Uhondo wa Championship kuendelea tena kesho

UHONDO wa Ligi ya Championship unaendelea kushika kasi na baada ya jana kupigwa michezo mitatu, kesho itapigwa mingine miwili kwenye viwanja mbalimbali, ili kuzisaka pointi tatu muhimu za kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Mtibwa Sugar iliyochapwa bao 1-0, mechi iliyopita dhidi ya Geita Gold, itakuwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mjini Morogoro kucheza na African Sports ‘Wanakimanumanu’, ambayo hai-jashinda mchezo wowote hadi sasa kati ya sita iliyocheza.

Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, wenyeji Mbeya Kwanza iliyoichapa Stand United katika mechi iliyopita bao 1-0, itaikaribisha Bigman FC, yenye kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wao wa mwisho pia bao 1-0 dhidi ya Biashara United.

Ligi hiyo itaendelea keshokutwa Jumapili kwa michezo mitatu kupigwa na Songea United iliyotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya TMA, itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji Ruvuma kuikaribisha Mbeya City iliyotoka kuifunga Mbuni ya jijini Arusha bao 1-0.

Geita Gold itasalia Uwanja wa Nyankumbu kucheza na Maafande wa Polisi Tanzania iliyoifunga African Sports bao 1-0, mechi iliyopita, huku mchezo wa mwisho ukiwa ni ‘Dabi ya Arusha’ kati ya Mbuni na TMA, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kocha Mkuu wa TMA, Maka Mwalwisi alisema anatarajia mchezo mgumu kutokana na ukaribu na wapinzani wao huku Kocha Mkuu wa Mbuni, Leonard Budeba akieleza wanataka pointi tatu muhimu ili kurejesha morali ya timu kutokana na kuanza Ligi vibaya.

Related Posts