Serikali yataja mikakati wanawake makandarasi kupenya miradi mikubwa

Dar es Salaam. Serikali imesema ipo tayari kushirikiana na Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA) pamoja na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi wanayostahili, hususan kwenye miradi mikubwa inayoweza kuchangia kujenga uwezo wao kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa jana Alhamisi Oktoba 31, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kwenye kongamano la nne la TWCA ambako aliwakilishwa na katibu mkuu wa wizara hayo, Balozi Mhandisi Aisha Amour. Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa ‘Uwezeshaji makandarasi wanawake, kujenga uwezo wa ndani, kuleta matokeo chanya kimataifa’

Amesema Serikali imeshaanza kutoa miradi mikubwa ili kuwajengea uwezo wanawake makandarasa ambapo  kilometa 20 zitajengwa kwa kiwango cha lami huko Kongwa, mkoani Dodoma na kampuni nne za wanawake walioungana wamepewa kazi hiyo.

“Tunaamini watafanya kazi kwa waledi mkubwa, kumaliza kwa wakati na katika ubora, ili Serikali iendelee kuwapatia kazi za viwango mbalimbali,” amesema Bashungwa.

Awali, rais wa TWCA, Judith Odunga ameiomba CRB kupandisha kiwango cha ukomo kwenye madaraja yao ili kukidhi sheria iliyopitishwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo makandarasi wazawa.

Amesema hali hiyo inatokana na mabadiliko ya sheria ambayo mkandarasi mzawa anaweza kuomba kazi mpaka ya Sh50 bilioni.

Kuhusu ombi hilo, Waziri Bashungwa amesema, “tumelipokea na tutawasiliana na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) kuona ni jinsi gani itaongeza viwango vya ukomo kwenye madaraja, ili mkandarasi mzawa anufaike na sheria iliyopitishwa ya kuwajengea uwezo makandarasi.”

Pia TWCA imeiomba Serikali ilipe makandarasi kwa wakati ili ijenge uwezo kwa kukua kwa makandarasi wazawa.

“Ucheleweshaji wa malipo husababisha riba kuwa kubwa, mwihso wa malipo mkandarasi hapati faida, kwani pesa zote zinakuwa zimelipa riba ya mkopo inayochukuliwa,” amesema Odunga.

Akijibu hilo, Waziri Mashungwa amesema Serikali imejipanga kufanya maboresho katika taratibu za malipo, ili kuepusha athari kwa miradi na kuimarisha uwezo wa makandarasi wazawa.

Pamoja na hayo, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sera na miongozo ambayo itaongeza ushiriki wa wanawake katika miradi mikubwa ya kimkakati nchini.

“Ninawatia moyo muendelee kushikamana na kushirikiana, sisi kama wizara na Serikali kwa ujumla tutaendelea kuwa nanyi tukiimarisha sekta ya ujenzi na kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma katika safari hii ya kujenga taifa letu,” amesema.

Awali, Odunga amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2020, miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni taasisi za manunuzi ya umma kutotambua makandarasi wanawake waliosajili CRB kama wanufaika wa asilimia 30 ya makundi maalumu wakiwamo wanawake.

Amesema hali hiyo inachangia kupitwa na fursa hiyo ambayo inamlenga kila mwanamke, hivyo kuomba sera ya manunuzi ya umma irekebishwe, imtambue mwanamke mkandarasi mmiliki wa kampuni, ili naye anufaike na fursa hiyo itakayomuwezesha kukua kiuchumi.

Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni kukosa fedha za kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake makandarasi, ili kupata elimu ya Tehama katika mfumo wa Nest katika kuweka taarifa za kampuni na kuomba kazi, usimamizi wa mikataba, usimamizi wa miradi na utafutaji wa masoko

Mmoja wa wakandarasi hao, Hidaya Amri amewashauri wanawake kuchangamkia fursa na kuomba zabuni, wakipata wafanye kazi kwa bidi ili wapate miradi mingi zaidi.

“Siku zote unapoamua kufanya kazi usiogope, unapopata kazi moja ifanye vizuri, utakapoomba tena CV itakubeba… wanawake wasiogope, wasijione kuwa mimi mwanamke siwezi. Kwa kweli mimi katika kazi zote sijawahi kushikwa mkono, nimepata miradi ya kutosha.

“Nimejenga terminal one (ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam) nikiwa kama mwanamke, sehemu ya kuegesha magari, nenda pale terminal one utaona kabisa mandhari imebadilika, aliyefanya kazi yote ile lami, miundombinu yote, maua…yaani muonekano nimeubadilisha kabisa, kazi hiyo imefanywa na mwanamke,” amesema na kuongeza;

“Kazi nyingi za lami zimezifanya ambazo zamani kulikuwa na dhana potofu kwamba anayeweza kufanya kitu hicho ni mwanaume, ukienda pale Hospitali ya Mgulani JKT kulikuwa na udongo, barabara haifai, lakini nenda leo kuna miundombinu imewekwa vizuri,” amesema.

Related Posts