London. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amewaomba wakuu wa kampuni za kimataifa na wawekezaji kutumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.
January ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga, ametoa wito huo jana Oktoba 31, 2024 baada ya kushiriki mkutano wa Financial Times Africa 2024 uliofanyika jijini London nchini Uingereza kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni katika nchi hiyo.
Katika maelezo yake January ambaye ameonekana kwa mara ya kwanza kwenye majukwaa ya kimataifa tangu alipoondolewa kwenye wadhifa huo, amehimiza kuongezeka kwa uwekezaji wa moja kwa moja (FDI) nchini na kuhimiza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ili kukidhi mahitaji ya Afrika ya dola 170 bilioni (sawa na Sh459 trilioni) kwa mwaka kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu.
Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mtazamo wa mageuzi, tayari amebadilisha mwelekeo wa Tanzania tangu aingie madarakani miaka mitatu iliyopita, akilenga sera za kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI).
“Takwimu hazidanganyi… mwaka 2020 miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ilikuwa ya thamani ya dola bilioni 1 (Sh2.7 trilioni). Hadi Septemba, 2024 imefikia dola bilioni 7 (Sh18.9 trilioni). Unaweza kuona kiwango cha mafanikio ambayo Tanzania imepiga kwa haraka.”
Pia, January ameeleza kuwa fursa za kipekee za uwekezaji Tanzania, akitaja eneo lake la kijiografia, utulivu wa kisiasa, motisha za kifedha na mazingira bora ya sera na sheria.
“Tuna matumaini makubwa kuwa kwa ujumbe wa Rais Samia na msisitizo wake kuwa huu ndio mwelekeo sahihi, tunaamini mtiririko wa FDI utaendelea kuongezeka,” amesema.
Kwa upande wake mfanyabiashara Rostam Aziz ameeleza matumaini yake kwa Tanzania, akisema: “Nimekuwa kwenye biashara kwa miaka 32 na nimeona nchi ikikua kutoka msingi mdogo hadi tulipo sasa. Nina matumaini makubwa kuhusu mustakabali na ukuaji wa kasi zaidi. Ngoja muone.”
Kuhusu mkkataba wa DP World
Kuhusu mkataba kati ya kampuni ya DP World na Serikali ya Tanzania uliosainiwa Oktoba 2023 kwa lengo la kuogeza ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam, Rostam amewaambia wakuu wa kimataifa na wawekezaji kuwa uamuzi huo ulilenga kuongeza ufanisi.
“Ufanisi ulikuwa mdogo na meli zilikuwa zikisubiri baharini kwa siku kadhaa hivyo, kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na kuathiri watumiaji wa mwisho.”
Kuhusu mradi wa gesi asilia (LNG) wa dola 42 bilioni (Sh113.4 trilioni), Rostam amefafanua kuwa kucheleweshwa kwake kulitokana na juhudi za Tanzania kupata makubaliano bora ili kuepuka madhara ya laana ya rasilimali.
Rostam amesema kuwa timu ya majadiliano ya Serikali (GNT) na muungano wa wawekezaji wa kigeni katika mradi wa LNG, wakiwemo Equinor ASA, Shell Plc na Exxon Mobil Corp, wako karibu kufikia makubaliano.
“Mara ya mwisho nilipokagua walikuwa karibu sana kufikia muafaka, ingawa bado kulikuwa na masuala matatu au manne yanayojadiliwa. Nina matumaini kuwa tutafikia mwisho na kuwa na mradi,” amesema.
Hata hivyo, January kwa upande wake amekosoa upendeleo wa wakala wa alama za mikopo wa Moody’s, Standard and Poor’s (S&P) na Fitch dhidi ya nchi za Afrika.
Amerejelea ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ya mwaka 2023 ikionyesha jinsi tathmini za hatari zisizo za haki zilivyopelekea Afrika kukosa mapato na kugharimu zaidi ya dola bilioni 75 (Sh202.5 trilioni).
“Kuongeza hatari za uwekezaji barani Afrika si haki. Wafanyabiashara wanahitaji marejesho makubwa (ROI) kutoka Afrika kuliko kwingine, jambo ambalo si haki,” amesema January.