Oktoba 17, 2024, ilikuwa Alhamisi. Zilikuwa saa za mshawasha Kenya. Shauri la kumng’oa Naibu Rais Rigathi Gachagua, lilifikia hatua ya uamuzi kwenye Baraza la Seneti. Gachagua alipaswa kufika kwenye ukumbi wa Seneti kujitetea mashitaka dhidi yake.
Taarifa ikafika Seneti kuwa Gachagua ni mgonjwa. Aliumwa ghafla kabla ya kufika Seneti, akalazwa Hospitali ya Karen, Nairobi. Spika wa Seneti, Amason Kingi, akasema muda unabana. Supu hunywewa ikiwa ya moto. Kumsubiri Gachagua alone ni kupoteza wakati. Akaondolewa bila kusikilizwa.
Baada ya wajumbe wa Seneti kwa wingi wao kupiga kura kuunga mkono hoja ya kumng’oa Gachagua kwenye kiti cha naibu rais, Rais William Ruto, hakupitisha saa 24, alipeleka jina la Profesa Kithure Kindiki, kwenye Bunge la Kenya, kumwombea uthibitisho awe Naibu Rais mpya. Ni kama kata mti, panda mti.
Mambo mawili nyuma ya Gachagua kupigiwa kura ya kung’olewa unaibu rais. Mosi, ameondolewa na Seneti bila kusikilizwa na tayari mahakama imezuia kuondolewa kwake. Pili, ni historia ya mkwamo wa kuwavua madaraka magavana Kenya.
Tangu kuanza kutumika kwa Katiba ya Kenya mwaka 2010, yameshafanyika majaribio ya kuwang’oa madarakani magavana 11, lakini ni mawili tu yalifanikiwa. Wawili waliong’olewa ni aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Mike Sonko na Ferdinand Waititu, ambaye aliondolewa Kaunti ya Kiambu.
Wengine wote, kuanzia Gavana Martin Wambora, ambaye alikuwa gavana wa kwanza Kenya, kufunguliwa mashitaka kwenye bunge la Kaunti ya Embu, mpaka Gavana Kawira Mwangaza, wote uamuzi wa kuwaondoa kwenye kiti ulibatilishwa na mahakama.
Kauli za majaji zimekuwa zikifanana, kwamba mabunge ya kaunti na mabaraza yao ya seneti, hutafsiri vibaya ibara ya 181 ya Katiba ya Kenya, vilevile hutumia vibaya mamlaka yao ya kuwaondoa magavana kwenye kiti. Ibara ya 181 ya Katiba ya Kenya 2010, ndiyo inayoelekeza namna ya kuwafuta kazi magavana kupitia mabunge ya kaunti na mabaraza ya seneti.
Historia ya mkwamo wa kuwaondoa viongozi kwenye viti Kenya, upo hata kwa naibu magavana watatu, ambao michakato ilikwenda vizuri bungeni na seneti, lakini mahakama ilibatilisha uamuzi.
Kipindi hiki Gachagua ameondolewa kwenye kiti, na wakati huohuo Mahakama ikiwa imeweka zuio kwa muda, swali ni je, hayatajirudia ya magavana, majaji wakasema wabunge na maseneta waliitumia vibaya ibara ya 145 ya Katiba ya Kenya? Rais na Naibu Rais Kenya, wanaweza kuondolewa madarakani kwa utaratibu uliowekwa kwenye ibara ya 145.
Oktoba 20, 2024, nilimwona Gachagua mbele ya waandishi wa habari, eneo la maegesho ya magari, Hospitali ya Karen. Mnyonge, mpole, dhaifu, anazungumza sauti inayotoka moyoni. Ni kipindi hicho sasa hazunguki, anamkabili moja kwa moja Rais Ruto.
“Rais Ruto, kaka yangu, rafiki yangu, niruhusu niishi. Usiwasumbue watoto wangu,” alisema Gachagua. Hapo kabla, alikuwa akisema watu waliomzunguka Ruto ndiyo waliokuwa wakijenga utenganisho baina yao. Sasa, Gachagua anajua kwamba hana adui mwingine, isipokuwa Ruto.
Zile tambo pamoja wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu Kenya 2022. Walivyopambana pamoja kuingia madarakani, leo hii ni uadui kati yao. Ilitokea Uhuru Kenyatta akiwa Rais, Ruto Naibu Rais. Ungewaona wakivaa mavazi yanayofanana. Machoni walipendana. Baadaye ukawa uadui.
