London. Waziri wa zamani, January Makamba na mfanyabiashara maarufu Rostam Aziz wamewaomba wakuu wa kampuni za kimataifa na wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania.
Wametoa wito huo Oktoba 31, 2024 baada ya kushiriki mkutano wa Financial Times Africa 2024, uliofanyika jijini London, Uingereza Oktoba 29-30, 2024 kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni katika nchi hiyo.
Katika maelezo yake aliyotoa kupitia mtandao wa Tanzania Business Insight, Makamba ametoa wito wa kuongezeka kwa uwekezaji wa moja kwa moja (FDI) nchini na kuhimiza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kukidhi mahitaji ya Afrika ya dola 170, bilioni (sawa na Sh459 trilioni) kwa mwaka kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu.
Makamba ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa na mtazamo wa mageuzi, amebadilisha mwelekeo wa Tanzania tangu aingie madarakani miaka mitatu iliyopita, akilenga sera za kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI).
Amesema, “takwimu hazidanganyi… Mwaka 2020 miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ilikuwa ya thamani ya dola 1 bilioni (Sawa na Sh2.7 trilioni). Hadi Septemba mwaka huu, imefikia dola 7 bilioni (sawa 18.9 trilioni). Unaweza kuona kiwango cha mafanikio.”
Pia ameeleza fursa za kipekee za uwekezaji Tanzania, akitaja eneo la nchi a kijiografia, utulivu wa kisiasa, motisha za kifedha na mazingira bora ya sera na sheria.
“Tuna matumaini makubwa kwamba kwa ujumbe wa Rais Samia na msisitizo wake kuwa huu ndio mwelekeo sahihi, tunaamini mtiririko wa FDI utaendelea kuongezeka,” amesema.
Kwa upande wake Rostam ameeleza matumaini yake kwa Tanzania, akisema, “nimekuwa kwenye biashara kwa miaka 32 na nimeona nchi ikikua kutoka msingi mdogo hadi tulipo leo.
“Kwa hiyo nina matumaini makubwa kuhusu mustakabali. Ngoja muone,” amesema.
Rostam pia amezungumzia mkataba kati ya kampuni ya DP World uliosainiwa Oktoba 2023 kwa lengo la kuogeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, kuwa uamuzi huo ulilenga kuleta ufanisi.
“Ufanisi ulikuwa mdogo sana na meli zilikuwa zikisubiri baharini kwa siku kadhaa, na kuongeza gharama kwa walaji na uchumi,” amesema.
Amezungumzia pia mradi wa gesi asilia (LNG) wa dola 42 bilioni, (sawa na Sh113.4 trilioni), kuwa kucheleweshwa kwake kulitokana na juhudi za Tanzania kupata makubaliano bora ili kuepuka madhara ya laana ya rasilimali.
Kwa upande mwingine, Makamba amekosoa upendeleo wa wakala wa alama za mikopo wa Moody’s Standard and Poor’s (S&P) na Fitch dhidi ya nchi za Afrika.
Akijenga hoja yake amerejelea ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ya mwaka 2023, ikionyesha jinsi tathmini za hatari zisizo za haki zilivyopelekea Afrika kukosa mapato na kugharimu zaidi ya dola 75 bilioni (sawa na Sh202.5 trilioni).
“Kuongeza hatari za uwekezaji barani Afrika si haki. Wafanyabiashara wanahitaji marejesho makubwa kutoka Afrika kuliko kwingine, jambo ambalo si haki.”
Rostam alikubaliana na Makamba katika hilo, akieleza kuwa, ingawa Afrika ina kiwango kidogo zaidi cha kushindwa katika malipo, lakini bara hili bado linaadhibiwa na viwango vya juu vya riba.
“Afrika ina uwezekano mdogo wa kufeli lakini bado tunaadhibiwa na riba za juu. Hii ni changamoto tuliyonayo hapa.”