Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema vijana wanapaswa kuipenda nchi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa moyo wote na kuwa tayari kulilinda Taifa kwa gharama yoyote kama alivyofanya Jenerali mstaafu David Musuguri.
Amesema Watanzania wote wanapaswa kujitoa, hata ikibidi kufa kwa ajili ya kulinda na kutetea uhuru, heshima na masilahi ya Taifa.
Amesema hayo leo Novemba Mosi, 2024 wakati wa kuaga mwili wa Musuguri, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi nchini katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Musuguri (104) alifariki dunia Oktoba 29, 2024 mkoani Mwanza katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando akipatiwa matibabu.
Dk Mpango amesema makamanda na wapiganaji waliopewa dhamana ya uongozi katika Jeshi, hawana budi kuendelea kufuata mfano bora ulioachwa na Musuguri.
Amesema alilipenda jeshi maisha yake yote na alitamani vijana wengi wajiunge nalo hivyo, aliwaandikisha jeshini vijana wengi akiwa mwalimu na mlezi makini wa askari vijana.
Dk Mpango akimzungumzia Musuguri atakayezikwa Novemba 4, 2024 kijijini kwao Butiama mkoani Mara amesema; “Hayati Jenerali mstaafu Musuguri alilipenda jeshi maisha yake yote, leo asubuhi kijana wangu alikuwa ananiambia kabla ya kujiunga na jeshi alikuwa anajua David Musuguri ni cheo cha kijeshi.”
Amesema Musuguri alipopewa jukumu la kuongoza jeshi alifanya jitihada za kuliendeleza kuwa bora barani Afrika.
Alitoa mfano wa namna alivyoongoza jeshi katika vita vya Kagera kumng’oa Idi Amin Dada alipovamia eneo la Tanzania
“Inatupasa Watanzania wote askari na raia kujitoa na ikibidi kufa kwa kutetea na kulinda uhuru, heshima na masilahi ya nchi yetu. Rai yangu kwa vijana wa Tanzania ni kuipenda nchi yetu na jeshi letu kwa moyo wote kwa gharama yeyote,” amesema.
Mkuu wa majeshi wa kwanza, Jenerali mstaafu, Mirisho Sarakikya amesema Musuguri alimfahamu tangu mwaka 1961 na ndiye aliyempokea jeshini.
Amesema alimuonyesha njia ya maadili akisema wao ndio walioanzisha jeshi jipya, akimsifu Musuguri kwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
“Alikuwa mtu makini na mwenye busara, ushawishi na rafiki wa kila askari, kilichomsaidia kupanda kuwa Mkuu wa Majeshi ni upendo,” amesema.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema kumbukumbu za Jenerali mstaafu Musuguri zitaendelea kudumu milele.
“Alisimamia jeshi kipindi cha vita na amani, kifo chake kimeacha pengo kwa Taifa,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920 katika Kijiji cha Zanaki, Kata ya Butiama Muhunda, wilayani Musoma mkoani Mara, na alipata elimu katika ngazi mbalimbali.
Alijiunga na Jeshi Agosti 9, 1943. Alihudhuria kozi mbalimbali ikiwemo ya Effendes mwaka 1959 hadi 1960, Nakuru nchini Kenya. Alitunukiwa kamisheni Februari 6, 1962 na alihudhuria Kozi ya Ukamanda na Unadhimu mwaka 1975 hadi 1976 nchini China.
Katika kipindi cha utumishi wake jeshini alipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali hadi cheo cha Jenerali Aprili 26, 1985. Alilitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 45 na siku 24.
Katika utumishi wake jeshini, aliwahi kushika madaraka kadhaa yakiwemo Mkuu wa Utumishi Jeshini 1972, Kamanda Brigedi mwaka 1974, Kamanda Divisheni ya 20 mwaka 1978, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) mwaka 1980 hadi alipostaafu jeshini kwa heshima Septemba Mosi, 1988.
Kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kulitumikia Jeshi na kulinda Taifa, Rais na Amiri Jeshi Mkuu alimtunuku medali mbalimbali ikiwa ni pamoja na Medali ya Vita vya Kagera, Miaka 20 ya JWTZ, Utumishi Mrefu Tanzania na Utumishi Uliotukuka Tanzania.