Kitabu nilichoandika, “Kikwete Lowassa: Urafiki, Ndoa Yao ya Kisiasa. Uadui”, kingeweza kuwa tiba kwa Gachagua. Inaonekana bado hajajua mila na desturi za mamlaka. Hatambui ushirikiano na mipaka dhidi ya mwenye mamlaka.
Thamani ya Mamlaka inazidi kila kitu chini ya jua. Dunia haijabadilika kutoka utenzi wa Theogony, uliofanywa na mwandishi wa Ugiriki ya Kale, Hesiod, Karne Saba Kabla ya Kristo.
Uranus alikuwa mtawala wa ulimwengu. Cronus ni mtoto wa kiume wa Uranus. Cronus alimwonea wivu baba yake kutokana na Mamlaka makubwa aliyokuwa nayo. Akamuua. Kisha, Cronus, naye baadaye aliuawa na kijana wake, Zeus.
Mapenzi ya baba kwa mtoto hayajawahi kushinda utamu wa Mamlaka. Mfalme wa Urusi, Peter The Great, alimuua mwanaye wa kwanza, Alexei, kwa mateso makali, Julai 7, 1718. Peter aliona Alexei ni hatari kwa utawala wake.
Mahaba ya mama na mtoto yalipotea Karne ya 17, Ufaransa, Mfalme Louis XIII alipomfukuza nchi mama yake, Medici. Ni baada ya Medici kung’ang’ania Mamlaka ya mwanaye.
Mapenzi ya mke kwa mume hayana uzani mbele ya Mamlaka. Karne ya 18, Catherine The Great, alimpindua mume wake, Peter III, akamuua, kisha akajitangaza kuwa mtawala wa Urusi.
Kama Mfalme Henry VIII alimuua kaka yake, Arthur, kisha akakubali kumwoa mwanamke asiyempenda, Catherine wa Aragon, ili awe Mfalme wa Uingereza, unawezaje kupima nasaba na mahaba dhidi ya Mamlaka?
Ikiwa ni ukweli au uongo, Ruto alishapokea taarifa kitoka Idara ya Usalama Kenya, kuwa Gachagua alishakuwa na mpango wa kumpindua. Hivyo, Gachagua anapaswa kujua kuwa yeyote aliye na mamlaka, mtazame kwa makini. Anayapenda mamlaka yake kuliko chochote.
Baba anaweza kuua mwanaye au kinyume chake, kulinda utawala wake. Vivyo hivyo, mke kwa mume, ndugu wa damu kupangiana njama za mauti, yameshatokea na mifano ni dhahiri.
Ikiwa wenye mnyororo mmoja wa damu wanageukana. Wanaochangia kitanda na kujifunika shuka moja wanapinduana. Unadhani mamlaka yanaweza kuzidiwa thamani na urafiki wa kukutana kwenye safari za kimaisha?
Nani wa kuuona urafiki ni mtamu kuliko mamlaka? Ukiyataka mamlaka, ujue yana limbwata la hatari. Yatakulazimisha uyapende yenyewe kuliko yeyote na chochote.
Mamlaka yana wivu kupindukia na hayana kawaida ya kushindwa vita ya mapenzi. Wenye kuyaendea ndivyo sivyo, hao ndiyo hushindwa, huumia au hata kuangamia.
Ni sikitiko kwa Ruto na Gachagua, urafiki wao umezidiwa nguvu, ukapigwa dafrao na wivu wa mamlaka. Hiyo ndio sababu ndoa za kisiasa hazidumu.
Ukifunga ndoa ya kisiasa, baada ya kuingia madarakani, mamlaka huchanua wivu wake, ama uchague mwenzi wako au uyape yenyewe thamani yake. Mamlaka hayatambui ndoa za mitaala. Watu wawili hawawezi kutawala kwa pamoja. Moto utawaka.
Kuna wakati Gachagua alijisahau, akadhani yeye na Ruto wanatawala Kenya kwa pamoja. Mamlaka hayapendi kuchangiwa. Kosa kubwa zaidi, Gachagua akawa anatambia kuwa jamii yake ya Wakikuyu kutoka Mlima Kenya, ndiyo imempa Ruto urais. Hii ilikuwa kushusha hadhi ya mamlaka. Ni hatari sana.