TARI YAWAKUTANISHA WADAU WA AFYA YA UDONGO

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewakutanisha wadau mbalimbali wanaojishughulisha katika mnyororo wa thamani wa afya ya udongo ili kubaini changamoto za afya ya udongo zinazowakabili Wakulima pamoja na kuweka njia sahihi na endelevu za kutatua changamoto hizo kupitia mafunzo.

Hatua hiyo ni Utekelezaji wa Mradi unaolenga kujenga uwezo wa kitaasisi kwa Watafiti na maafisa ugani, pamoja na mafunzo kwa Wakulima juu ya afya endelevu ya udongo katika zama za mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo wa miaka minne (2024-2027) unatekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) na Taasisi ya Norwegian Institute for Bio economy Research (NIBIO), kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo la Norway (Norad).

Akieleza kuhusu mradi huo Dkt. Atugonza Bilaro, ambaye ni mratibu wa Mradi na Mtafiti kutoka TARI, amesema Wilaya tatu za Tanzania bara ambazo ni Kongwa na Babati kwa Mkoa wa Dodoma, Mbozi- Songwe pia Zanzibar katika visiwa vya Pemba na Unguja ndio maeneo ambayo mradi huo utafanyika.

Mradi huu unakuja na njia husishi ya Maabara hai ya afya ya udongo ambayo inajumuisha Wataalamu mbalimbali kutoka Taasisi tofauti za umma na binafsi wenye lengo Moja la kutatua changamoto za afya ya udongo ili kumuongezea Mkulima tija.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa wadau, uliofanyika Oktoba 31, Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana amesema Maabara hai ya afya ya Udongo inalenga kutatua changamoto mbalimbali za afya ya udongo lengo ikiwa ni kumsaidia Mkulima kupata tija bila kuingia gharama zisizo lazima.

“Tukiwa na uhakika wa afya ya udongo maana yake tunaenda kumsaidia Mkulima kutambua namna sahihi ya matumizi ya viuatilifu, mbolea na Pembejeo zingine hata aina ya zao linalofaa eneo husika” Amesema Dkt. Bwana.

Naye Mkurugenzi wa NIBIO, Profesa Udaya Sekhar, amesema suala la afya ya udongo ni muhimu katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Profesa Sekhar amesema kama suala la afya ya udongo halitaangaliwa kwa uzito unaostahili matokeo yake tija kwa Mkulima itapungua na hata kuhatarisha suala la usalama wa chakula.

TARI na NIBIO wamekuwa na ushirikiano katika suala la Utafiti wa Kilimo ambapo mradi mwingine unaotekelezwa na Taasisi hizo mbili ni mradi wa Kilimo shadidi cha Mpunga.
 

Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Thomas Bwana akizungumza na wadau wa afya ya udongo Jijini Dodoma.
 

 Picha ya pamoja ya wadau wa utafiti wa afya ya Udongo walipokutana jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Thomas Bwana akizungumza na wadau wa afya ya udongo Jijini Dodoma.

Related Posts