Gaborone. Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi amekubali kushindwa kwenye uchaguzi wa Oktoba 30, 2024 baada ya matokeo ya awali kuonyesha kuwa chama chake cha Botswana Democratic Party (BDP) kimepoteza wingi wa wabunge, ikiwa ni takriban miongo sita kikiwa madarakani.
Kukubaliwa kwa Masisi kushindwa leo Ijumaa Novemba mosi, 2024 kumekuja kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa rasmi, lakini chama hicho cha BDP kikiwa kwenye nafasi ya nne, kwa mujibu wa hesabu za Tume ya Uchaguzi.
Rais Masisi ambaye alikuwa akitafuta muhula wa pili wa miaka mitano katika uchaguzi uliofanyika Jumatano iliyopita, amesema ataondoka madarakani.
“Ningependa kuwapongeza wapinzani kwa ushindi wao na nakubali matokeo,” Masisi aliuambia mkutano wa waandishi wa habari jijini Gaborone.
“Ingawa nilitaka kuendelea kuwa Rais wenu, naheshimu matakwa ya wananchi na nampongeza Rais mteule. Nitajiondoa na nitaunga mkono Serikali mpya,” ameongeza.
Matokeo hayo yanatarajiwa kuthibitishwa na Tume ya Uchaguzi baadaye leo, lakini hesabu za awali zinaonyesha kuwa vyama vitatu vya upinzani kwa pamoja vimepata viti 31 kati ya 61 katika Bunge hilo.
Chini ya mfumo wa uchaguzi wa nchi hiyo, chama cha kwanza kikifikisha viti 31 kitatangazwa mshindi, kusimamisha mgombea Rais na kuunda Serikali.
BDP imetawala Taifa hilo lenye utajiri wa almasi Kusini mwa Afrika tangu mwaka 1966.
Chama kikuu cha upinzani cha Umbrella for Democratic Change (UDC) kimeongoza kwa kiasi kikubwa katika matokeo hayo na kumfanya kiongozi wake, Duma Boko kuwa mgombea urais.
Masisi amesema amempigia simu Boko kumjulisha kuwa anakubali kushindwa kwenye uchaguzi huo.
UDC tayari ilikuwa imepata viti zaidi ya 24, na ofisa wa chama, Mike Keakopa ameliambia shirika la habari la AFP kuwa na alikuwa na lengo la kufikia viti 31 ili kuwa mshindi wa moja kwa moja.
Hadi leo asubuhi, Boko alikuwa hajazungumzia hadharani ushindi wa chama chake tangu matokeo hayo ya awali kutangazwa.
Kwenye kampeni zake alikuwa anazungumzia masuala kama kuongeza kima cha chini cha mshahara na kuongeza ruzuku za kijamii.
Vyama vingine viwili vya upinzani, Botswana Congress Party na Botswana Patriotic Front, vilikuwa vimeshinda takriban viti 10 kwa pamoja. Hii ina maana BDP isingefikisha viti 31 vinavyotakiwa na hivyo imeshindwa rasmi katika uchaguzi.
Mji mkuu wa Botswana, Gaborone umekuwa na utulivu tangu asubuhi ya leo Ijumaa, huku vikundi vidogo vya wafuasi wa upinzani vikisherehekea mitaani.
“Sikuwahi kufikiria ningeweza kushuhudia mabadiliko haya maishani mwangu,” alisema Mpho Mogorosi, mwanafunzi wa miaka 23 aliyezungumza na mtandao wa The Guardian.
“BDP imekaa madarakani kwa muda mrefu sana na najivunia kuwa sehemu ya watu waliowaondoa kwa ajili ya Botswana bora.”
BDP kilikuwa chama cha pili cha muda mrefu madarakani kusini mwa Afrika kupata viti vichache vya Bunge katika uchaguzi mwaka huu, baada ya African National Congress (ANC) ya Afrika Kusini, ambayo pia ilipoteza wingi wa viti baada ya miaka 30 madarakani na kulazimika kuunda serikali ya muungano.
Botswana imekuwa ikichukuliwa kuwa nchi ya mfano na yenye mafanikio ya kidemokrasia barani Afrika.
Masisi, mwenye umri wa miaka 63, mwalimu wa zamani wa shule ya sekondari na mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda wingi wa wabunge na kuhudumu kwa muhula wa pili na wa mwisho.
Hata hivyo, vyanzo mbalimbali vimesema kudorora kwa mahitaji ya almasi duniani, ambayo yanachangia zaidi ya asilimia 80 ya mauzo ya nje ya nchi za Kusini mwa Afŕika, kumeathiri uchumi na kupeperusha matumaini yake.
Pia, ukosefu wa ajira umeongezeka hadi asilimia 27, huku sehemu kubwa zaidi ya vijana wakiwa hawana kazi.
Kabla ya upigaji kura, BDP ilikubali hitaji la kubadilisha uchumi, na kuahidi kuendeleza vichocheo vipya vya ukuaji kama vile kilimo na utalii.