ngumu.
“Siku zote tumekuwa na nidhamu ya kuwaheshimu wapinzani wetu, tunakwenda kukutana na Azam ambayo ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri na kocha mzuri ambaye nilifanya naye kazi miaka 25 iliyopita.
“Itakuwa mechi yenye ushindani, nadhani timu mbili bora zitashindana katikati ya uwanja, itakayokuwa vizuri kushinda nyingine itashinda, sisi tunataka kushinda ili tuendelee kulinda ubora wetu na kuweka hai malengo yetu,” amesema Gamondi.
Naye Kocha wa Azam, Rachid Taoussi, amesema timu yake inakwenda kucheza mchezo mkubwa lakini kikosi chake ni miongoni mwa timu bora Tanzania inayoundwa na wachezaji wa kimataifa.
Taoussi amesema Azam itakwenda kucheza mchezo huo ikitumia falsafa yake ambapo tayari wanajua uimara na mapungufu ya Yanga ambayo pia ina wachezaji na kocha bora.
“Hii ni mechi ngumu lakini Azam timu kubwa pia hapa Tanzania, ina wachezaji wakubwa saba mpaka nane wanaocheza timu za Taifa kwa hiyo tunakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Yanga,” amesema Taoussi na kuongeza.
“Tutakwenda kucheza kwa kutumia falsafa yetu, nina miezi miwili sasa hapa Tanzania nawajua wachezaji wa timu pinzani lakini pia tumewafanyia tathimini wapinzani wetu wana timu nzuri yenye wachezaji wazuri na kocha mzuri.
“Mimi na kocha wa Yanga (Gamondi) tunafahamiana sana, tumewahi kufanya kazi pamoja Wydad miaka ya nyuma, lakini sisi ni wataalam tutapambana uwanjani na kusahau urafiki wetu kwa dakika 90.”